Filed under: Maoni ya jumla
Hivi majuzi, nilishangaa mno kuona vioja vikitendeka hapa Nairobi. Mimi ni mpinzani mkubwa wa serikali hii iliyopo na ile iliyokuwepo kabla ya hii. Sababu yangu ni kwamba sioni tofauti yoyote kati ya serikali hii na ile iliyopita kama utahesabu mambo kama vile kuwajibika, kufuata na kuzingatia sheria, kuwa na dhati katika vita dhidi ya umasikini, maradhi, ukabila, rushwa na kutenda kazi kwa uaminifu na inavyotakikana.
Wakati wa utawala wa KANU, tulishuhudia watu wakivunja sheria na kuachwa kujisikia vizuri na utamu na uhuru pamoja na wapendwa wao. Kisa na maana? Walikuwa upande ufaao wa chama tawala.
Wakati Kibaki alipochukua kiapo cha kuitawala nchi hii, nakumbuka akipaaza sauti yake kwenye kipaza sauti akitangaza mwisho wa mambo fulani. Mojawapo ilikuwa ni uongozi wa mtu mmoja, ambapo mambo fulani makubwa yanayohusu sera hayafanywi tu kiholela barabarani. Kwa maneno yake mwenyewe, Kibaki aliharamisha ‘maazimio ya barabarani’. Haukuwa muda mrefu tulipomwona katika kibonzo kwenye gazeti moja la humu nchini, akiwa kama mwanafunzi ambaye alienda shuleni, na baada ya kupewa matokeo yake ambayo alifaa kuyalinganisha na majukumu yake, alirarua hiyo ripoti na kuendelea kujikongoja kwa mkwaju wake wa kucheza golfu, huku akipiga mbinja ni kama kwamba hakuna lililotendeka.
Wanupinzani wamekuwa wakilalamika (na wana haki ya kufanya hivyo) kuwa serikali hii ina kiburi mno. Na hilo ni jambo la kweli. Watazame tu mawaziri wetu. Utafikiri ni viumbe walioumbiwa kwenye chemba maalum kwenye mastakimu ya mfinyanzi mkuu aliyewafanya hao. Utadhani kwamba utawala wao ulitoka kwa Mungu, bali si kwa hawa watu kina yahe ambao wamebaki kuashama kwa njaa na magonjwa, huku kila aina ya tahadhari ikichukuliwa ili kuhahikikisha starehe na ulimbwende wa watawala wetu. Rais anajulikana wazi kwamba ana kimada, ambaye watu walio karibu naye wameamua kumwita mwanaharakati wa chama cha NARC (sasa ni NARC-Kenya) ambaye tunamlipia mpaka ulinzi wa polisi wa umma! Rais aliharamisha wabunge na viongozi wa serikali kuongoza mikutano ya harambee. Huku wahudumu wengine wa serikali na bunge wakiwa wamefungwa mikono, rais, kupitia nyumba ndogo, anaendelea kumwaga pesa.
Juzi tu, rais alisema kwamba anashangazwa na kuudhiwa na wanasiasa wa upinzani ambao tayari wameshaanza kupiga kampeni. Jambo ambalo hakutuambia ni kwamba yeye kampeni zake zilianza mwaka wa 2003 mara tu ya kuchukua hatamu za uongozi na kusahau ahadi zake kwa Wakenya kama rais atakayetuunganisha kama Wakenya, na kutuongoza kwenye barabara ya fahari inayoelekea mustakabali wa ufanisi. Badala yake amekuwa ndiye fisi mkuu na mlinzi nambari moja wa nunda mla watu.
Huku mawaziri wakilewa kiburi, ninashangaa kuwaona vigogo wa upinzani nao wakionyesha sifa za kinyonga kama za serikali.
Reuben Ndolo, mkosoaji mkuu wa serikali alikuwa kwenye habari juzi akikwepa kukamatwa na polisi kutokana na matumizi yake ya pesa za hazina ya usitawishaji maeneobunge. Ni kwa nini viongozi wa upinzani waende kuzingira nyumba ya Ndolo ili kuwazuia polisi kumkamata? Huu ni upuuzi mtupu. Ikiwa upinzani una haja ya kuwa chaguo bora kuliko serikla iliyopo sasa, ni lazima waanze kuonyesha dalili sasa. Kumkubalia tu kila mwizi kwa sababu yeye huongoza nyimbo za kuipinga serikali katika mikutano ya upinzani. Itakuwa bora ikiwa upinzani utamwepuka na kumkana mtu yeyote ambaye ataonekana kuwa na dosari hasa kutokana na matumizi mabaya ya pesa za wapiga kura.
Ni aibu kuona kuwa wale wanaotarajia kuunda serikali bora zaidi ya ile tuliyo nayo, nao wamekuwa ni wa kutetea wezi wa upande wao, huku wakipiga kelele kubwa kwa kutaka mchunguzi wa mambo ya ufisadi kuwachukulia hatua kali wale waliotajwa kwenye visa vya ufisadi kutoka upande wa serikali. Ni ya aina gani hii sheria? Ni maadili ya namna gani haya? Ilhali tunaambiwa kwamba uchaguzi mkuu ujao utakuwa kati ya ‘farasi wawili’, yaani ODM-Kenya na NARC-Kenya! Nakuhurumia ewe Mkenya!
Filed under: Hadithi Fupi
Ndugu na kina dada tunaokumbana katika uwanja huu. Nimekuwa kimya kwa muda kutokana na mambo kadha wa kadha, uvivu ukiwa ni mmojawapo, uandishi katika nyanja zingine pamoja na mbio kali za kusaka mkate na maji.
Nipo hapa na ningelipenda kuitikia salamu zenu nyote na kusema kwamba ni mwanzo mpya ambapo kublogu kutakuwa ni mionogni mwa mambo ya kimsingi kama ugali na maji.
Asanteni na karibuni sana, huku nikiahidi kwamba nitatoa jasho zaidi la moyo wangu hasa ikikumbukwa ya kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi nchin mwangu.
Tuko pamoja!
Amadi.
Filed under: Maoni ya jumla
Miezi michache iliyopita, ulimwengu uliadhimisha miaka ishirini na mitano tangu kugunduliwa kwa hali ya UKIMWI. Kuna mazoea ya watu kuiita hali hii ugonjwa. Madai yangu ni kwamba hii ni hali bali si ugonjwa. Ni hali ambayo huufanya mwili kupungukiwa na kinga na kuruhusu vimaradhi ambavyo kwa kawaida ni vya kuwinga tu, kuwa na uwezo wa kusababisha kifo. UKIMWI ni hali ambayo tumekuwa nayo kwa hicho kipindi kiasi kwamba kama angelikuwa ni mtoto, basi angelikuwa tayari ameshatupatia mjukuu. La kusikitisha ni kwamba, licha ya kipindi kirefu cha kuishi na hali hii pamoja na masaibu yake, bado tunaonyesha kiwango cha chini mno cha uelewa.
Unyanyapaa
Wakati kongamano likiendelea nchini Canada, kuna madaktari ambao walikutana mjini Nairobi. Miongoni mwa hawa madaktari walikuwa na mawazo ambayo yalinifanya kupigwa na butwaa. Kundi moja lilidai kwamba kutengenezwa na kusambazwa kwa madawa yanayopunguza makali ya virusi vya UKIMWI ni jambo baya sana. Kulingana na kundi hili la madaktari, hali ya kutumia madawa na kurejesha nguvu mwilini ni mbaya sana. Eti wale walioambukizwa viini hivi huwahadaa watu walio ’sawa’ kwamba wao ni watu sawa na wao, hivyo basi kuwaambukiza kiholela! Rai yao ni kwamba heri tungeliwaacha wahasiriwa wafilie mbali kwani wanastahili kufa. Haya ni mawazo yaliyojaa unyanyapaa. Ninashindwa kuelewa ikiwa madaktari wana mawazo kama hayo, basi watu wa kawaida nao watakuwa na mawazo ya namna gani?
Miaka kumi na saba nyuma
Nakumbuka miaka kumi na saba iliyopita wakati nikiwa shuleni. Tulisikia kwa mara ya kwanza kwamba UKIMWI ulikuwa umetufikia kwenye ujirani wetu. Hapo awali, tulikuwa tumefundishwa shuleni kwamba kulikuwa na ugonjwa ambao ulikuwa ni wa wasenge. Ninafikiri ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kusikia neno hilo ’usenge’ na halikuwa na maana sana kwangu. Sikujua ni nini na mwalimu wetu alichukua muda mrefu kujaribu kutuelezea (wakati huo tukiwa shule ya msingi kule mashamabani) hali hiyo na inavyoamili. Tuliambiwa kuwa ilikuwa ni hali ya mazoea ya Wazungu. Basi niliwashangaa sana Wazungu. Sikudhani kama kwetu pia tunayafanya mambo kama hayo. Tulipunga mikono na kusema kuwa tungelijali mambo hayo siku ile tutakayofika Ulaya, kwani sote tulikuwa tunasoma kwa bidii ili tufike Ulaya.
Jirani mhasiriwa
Basi fununu zilianza kutanda kijijini kwetu kuhusu huyu jama ambaye alikuwa jirani yangu na ambaye alikuwa ameishi Nairobi kwa miaka kadha. Alirudishwa nyumbani akiwa amenyauka kweli. Watu walisema kuwa alikuwa na ule ugonjwa ’uliokuja kwa meli’. Tuliogopa kuutaja ugonjwa huo kwa jina lake kamili kwa kuwa tuliogopa kuwa kama nyoka anayetajwa kwa jina usiku, tungeliuchochea kuja karibu nasi kwa haraka. Watu walitazama kando kwa kando. Majirani tukawa hatuingii mji huo kuomba maji tena. Njia iliyokuwa ikipitia mjini humo kama ilivyo kawaida na vijia na vichochoro vya vijijini tukawa tunaiepuka jinsi mkoma alivyoepukwa katika enzi za Yesu.
Mavuno ya kwanza
Siku ya kupumzika kwa mwenzetu ilifika. Alifariki nyumbani na sisi kama majirani tukaomba ruhusa shuleni ili kuhudhuria matanga kwani mmoja wetu alikuwa ni mpwa wake marehemu. Tulipigwa na bumbwazi tulipofika pale na kupata kaburi linachimbwa. Tangu lini kaburi likachimbwa mchana Maragoli? Sisi tulijitosa ndani ya mojawapo ya nyumba za hapo na kuendelea kunywa chai, huku tukipiga soga na kuburudika kwa muziki ambao ulikuwa umeshamiri wakati huo. Wakati tulipotoka nje, kulikuwa na kaburi bichi ambalo tayari lilikuwa limefukiwa. Mji mweupe! Isipokuwa waliofiwa ambao walikuwepo, vichwa chini. Tuliokuwa ndani tuliemewa. Kwa bahati nzuri, mahudhura watarajiwa kwenye matanga haya walipata udhuru kwani malaika wa kifo alipiga panda yake kwa jirani na wote ambao wangelikuja kulala hapa matangani kama ilivyo kawaida ya destri zetu wakapata pengine pa kwenda, na udhuru tosha wa kutowaliwaza hawa ambao walikuwa wamemzika mgonjwa aliyekufa kutokana na matatizo yaliyosababishwa na UKIMWI. Tuliokuwa ndani wakati wa mazishi tuliambiwa kwamba askari walikuja, pamoja na madaktari wakubwa ambao waliagiza kuzikwa mara moja kwa marehemu. Kwa hivyo mwili ulifungwa kwenye karatasi jeusi la nailoni, kisha madaktari wakavaa glavu, wakajipaka viuaviini, kabla ya kuongoza katika sherehe ya kumzika marehemu. Askari walikuwa tayari kukabiliana na yeyote ambaye angeingiza ndani mambo ya utamaduni. Eti mtu kuzikwa na watu wake; aka! Huyu alikuwa ni mfu hatari.Fikira zilizodumaa
Ninashangaa kuona jinsi tulivyodumaa katika mawazo, fikira na imani zetu tangu miaka hiyo. Tumefundishwa kuogopa UKIMWI. Hatujafundishwa kuuelewa. Tangu wakati huo, tumechora picha mbalimbali za wahasiriwa. Tumewaona kama jama ambao wamekondeana na kuwa na kikohozi kisichopona, huku wakiwa na majipu mwili mzima. Taswira hii imetawala fikira zetu hadi wa leo. Sasa, madaktari wetu wazuri hawataki kukubali kwamba mtu unaweza kuwa na viini hivi hatari na ukaishi maisha ya kawaida kwa tahadhari zako kwa miaka mingi. Madaktari wanataka ufe! Kitambo kidogo, nilisoma katika magazeti yetu humu nchini kuwa kuna jama ambaye baada ya kupelekwa hospitali kwa kulemewa na maradhi nyemelezi, alikaa na baadaye kidogo akaomba kurudishwa nyumbani ili kufa. Kweli, baada ya siku tatu aliaga dunia. Kisa na maana? Wahasiriwa watakwambia kwamba kila wanapoenda hospitali, waganga huwatupia lile jicho la kufifilika. Ni kama kwamba yale wanayoyapitia ni matokeo ya msiba wa kujitakia mwenyewe. Tuliuchukua UKIMWI kuwa tatizo la makahaba na watu ambao hawajijali. Watu wenye maadili mema hawakutarajiwa kupata UKIMWI. Hali hii ilikuwa ni adhabu kwa watenda dhambi. Hata makanisani, nimeshasikia wahubiri wakiwakemea watu wenye UKIMWI kwa kuwataja kama wazinzi ambao Mungu amewapiga kiboko. Juzi, mhubiri fulani alikuja mkahawani tulipokuwa tunapata chamcha na kuhuruju mno kuhusu jinisi tunavyokataa kumpa yeye sadaka ilhali tunawalimbikizia pesa watu wenye UKIMWI, kama kwamba wanafaa kupewa tuzo. Eti watu wengine wanautafuta UKIMWI kwa kuwa kuna pesa sasa. Mhubiri hakutaka kujua kama kwenye ule mkahawa kulikuwa na mtu ambaye alikuwa anaishi na hali hii. Ajabu ni kuwa, hapo mbeleni, kulikuwa na kongamano mjini Nairobi la viongozi wa kidini ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI. Wao pia?Utata wa wenye ugonjwa
Huku sisi tukiuchukua UKIMWI kuwa janga la wataleshi, Wazungu nao walikuwa na yao ya kusema. Waliona janga hili kama janga la Afrika. Hata sasa, mojawapo ya viwakilishi ambavyo vinatumiwa kuelezea Afrika ni magonjwa na hasa UKIMWI. Kwa kulitazama swala hili katika mkabala huu, tunaweza kuona ni kwa kiasi gani tumemtenga maskini mhasiriwa wa UKIMWI. Yeye ni Mwafrika mzinzi! Siku hizi, kunao makasisi ambao wanakataa kufungisha ndoa kati ya watu ambao wanajulikana kuwa na viini vya UKIMWI. Makanisa kadha huwa yanasisitiza kwamba kabla ya ndoa, wahusika waende kwenye kituo cha kupima na kuja na cheti cha kuonyesha hali yao. Kwanza, matakwa haya ni kinyume cha maadili yanayoongoza upimaji. Kupimwa kunafaa kuwa kwa hiari na kufichua kwa matokeo ni hiari ya mtu. Kimsingi, ni muhimu kwa wawili wanaotaka kuoana kujua hali yao. La kusikitisha ni kwamba, mara nyingi kupimwa huwa kunachangia kuvunjika kwa uchumba wa wawili wanaohusika. Jamii haijaweka misingi ya kuweza kuwalea watu wao hata kama mmoja wao amepatikana kuwa na hali hii. Kwa kuwatenga wenzetu, tumekuwa wa kuendeleza hali ya ubaguzi mithili ya ule wa Afrika Kusini miaka kadha iliyopita. Matendo kama haya yanaeneza hofu, hasa ya mtu kujua hali yake, kwa kuwa matokeo yakionyesha kuwa unao, basi utakuwa midomoni mwa watu, kutengwa na kubaguliwa na waganga ambao wanafaa kuwa wanajua zaidi, kupachikwa majina machafu kama vile taleshi na kadhalika. Hali hii imewafanya wahasiriwa wengi wa UKIMWI kujitia kitanzi ili kuepukana na dunia kali isiyowajali.UKIMWI waenea kama kabobo
Ni katika mkorogo huu wa imani potovu tunapopata UKIMWI ukienea kama zilizala. Watu wanapoogopa kupimwa kwa kuwa watatengwa au kuachwa, huwa wanatoa nafasi ya kueneza zaidi maambukizi haya. Baadhi ya watu wanapojua kuwa wanao, wanakuwa na hofu ya kufichua kwa kuwa wakifanya hivyo, basi watakataliwa. Mhasiriwa anapofanya juhudi za kumkinga mwenzake, kuna baadhi ya visa ambapo mwenzake huona ni kama ni yeye ambaye haaminiwi, na hivyo basi kumweka mtu katika hali ngumu ambapo ni aidha lazima atoboe siri (ambalo ni jambo gumu) au atende matendo hatari. Haya yote ukiyatazama yanakuelekeza kwenye unyanyapaa. Unyanyapaa unaeneza UKIMWI zaidi ya uzinzi na mambo mengine mengi. Wakati tunapofikiri kwamba hali hii ni shida ya wazinzi, tunakosea kwani watu wanaohusika na wazinzi wamepatikana kuchukua tahadhari kubwa zaidi kuliko wanapohusiana na wenzao wa kawaida.
Moto wawaka uzunguni
Wakati ulimwengu wa Wazungu ukikana kwamba hawamo humu, kuna moto unaofoka kwao. Wazungu wameweka vizingiti kwa wahamiaji na wasafiri wengine ambao wana haja ya kuhamia kwao kwa muda. Ikiwa unataka kwenda kusomea nchi hizi zilizopea, lazima upitie mitihani mingi. Mmojawepo ukiwa ni mtihani wa kupimwa UKIMWI ili ijulikane kama unao, ili unyimwe kibali. Hatua hii inaonekana ya kupunguza uwezekano wa kuhamisha maradhi kutoka Afrika hadi kwenye nchi za watu. Hiki ndicho kilele cha mkanganyiko. Ikiwa utafiti tunaoripotiwa unasema kwamba kunao watu ambao wameishi na hivi virusi kwa miaka thelathini sasa, ni kwa nini umnyime mtu nafasi ya kusoma kwa kuamini kuwa atakuwa mfu hivi karibuni tu? Je, ni kusema kuwa kila mtu ambaye ameambukizwa viini hivi ana haja ya kuambukiza mwenzake? Na je, unapomtenga mwenzako, una uhakika gani kuwa wewe uko salama, na utaendelea kuwa hivyo? Hivi majuzi, serikali ya Zanzibar ilianzisha mjadala kuhusu haja ya kuwataka wageni wote kupimwa kabla ya kuingia kisiwani humo. Kulingana na taarifa hiyo, wale watakaopatikana kuwa na viini vya UKIMWI hawataruhusiwa kuingia kisiwani humo. Tunaambiwa kwamba hii ni hatua ya kupunguza kuenea kwa UKIMWI kisiwani Zanzibar. Ningelipenda kuwaambia kaka zangu wa visiwani kwamba hatua yao ni ya kuendeleza ubaguzi na pia kuendeleza ujinga. Kitu muhimu ni kuwahimiza watu kuwa waangalifu na kutahadhari wakati wa kujihusisha katika mapenzi. Wasije wakawaona wageni wanang’ara wakadhani kila kitu kiko shwari. Kuzuia wageni kuingia nchini ni kulinda ujinga wa watu wenu. Tukumbuke kuwa katika kisiwa cha Zanzibar, kuna shida kubwa sana ya matumizi ya mihadarati. Hili ni tatizo ambalo linafunikiwa pazia na hakuna anayetaka kupambana nalo moja kwa moja. Pindi tunavyoendelea kubugia mihadarati, hata bandari zetu ziwe salama vipi kwa wanabeba viini, bado tumo hatarini. Pindi tunavyozidi kufanya mapenze bila kujali usalama, suluhu haipo karibu. Pindi tunavyoendelea kuwabagua wanaosheheni viini vya UKIMWI na wale ambao wana UKIMWI mpevu, bado hatuna usalama.Kipindi cha Oprah Winfrey
Jambo lingine ambalo limeziteka fikira zangu ni kuhusiana na kipindi cha Oprah Winfrey kilichofanykia hivi majuzi (angalau kimetangazwa kwenye runinga za Marekani). Kwenye kipindi hicho ambacho ninaomba kwamba kipeperushwe Kenya hivi karibuni, Oprah anawahoji watu kadha ambao wanaishi na virusi. Mmoja wao ni Magic Johnson, yule mwanavikapu mashuhuri ambaye mimi nilimjua mapema miaka ya tisini kwa kuwa alitangaza hadharani kuwa alikuwa na virusi vya UKIMWI. Matokeo hayo yalisababisha kuondolewa kwake kwenye timu ya taifa…. Muhimu ni kauli ambayo aliitoa wakati huo. Johnson alisema kwamba, unapofikiria kuhusu UKIMWI, huwa hufikirii kuwa unaweza kukupata wewe pia. UKIMWI huwa ni ndwele ya wale watu wengine tu! Je, wakereketwa wa unyanyapaa twasikia?
Tovuti na blogu za walio na virusi
Katika chakurachakura zangu, nimepata tovuti inayoitwa aidsmeds.com, ambayo inasimamiwa na kuchangiwa na watu ambao wanaishi na virusi vinavyosababisha UKIMWI. Tovuti hii huchapisha jarida pepe ambalo husambazwa kwa wale wanaotaka. Wawili kati yao walikuwa miongoni mwa wageni mashuhuri katika kipindi hiki cha Oprah. Mmoja wao ni mhariri mkuu wa jarida pepe hili na katika blogu yake, alisema: ”Watu wengi mno wanafikiri kwamba jambo hili haliwezi kuwatendekea. Aghalabu, ninapowaambia watu hali yangu, ninafikiri kuwa watu hutumia dakika kadha za kwanza kudhihirisha ni vipi nilivyo tofauti na wao-kama kwamba kwa kutambua tofauti zilizoko kati yetu ndivyo wanavyozidi kupunguza uwezekano wa wao kuwa na viini vya UKIMWI. Nikifikiri, wao huchukua muda mfupi zaidi baadaye kuchambua tafsili za maisha yao ya ngono, na kushangaa ikiwa wamejihatarisha mbele ya virusi hivi”. Nukuu hii ninaipenda kwa sababu inatuelezea sisi kama tunavyofikiria. Tunajiona kuwa watu mahususi na kuwa hiyo taabu ya UKIMWI ni ya watu wengine. Huyu dada anayezungumza ni Mmarekani mweupe. Katika dondoo lingine, dada yetu anasema jinsi alivyosisitiza kuwa anataka kiti cha ndege kando ya dirisha, wakati wa kusafiri kuelekea mahali pa kurekodia kipindi hiki. Anasema: ”Nilisema kuwa nilikuwa nina hofu ya kufa kutokana na ajali ya ndege (licha ya kuwa ni wazo la kipumbavu ukipima hatari inayohusika). Lakini nilikuwa na imani kwamba ningeliyaokoa maisha ya watu kadha ikiwa ningelitokea kwenye runinga. Na hata kama mtu mmoja tu angeliamini yale niliyokuwa ninasema kwenye kipindi hicho, angalau maisha ya mtu mmoja yangeliokolewa, na hiyo ingelifidia hofu ya kuonekana kwenye runinga.”Mhasiriwa kuwakinga wenzake
Hebu angalia jinsi mhasiriwa anavyofanya bidii ya kuwakinga watu. Hapa nyumbani, kunao watu kadha ambao wanaongoza katika vita dhidi ya UKIMWI na ambao wenyewe wanao. Je, wamjua Joe Muriuki? Huyu ni mtu wa kwanza mimi kusikia akitangaza hadharani kuwa alikuwa na UKIMWI. Hii ni kama miaka kumi na saba iliyopita. Bado yupo na anaongoza kampeni za kuhamasisha umma kuhusu hali hii. Haenezi! Yeye na mkewe ni kielelezo chema kwetu hasa kwa kupambana na unyanyapaa. Baada ya kugundua kuwa anao, mkewe ambaye yeye hana, alikata shauri kufunga pingu za maisha na mumewe! Bado wangali pamoja. Mkewe Magic Johnson pia hajamtoroka. Asunta Wagura naye ni kielelezo chema cha mtu aliye na UKIMWI, huku maisha anayaendesha kama kawaida. Ana mpenzi wake na mojawapo ya mambo anayofaidi maishani ni ngono. Rawland Lenya naye ni mfano wa mtu ambaye kimo cha mwili wake kinapinga tafsili zote ulizopewa na walimu wako kuhusu mhasiriwa wa UKIMWI. Je, watu wanaowazuia walio na virusi kuendelea na shughuli zao na kutafuta maendeleo maishani wanatoa imani zao wapi?
Filed under: Maoni ya jumla
Juzi, nilipokea habari za mkuu wa sheria Amos Shitswila Wako bila ya mshangao wowote. Wako alisema kwamba wale ambao walitajwa na tume ya kupambana na ufisadi hawangeliweza kufunguliwa mashtaka.
Kimsingi, Wako alidai kwamba hawa ni watu ambo ni wahasiriwa wa uchunguzi uliovivia. Eti uchunguzi dhidi yao ulikuwa haujakamilika na kuwa faili alizopewa zilikuwa na mashimo mengi. Kijuujuu, hii ni hatua muhimu katika uchunguzi wowote, hasa ule unaohusisha jambo nyeti kama vile wizi wa mali ya umma, ambao niliahidiwa na rais Kibaki wakati wa kutawazwa kwake kwamba ungelikumbana na adhabu kali isiyojua huruma. Hata hivyo, kama matukio ya hivi karibuni yana uzito wowote, basi ningelipenda kudai kwamba mkuu wa sheria ametufunga goli tena.
Shitswila wa Wako
Kwanza, tumchambue huyu jama ambaye jina lake la pili ni Shitswila, katika lugha ya wenyeji wa upande wake, maana yake ni kitu kinacholia kwa sauti kali. Kinaya ni kwamba, huyu ni jama ambaye daima anatabasamu. Tangu mheshimiwa tabasamu kuingia madarakani, tumejionea mambo kadha ambayo yalituacha tukijiuliza maswali kuhusu uhalali wake kuwa madarakani. Wako alikuwa mwanasheria aliyeheshimiwa
sana katika miaka ya hapo nyuma. Kulipotokea ghasia kule Timor Mashariki, ni Wako aliyechaguliwa na Umoja wa Mataifa, kama wakili anayetetea haki za kibinadamu, ili kwenda kuchunguza yaliyotokea. Habari zilionyesha kwamba wanajeshi wa Indonesia, ambayo ilikuwa imeikalia nchi hiyo kimabavu, walikuwa wamewapiga risasi watu kadha waliokuwa wanaomboleza. Wako alifanya kazi yake na ikawa nzuri.
Kiongozi wa mashitaka dhidi ya haki
Kunao wanaosema kwamba, Mungu anapotaka kumharibu mtu, kwanza humfanya kuwa mwehu (Nafikiri ni nukuu kutoka mojawapo ya tamthilia za Shakespear). Wako aliharibiwa akili na pesa ambazo aliyekuwa mtawala wa Kenya wakati huo-Daniel arap Moi- alimpatia. Wako alipewa wadhifa wa Mkuu wa Sheria. Hapo, Wako alionyeshwa mshahara mzito na marupurupu mengine ambayo huenda na vyeo nchini humu (Kumbuka majaribu ya Yesu jangwani). Domo la Wako lilijazwa chakula na akawa hana nafasi ya kuongea ila kwa kuitetea serikali. Mwanasheria wa kutetea haki za kibinadamu alikuwa mamlakani bila kulalamika katu, wakati ukandamizaji mkubwa wa kisiasa ulikuwa ukiendelea. Huyu ni mtu ambaye alikaa kitako katika ofisi isiyokuwa mbali na jumba ambamo kulikuwa na vizimba vya kuwatesa wapinzani wa serikali. Huyu ndiye mtetezi wa utu na haki ambaye alinyamaa huku haki ya kujieleza ikiwa ni haramu. Huyu ndiye mwenye haki ambaye hata hakushutumu mazoea ya kuwapeleka watu mahakamani usiku. Huyu ndiye mtu aliyeelekeza utendakazi wa watu kama vile George Omondi Tunya, ambaye ndiye aliyekuwa hakimu mkuu mkazi wa Nairobi na ambaye ndiye aliyekuwa na wajibu wa kushughulikia hasa kesi za kisiasa ambazo ziliendeshwa usiku. Huyu ndiye wakili ambaye alibadilisha neno fulani katika kifungu cha sheria ili kutoa faida kwa chama tawala KANU mara tu kbla ya kura za mwaka wa 1992. Yeye ndiye aliyekuwa akitoa uhalali kwa kazi ya watu
kama vile kina Petkay Miriti, ambao sasa ni mawaziri katika serikali hii, ambao walikuwa wahudumu katika kitengo cha utesaji wa wapinzani wa serikali kule katika jumba tukufu la Nyayo! Kumbuka kuwa Wako ndiye aliyeishauri serikali kuwa malipo yaliyotolewa kwa kampuni ya Goldenberg International, (kampuni ambayo ilikuwa ikiuza almasi na dhahabu hewa kutoka Kenya katika nchi za kigeni na kulipwa fidia nono na serikali) yalikuwa halali.
Serikali mpya iliyorithi ufisadi kwa mdadi Serikali hii ambayo inaendesha shughuli za taifa sasa, -na ambayo tumeambiwa mara nyingi kuwa ni mpya- ilipochukua madaraka, ya kututawala, ilikuwa ni ajabu kuona kuwa huyu mpiga tabasamu alikuwa bado ndiye mkuu wa sheria. Kumbe dalili ya mvua ni mawingu. Sikujua kwamba serikali hii ilikuwa inamtafuta mtu ambaye ataweka mhuri wa uhalali kwenye shughuli ambazo ni haramu!
Basi zilikuja kasheshe za Anglo Leasing na zinginezo ambako pesa ninazokatwa kila siku na serikali hii yenye uchu mwingi wa pesa, zinaishia tu mifukoni mwa matajiri walafi ambao nimelazimishwa kuwaita waheshimiwa. Katu siwaheshimu, kuanzia mkubwa wao, kupitia huyu mwingine mwanatabasamu, hadi chini kwa vibaraka wao wanaowatungia mashairi na kuwaongoa kwa maneno mazito wasiyokuwa na dhati ya roho nayo.
Injili kama ilivyoandikwa na John Githongo
Katika taarifa tuliyopewa na aliyekuwa katibu wa kudumu wa maadili na utawala Bw. John Githongo, ufisadi ni jambo ambalo limelindwa kutoka ikulu, kupitia ofisi ya mpiga tabasamu, hadi kwenye vyombo vya dola. Ufisadi wa serikali ya NARC umepigiwa ua wa ukiritimba ambako kama wewe ni yahe, basi hufai kuwa fisadi. Mwachie mbunge wako, waziri au wanaotoka katika nyumba kubwa. Ukijaribu wewe utaumia. Tunaambiwa na Githongo jinsi rais mwenyewe anavyowajua marafiki zake wafisadi na kamwe hawezi kuwafuta. Tunaambiwa pia kwamba mara tu baada ya kutawazwa, rais wangu alisahau kuwa nilimchagua kutokana na ahadi nzuri alizonipa, ahadi ambazo ziliambatana na ndoto za taifa hili nilipendalo kwa roho yangu yote. Badala yake, aliona kuwa alikuwa ameingia kwenye ghala la vinono. Alianza kupanga njama, yeye na watu wake, za jinsi ya kurudi ikulu kwa hongo. Licha ya kuwa yeye na watawala wenzake ni matajiri wakubwa, walilenga pesa ambazo zinafaa kununua madawa kwa masikini wanaoenda kwenye hospitali za umma, madawati, vitabu na vifaa vya kufundisha kwa shule za umma, kujenga barabara, kuanzisha miradi ya unyunyiziaji maji katika sehemu kame, kupambana na malaria, UKIMWI……
Mshtaki ni mmoja wao! Ripoti ya Githongo ilimtaja bwanatabasamu Shitswila kama mmoja wa wale ambao walikuwa katikati ya mduara wa maovu wa kutafuna pesa za umma. Vilevile, kiongozi wa mojawapo ya tume nyingi za kupambana na ufisadi alidhihirika kuwa kiongozi wa tume ya kutetea na kuhami ufisadi. Githongo anasema kuwa alipewa onyo dhidi ya kuwalunga sana wale mawaziri ambao walikuwa wametajwa katika ripoti yake, kwani walikuwa wameteseka vya kutosha. Utasema nini kama kuna kesi kati ya mbuzi na chui, huku chui akiwa hakimu? Je, utaamini kwamba Aaron Ringera ambaye ndiye mlinzi mkuu wa wafisadi atatoa faili inayotoa maongozi kamili dhidi ya wafisadi ambao anafanya bidii kuwaficha na kuwahifadhi? Si ajabu basi kuwa amempa mwenzake wa kutabasamu faili ambazo uchunguzi wake ni wa kutiliwa shaka. Ninaamini kuwa kwa kufanya mambo kama haya, Wako na mwenzake Ringera wangelipenda kuwachezea Wakenya mchezo wa mwajificho, ambako wanataka kupoteza muda ili tusahau kuwa tulikuwa tumewalenga wao. Hebu fikiria, Ringera ni mtu ambaye amefuzu vizuri sana katika somo la sheria. Kabla ya kuingia katika shoroba za ufisadi, Ringera alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu katika idara ya sheria. Je, huyu ni mtu ambaye hajui mchakato wa kutayarisha faili za mashitaka? Kwa ujuzi alio nao, Ringera ni mtu ambaye anafaa kuwa hakimu. Ikiwa ametayarisha faili ambazo si kamili, basi kuna jambo ambalo ni la mchezo wa ping pong ili kuwahadaa wananchi wa kawaida.
Serikali haina wezi!
Wino uliotumiwa kuandika orodha ya aibu ambayo ilisomwa hadharani na waziri wa haki na masuala ya katiba ulikuwa haujakauka wakati alipojipinda nyuma chambilecho Waingereza, na kuanza kusema kwamba miongoni mwa wale waliokuwa wametajwa (wale walioko serikalini) walikuwa hawana hatia. Yeye kama nani? Kwa misingi gani? Mbona wasifikishwe mahakamani ili vyombo vya dola vinavyotoa huduma za haki vipate kufanya kazi yao? Kwa kinywa chicho hicho, waziri na wenzake walikuwa wakipaaza sauti dhidi ya viongozi wa chama pinzani cha ODM-Kenya kuwa chuma chao kilikuwa motoni kufuatia kuwa kwao kwenye orodha ya aibu. Hebu fikiria, hata makamu wa rais Moody Awori naye alipayuka akisema kwamba wale viongozi wa ODM-Kenya waliotajwa kwenye orodha hiyo walikuwa wakikimbilia makabila yao kwa hifadhi. Je, wakumbuka yale makala ya kumtetea mwizi wa kabila langu? Je, wakumbuka ile kauli ya lero luno muri nange khandi? Aliyevua nguo huchutama bwana Awori! Usiwe nyani wa kulichekelea kundu la mwenzio. Lako pia lachukiza ajabu. Viongozi wa ODM-Kenya nao wakajipaka tope kwa kuwatetea wezi miongoni mwao wakisema kuwa kwa kuwa wao ni wafuasi na viongozi wa ODM-Kenya, basi hawangelikuwa na hatia. Katika somo la mantiki, hii ni mojawapo ya fikira lemavu na inapatikana kwenye kamusi ya fikira kama hizi. Jinamizi la Anglo Leasing
Je, unakumbuka hatima ya matokeo ya uchunguzi wa kashfa ya Anglo Leasing? Je, unajua kuwa aliyekuwa waziri wa fedha wakati wa Goldenberg George Saitoti hawezi kushitakiwa tena? Basi niambie ulitarajia nini kutoka kwa Amos Shitswila Wako? Unakumbuka usuhuba kati ya waziri Soita Shitanda na Wako? Mojawpo ya watu ambao walikuwa wametajwa katika orodha ya Maina Kiai (mwenyekiti wa tume ya kutetea haki za kibinadamu) ni Soita Shitanda. Soita alipoliona jina lake kwenye orodha hiyo, alitisha kujiuzulu ikiwa angelifikishwa mahakamani kwa kosa la udanganyifu ambao ulifanya serikali kumlipa pesa asizostahili. Wako alisema kwamba atachanganya sheria na huruma. Basi Shitanda aliambiwa kuwa alikuwa ametenda jambo lisilostahili kushitakiwa. Je, hujaamini kuwa ufisadi ni biashara kiritimba ya viongozi wa serikali? Tayari, Waluhya wameanza kusema kuwa Wako anaingiliwa kwa sababu watu fulani hawataki Mluhya kuwa Mkuu wa Sheria. Nani kasema kuwa Uluhyani kuna mwanasheria mmoja tu na kuwa kama huyu tuliye naye akiondolewa basi hakuna mwingine? Mbona tuwapatie watu yai bovu wakati tukiwa na mayai mengi mazuri? Waluhya tunafaa kukubali ukweli kuwa Wako ni mtu anayetuaibisha. Katika malezi yangu ambayo yalikuwa na kiasi cha ukereketwa wa Kiluhya, sikuwahi kumwona mzazi au mlezi aliyenishauri kuwa wizi, udanganyifu, unyama na ubatili wa haki ni maadili mema! Jitu bovu ni bovu tu, liwe la kabila langu au la kabila ninalosikia kwa mara ya kwanza tangu kuumbwa. Nimfuate Mudavadi Kamiti!?
Tayari nimeanza kupokea ujumbe mfupi kwenye simu yangu, unaonihimiza kumfuata Musalia Mudavadi kwenye jela ya Kamiti, ikiwa atahukumiwa kifungo kwa dhambi alizonitendea alipokuwa waziri wa fedha. Kwani mimi ninajichukia kiasi gani mpaka nimshangilie mwanakabila langu anaponinyonya bila aibu? Chambilecho Socrates kwenye kitabu chake kiitwacho Jamhuri, tayari, nimeukana wendawazimu!
Filed under: Mashairi
Mpenzi mwandani mahabubu
Naanza kwa kukuomba samahani
Kuandika kwa lugha hii legevu
Nilijaribu lakini sikuweza
Kuyasarifu maneno matamu
Kwa lugha muafaka ya kimapenzi
Mara nyingine ninaahidi
Kutakalamu kwa lugha inayofaa
Bidii nitafanya
Kuyaelewa machungu na matamu yangu
Kwa lugha tukufu isiyo yangu
Badala ya hiki kishairi duni,
Nitakwandikia poem
Nitajitahidi mpenzi
Maneno kuyaelewa
Si kwa jicho la kwangu kijijni
Bali kwa mboni na urazini wa kule kulikotukuka
Nitayatongoza machozi yangu
Kububujika kwa vokali na konsonanti za kimombo
Makali ya moyo wangu kulipuka kwa Kireno,
Kitaliani au Kituruki
Badala ya huu msamiati nilokujazia hapa,
Nitakuwa na vocabulary Mpenzi nitakusifu
Kwa majina ya mimea, wanyama na ndege
Wasiopatikana kwetuNitakutungia koja
Nilirembe kwa vito na maua ya nchi za baridi
Au mimea ya jangwaniNisamehe kwa sasa mpenzi
Naikumbuka tu lugha yangu
Ilonitoa tumboni mwa mama
Ninajua mpenzi
Ni vigumu kwangu kujieleza
Vigumu kwako kuelewa
Nyimbo za nyumbani kwetu kijijini
Ambako tulitembea pamoja tukivikwea vilima
Mikono yetu ikiwa kama sumaku na chuma
Ni vigumu mpenzi
Wewe kuzikumbuka zile harufu
Za mimea iliyotushangilia
Katika sherehe yetu ya mahaba na huba
Samahani mpenzi
Nimeianza barua hii kwa jina lako la kwanza
Wewe kwako ndilo jinalo la kati
Lililotumika kule nyumbani
Kabla ya kuujua mji,
Ugeni na ustaarabu wake.
Nitakuita kwa jina ajualo nyanyako kutamka
Nitajitahidi mpenzi
Kukujua kwa jina lako la mjini, dini na usasa wake
Niwie radhi mpenzi
Nitasema nawe kwa sauti
Wanaokuona na kukusikia laazizi
Wajue asili na usuli wako
Kwa muda wasikunasibishe
Na ungwana wa lugha uliyoizoea
Kwa mishangao waashame
Badala ya salaale
Wamake na kubweka ’gosh’!
Ningelipenda kuahidi kwenda nawe kupata mlo
Lakini natanguliza samahani
Ni haja yangu kukupeleka kula pizza
Lakini nimetafuta jinale katika lugha yangu
Nikakosa kabisa kabisa
Kwa hivyo mpenzi
Samahani zangu zikitangulia
Nakuahidi ugali wa wimbi
Samaki wa kuchemsha
Na mkunde wa kibakuli cha kando
Mpenzi hitari kula mtori
Jasiri pia kuonja makande,
Rojo la mrenda,
Mukimo na muthogoi.
Tutakula pia sageti,
Managu na wenzao.
Tutanyunyiza mafuta
Matamu ya samli,
Kisha tummemene tombo,
Alochomwa kwa makaa.
Jioni tutakaa
Chini ya uso wa mbalamwezi
Tukichoma ndizi,
Viazi na mihogo
Anga zitachanua
Kwa thureya ya nyota
Zikiimba wimbo bora
Wa mapenzi motomoto
Hewani kutafukizwa,
Uturi wa manukato
Ya samadi kavu inayoungua.
Samahani mahabubu,
Ingawa utatamani,
Kifukuza mbu muafaka,
Hii mwandani, haina viletamaradhi.
Sikio letu kichuna,
Tutamwazima bibi,
Babu akiwa mwenzake
Fikira zetu tuwape pia
Kutusafirisha mbali
Watupatie paukwa pakawa
Za miaka hii na iliyokuwa
Samahani mpenzi
Yameniishia maneno
Nimeyatesa macho yako,
Masikio na fikira zako
Misri kukurudisha
Japo kwa muda kidogo
Nikuandikiapo mara nyingine,
Nitakupeleka Zayuni
Kwenye miji mikuu ya utandawazi.
Amadi
Filed under: Maoni ya jumla
Kujiwachilia
Kuna baadhi ya masaibu zangu ambao mimi hujumuika nao katika utundu wa hapa na pale. Wakati huu, inaaminika kwamba watu huwa wanataka kujihusisha katika utundu kwa sababu ya kutulia na kusahau mawazo ya kina.
Kama wasemavyo Wakenya, watu huwa wanataka ‘kujiwachilia’.
Kwa bahati mbaya, huku kujiwachilia huwa hakufanikiwi wakati nikiwa na watu fulani. Tukiwa pamoja, huwa tunataka kuswali kila kitu kwa kina na mapana yake. Ni kutokana na vikao hivi ambapo zimezuka hadithi na mitazamo ambayo tunataraji kuichapisha chini ya anwani ya lugha ya wenyewe “Looking at the World from Down Under”. Hii ni mitazamo ambayo inaelekea kwenye ulimwengu wa kufikirika na kuangalia mambo kama jinsi yangelifanyika. Huwa pia ni wakati wa kuchora taswira ambayo inaweza kuyaelezea mazingira yetu kwa uwazi na ujasiri zaidi.
Faru Hamsini
Ni kutokana na mojawapo ya vikao hivi kulipozuka taswira ambayo ilisema hivi:Waafrika tumezingirwa. Sisi hali yetu ni kama ile hali ya mtu anayejipata peke yake msituni, akiwa amekabiliwa na faru hamsini; wamemweka katikati, wakiwa umbali wa mita hamsini kila mmoja na pembe zake zikiwa tayari kukita. Hizi mita hamsini ni za kuwawezesha kupiga kasi na kumdengua mhasiriwa vilivyo.Kauli hii iliniacha nikiwa ninawaza zaidi. Ni kwa nini picha inayotuelezea sisi iwe kali na ya kutamausha kiasi hiki? Basi katika pitapita na donoadonoa zangu za kujaribu kupata maarifa zaidi, nilikumbana na mambo mawili ambayo yalinifunulia ukweli kwamba huenda kauli hii ikawa ni ya ukweli. Ni dhahiri kwamba kuendelea kuwa hai kama Mwafrika mwenye heshima na fahari yako ni jambo gumu sana. Kumbuka mambo ambayo yaliwahi kuwafika wale Waafrika ambao walikataa. Tazama masaibu ya wapiganiaji uhuru kama vile mashujaa wa Mau Mau. Hawa ni watu waliojitolea na kuyahatarisha maisha yao ili kutukomboa. Walikataa. Sasa hivi, wao ni masikini wa sina sinani. Wale waliokataa kama vile Marehemu Bildad Kaggia vile vile walijipata wakiwa kwenye Saiberia ya kisiasa; kama wasemavyo katika hiyo semi ya Kirusi.Marais wa Afrika ambao walikataa kumfuata mzungu kikondoo na wakasisitiza fahari ya Mwafrika wote walishughulikiwa. Kumbuka Lumbumba alivyouawa kinyama na kuyeyusha kwa chachu! Mkumbuke Thomas Sankara wa Bourkina Faso. Mifano ni mingi.
Mambo mawili yanayovuta nadhari
Hata hivyo, sinuii kuzungumzia marais ambao walidenguliwa na ulimwengu wenye nguvu kwa kosa lao la kuwatetea watu weusi. Niliguswa mno na mambo mawili katika majuma machache yaliyopita. Kwanza, ilikuwa ni ripoti katika mojawapo ya magazeti ya humu nchini Kenya, ambayo ilizungumzia mambo kuhusu maradhi na vile mataifa yaliyoendelea yanavyotufanyia mzaha sisi kama Waafrika. Pili ilikuwa ni mswada wa sheria ambao uliwasilishwa bungeni mwetu hivi karibuni na kupelekea wanaharakati kuandamana mjini nje yao majengo ya bunge.Kwanza, ni swala la magonjwa. Je, ulijua kwamba katika ulimwengu, kunayo magonjwa ambayo ni magonjwa ya maeneo fulani? Je, wajua kwamba mataifa yaliyoendelea na makampuni ya kutengeneza madawa huwa yana haja nayo sana? Ni kweli kwamba mashirika haya pamoja na vyuo na wataalamu wa nchi zilizoendelea wana hela za kuwawezesha kufanya utafiti. Kwa hivyo janga linapotokea katika mataifa ya Kusini kama yanavyoitwa haya mataifa yetu ya hela za madafu; wataalamu hawa hukimbia mbio na kuingia kwenye mataifa haya tayari kutafiti. Wingi wa utafiti hufanikiwa na dawa kupatikana. Jambo la kusikitisha ni kwamba, hata baada ya dawa kupatikana, shida huendelea kuwakumba watu wa mataifa haya kwa kuwa kifo huwa kimewakodolea macho makavu. Kisa na maana? Watafiti hawa kutoka nchi zilizotukuka huwa wanachukua hati miliki ya madawa haya na hivyo kuwazuia wanachi wa mataifa madogo kuzalisha dawa hizi. Kutokana na akili zao za kibepari, watu ni nyenzo ya kibiashara. Ikiwa uwezo wa kibiashara si mkubwa katika kuzalisha kitu fulani, huwa hakuna haja ya kuingilia shughuli kama hii ya uzalishaji. Ndio, ni takwa la kimsingi kwa ubepari kutegemea faida. Lakini ni utu gani kuzuia uokoaji wa maisha?
Hati miliki
Je, wajua kwamba kuna madawa fulani ambayo yamepewa ulinzi wa hati miliki kiasi kwamba hata ninyi mkiitaka hati miliki hiyo kwa kukodi au kununua, hamuwezi kupewa? Jiulize haja hapa ni nini? Hebu fikiria na ujaribu kupata urazini ulioko katika hali hii hasa ukizingatia kwamba vingi vya vyanzo vya dawa hizi ni vyetu hapa! Ikiwa chembechembe za mkafuri, mkinduri au mwasumini ambao unaota kitaluni mwako zitahifadhiwa kwa hati miliki, je, kuna haki gani? Fikiria kwamba miti ambayo wazee wetu wamekuwa wakihifadhi kwa karne na karne wakifanyia ibada zao chini ya miti hii, sasa iko mikononi mwa watu ambao wanajali tu faida ya pesa ambayo wanataka kupata. Sasa ikiwa chembechembe za miti zitawekewa ulinzi wa hati miliki, basi tunayo miti ya kikwetu kweli?
Magojwa madogo na makubwa
Ndiposa unapata kuna magonjwa kama vile kalaazar na mengineyo, ambayo yanapatikana tu kwenye mataifa haya yetu, na ambayo wenzetu washajua tiba yake, lakini kwa sababu hati miliki wanayo wao, sisi twaendelea kufa tu kwa sababu haina faida kwao ikiwa tutapewa nafasi ya kujizalishia dawa. Kumbuka kwamba uwezo wetu wa kuzalisha dawa ulipigwa fimbo kwa kuambiwa kwamba waganga wetu ni wachawi. Tulisema Haleluyah na kukimbilia kanisani na misikitini na kusubiri dawa kutoka kwa wale waliotufundisha kujidharau. Sasa wakati tukiwa tumefumba macho yetu na kuwasubiri kumaliza sala, tunapata ni hii hii tu miti na magugu yetu ambayo yanatumiwa kutengenezea dawa, na yamemilikiwa! Hata katika taasisi zetu za utafiti, utapata kuwa kunao wageni wengi sana ambao wanakuja kuhudumu ndani. Jiulize ni kwa nini shirika kama vile KEMRI (Taasisi Ya Utafiti wa Kimatibabu ya Kenya) linapendwa sana na wageni. Utapata kwamba taasisi hii inapewa hela nyingi sana na wageni ambao wanazifuata ili kuja kuwa watafiti wakuu. Haja hapa ni kwamba kila matokeo yatakayopatikana yatakuwa na mvutano wa umiliki. Je, unacho kisa cha yule mtafiti wa
Cameroun kwa jina Victor Anomah Ngu? Huyu ni professa ambaye amefanya uchunguzi na kupata majibu fulani kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI. Mara tu walipojua wageni kwamba ana kitu
kama hiki, walikuja na kuomba kwamba washirikiane. Kufumba na kufumbua, ujuzi wake ulikuwa tayari umeshakuwa mali ya Mfaransa.
Vita juu ya umiliki wa madawa
Hapa nyumbani, kuna Authur Obel ambaye alifanya utafiti kwa kushirikiana na Dr. Davy Koech na wakazalisha dawa fulani ambayo waliiita Kemron. Kulitokea ugomvi mkubwa kutokana na dawa hii mpaka ikapigwa kumbo na kuondolewa sokoni. Kisa na maana? Ikiwa dawa hii ingelizalishiwa tu hapa Mbagathi na kusambazwa, soko la makampuni ya kuzalisha madawa la Afrika Mashariki na kati, na hata Afrika Kusini lingelikuwa nimechukuliwa. Vita vilizuka na kusema kwamba hiyo haikuwa tiba. Nani amesema kwamba sumu tunayoletewa na makampuni ya kimataifa ni dawa? Fikira zao zilikuwa kwamba kwa kuwa eneo hili (Afrika Mashariki, Upembe wa Afrika, Afrika ya Kusini) ndilo lililo na asilimia sabini ya wahasiriwa wa UKIMWI ulimwenguni. Hili ni soko kubwa sana kwa haya madawa ya kuja kwa meli na ndege. Vipi Wakenya wapewe ufunguo wa soko hili muhimu? Baadaye nilisoma katika vyombo vya habari kwamba Kemron, dawa iliyokataliwa hata na rais mwenyewe ilikuwa imerudi, kwa jina tofauti lakini kutoka Australia. Niambie kama huyo si faru aliyekulenga ewe Mwafrika?
Makahaba wetu, dawa si yetu
Tunakumbuka ule mvutano uliokuwepo kati ya watafiti wa Uingereza na maprofesa wa Chuo Kikuu cha
Nairobi kuhusiana na chanjo ambayo ilikuwa ikijaribiwa kutokana na utafiti uliofanyiwa makahaba wetu hapa nchini Kenya katika mtaa wa Majengo mjini Nairobi. Maprofesa hawa wa Uijngereza walichukua matokeo ya utafiti na wakaanza kuuendeleza, huku watafiti awali ambao walikuwa ni wasomi Wakenya wakiwa wanachukuliwa kuwa watu wa mkono tu.
Waliomakini wanunuliwa
Niliwahi kuwa na mazungumzo na daktari mmoja wa madawa ya kienyeji ambaye pia anazingatia
sana uchunguzi na matendo ya kisayansi kulingana na wazungu. Mganga huyu aliniambia kwamba kuna vita baridi vinavyoendelea kati ya makampuni ya kutengeneza madawa na waganga wa kienyeji. Mganga huyu alinifunulia kwamba ikiwa makampuni haya yatajua kwamba unafanya vizuri na kwamba wewe ni mtu makini, huwa wanafuatilia akaunti yako kwenye benki, kujua kiasi cha pesa unachozalisha, kisha wanakuita kando na kukupatia bonge la kazi katika kampuni yao. Hapa, unapewa mshahara mkubwa na majukumu ya kuhudhuri makongamano, warsha zisizokuwa na malengo maalum, na kadhalika. Haya yote yanafanywa ili kukukengeusha kutokana na lengo lako la kupata tiba kwa manufaa ya watu wako. Niambie kama hujazingirwa masikini Mwafrika!
UKIMWI kwenye orodha ya magonjwa madogo!
Katika ripoti ambayo niliirejelea hapo juu, inasemekana kwamba ikiwa magonjwa ya aina fulani hayawadhuru kwa wingi hawa wenzetu, basi huwa hawajishughulishi sana nayo.Kama takwimu za ulimwengu zinatwambia ukweli, basi ni kweli kwamba UKIMWI ni ugonjwa ambao una sura nyeusi. Wengi wa wahanga ni watu wa mataifa ya Afrika. Katika mataifa ya weupe, wengi wa wahasiriwa ni watu weusi. Kulingana na hiyo ripoti ambayo bado ninaifuata, huu UKIMWI umeshadhihirika kama ugonjwa ambao si wa weupe. Ni ugonjwa ambao hauwagusi sana wananchi wa mataifa yaliyoendelea. Hapa, unaweza kuwa unajiuliza ni vipi usiwe ugonjwa wao ikiwa weusi miongoni mwao wameathiriwa kwa kiasi kikubwa kuliko weupe? Hapa, nitakutuma kwa mshairi wa Jamaica, Mutabaruka, ambaye anasema “It no good to stay in a white man country too long!” Mwenzake Linton Kwesi Johnstone wa Uingereza atakwambia “England Is a Bitch” Uklweni ni kwamba hata ukae kitambo gani katika nchi hizi tunazozikimbilia, hutawahi kuwa mmoja wao! Kwa hivyo, kuna juhudi ambako sasa mataifa haya yatajiondoa katika kushughulika na utafiti na uzalishaji wa madawa ya kupambana na gonjwa hili. Jambo hili sasa linatuleta kwenye tajiriba niliyoirejelea ya maandamano mjini Nairobi.
Maandamano Mjini Nairobi
Wanaharakati wa kupambana na UKIMWI, pamoja na wahasiriwa walijimwaga jijini na kulizingira bunge ili kuweza kuzipaaza sauti zao za wanyonge kwa wabunge wao ambao wamepanda ngazi na kuingia kwenye jumba la ulaji na kuwasahau kule chini. Wabunge, kwa udhamini wa makampuni makubwa ya kutengeneza madawa walikuwa wameletwa mswada kuhusiana na hati miliki. Kifungu katika mswada huu kilisema mambo kuhusiana na ununuzi wa madawa kutoka ng’ambo. Kifungu hiki kilinuia kuharamisha uagizaji wa madawa mbadala kutoka nchi ambazo zinayazalisha na kuyauza kwa bei nafuu. Wenye madawa haya wameutupilia mbali utu na kufuata faida. Ikiwa mswada huu ungelipitishwa, basi bei ya madawa ya kupunguza makali ya UKIMWI yangelipanda bei kwa asilimia elfu moja. Bei hii ingelikuwa juu sana kiasi kwamba masikini, ambao ndio wengi wa wananchi wa taifa hili, hawangelimudu bei ya madawa haya.
Mbona wenzetu mmetuacha?
Sijui ni kwa nini wabunge wetu hawakuyaona haya. Sijui ni kwa nini wabunge nao wamejiunga na hili genge la kuwala watu wao wenyewe. Ilichukua uingiliaji kati wa wizara ya afya kupitia mkurugenzi wa huduma za afya, kwa serikali kulegeza msimamo wake wa kuwa pamoja na hawa wageni walafi. Ninatumai kwamba mswada huu utapitishwa na marekebisho muafaka kama tulivyofahamishwa na wizara ya masuala ya kikatiba ya kwamba kipengele cha kuhusiana na madawa ya UKIMWI imeondolewa.
Ikiwa Mwafrika ungelijua jinsi ulivyozingirwa, hungelimchukia ndugu yako. Hizi tofauti za kipumbavu zilizoko kati yetu zingeliyeyuka. Mwafrika, jiulize na ufikirie tena!
Amadi(Msailimambo)
Filed under: Maoni ya jumla
Kujitia usipotakikana ni msopeko
Nakumbuka wakati fulani ambapo nilisoma shairi fulani ambalo mtunzi wake nimemsahau ila ningelipenda kuamini kwamba lilitungwa na Ustadh Hassan Mwalimu Mbega; yule gwiji wa lugha na fasihi ya Kiswahili. Katika shairi hili, kulikuwa na mkarara ambao ulisema kwamba mtu kujitia mahali usipotakiwa, huo ni msopeko.
Ningelipenda kuamini kwamba kuendelea kushiriki kwa timu za Afrika katika mashindano ya kombe la dunia ni msopeko.Ninaamini kwamba hii ni mojawapo ya hila ambazo zinatumiwa na mataifa makubwa kuonyesha picha ya uongo kwamba tuko sawa na kwamba kuna haki katika mfumo wote wa jinsi mambo yanavyofanywa. Ni sawa na kumchukua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoka Amerika ya Kusini (Javier Peres De Cueller) au Afrika (Boutros Boutros Ghali na sasa Kofi Anan) na kwa kufanya hivyo kutaka watu kuamini ya kwamba Afrika au huyo mteuliwa ana ushawishi wowote dhidi ya kile ambacho Marekani, Uingereza na washirika wao wanataka kutekeleza.
Uongo Mtupu!
Kombe la dunia ni uongo mtupu.Tusijidanganye kwamba ni kitu amabacho huwa kinashindaniwa kwa usawa na haki. Timu za Afrika zinazoshiriki huwa ni kiwakifishi cha hila na kiinimacho cha kujaribu kutakasa jambo ambalo tayari limekwama katika uchafu.
Kombe hili lilipochezwa kwa mara ya kwanza nchini Uruguay, hakuna timu yoyote kutoka bara hili ambayo ilishiriki katika kinyang’anyiro hiki. Mara ya kwanza kushirikisha Afrika, kulikuwa na jumla ya timu 16 tu, na kulikuwa na nafasi moja tu kwa timu kutoka Afrika. Usiulize ni kwa misingi gani Afrika ikawa na timu moja tu wakati bara hili ni kubwa kushinda mabara mengine mengi ya ulimwengu.
Misri ilikuwa ndiyo timu ya kwanza kuwakilisha Afrika mnamo mwaka wa 1934 kule Italia. Afrika ilikuwa nje ya mashindano haya hadi mwaka wa 1970 ambapo Morocco iliwakilisha Afrika kule
Mexico.
Katika mashindano haya kama historia ya kombe hili inavyoonyesha, timu za Kiafrika zimekuwa zikifanya vizuri sana na kuonyesha dalili za kuweza kulishinda kombe hili.
Kombe la Dunia Kuja Afrika
Yule mchawi wa soka; Edmond Arantes Dos Nasesmento au kwa jina maarufu Pele, aliwahi kutabiri kwamba kabla ya mwisho wa karne iliyopita, kombe hili lingelinyakuliwa na timu kutoka bara la Afrika. Kufikia mwaka wa 1978, bara la Afrika lilikuwa limepata matumaini makubwa sana ya kufanikia katika ndoto hii. Wawakilishi wao ambao walikuwa ni Tunisia walifanya vizuri sana na wakazuiliwa na Wajerumani kwa kuwa walihitaji kushinda mechi kati yao ambayo iliishia droo tasa. Waliporudi nyumbani baada ya mechi hii ambayo iliwatosa nje, kocha wao alisema ‘Ulimwengu umekuwa ukichekelea Afrika lakini sasa hiyo kejeli imeisha’. Kabla ya hapo baada ya Mexico, nahodha wa timu ya Morocco alisema baada ya kurejea kwao ‘Tuliacha alama yetu kule Mexico na tunajivunia jambo hilo’.Pengine ndoto ya Afrika kulingana na utabiri wa Pele ilikuwa ikijitokeza kwa picha kamili na ya kuaminika sana.
Matokeo ya timu za Afrika katika miaka iliyofuata yalionyesha kwamba Afrika ilikuwa imefikia ukomavu wa kisoka ambao ulikuwa ni mgumu kupuuza. Kulikuwa hakuna kejeli tena bali woga; woga wa watawala wa ulimwengu kuona kwamba mashindano yao huenda yakanyakuliwa na hawa wageni ambao wanafanya msopeko. Ndiposa tukaanza kuona mambo yakichukua mwelekeo ambao ni wa kawaida
sana Afrika ikutanapo na ulimwengu wa Wazungu.
Mwaka wa 1982, idadi ya timu za kushiriki katika kombe la dunia iliongezeka na kufikia timu 32, na
kama kawaida, Afrika iliongezewa nafasi moja tu. Mwaka huu, ni timu za Algeria na Cameroun zilizowakilisha Afrika kule Uhispania. Katika michuano yao ya ufunguzi, Algeria walifanya vyema sana na waliwatandika Ujerumani Magharibi mabao mawili kwa moja. Unakumbuka zile enzi ambazo tulikuwa tukiambiwa kwamba kabumbu ilitengenezewa Ujerumani (hasa Ujerumani Magharibi)? Kwa bahati mbaya, walipoteza mechi yao dhidi ya Austria kwa mabao mawili kwa bila. Matokeo haya yaliwafanya kuwa katika hali teketeke kwani iliwabidi kushinda kwa mabao mengi zaidi ili kuweza kuibuka washindi dhidi ya wapinzani wao Ujerumani. Basi licha ya kuwacharaza Wachili mabao matatu kwa mawili katika mchuano wao uliofuata, masikini walijipata wakiwa wamekabiliwa na ukweli kuhusu msopeko. Katika hali ya msopeko, unaweza kukaribishwa na kula makombo ila huruhusiwi wala kukaribishwa kwenye meza kuu; meza ya waheshimiwa. Basi Ajerumani na jirani zao Waaustria wakakutana katika kile ambacho mwandishi wa “New African” (Toleo la Juni 2006) Peter Law alikieleza kuwa mojawapo ya mechi za kuaibisha sana katika historia ya kombe la dunia. Sababu ni kwamba, Wajerumani na Waaustria walikuwa wamesoma hali ya mambo kwenye orodha ya matokeo na wakajua kwamba ikiwa Ujerumani ingelishinda kwa bao moja tu, basi Waafrika wangeliyaaga mashindano kwa tofauti ya mabao.
Ujerumani na Austria Wala Njama
Hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati Wajerumani walipowapachika kaka na jirani zao bao moja tu. Timu zote mbili zilianza kucheza mchezo ambao ulikuwa wa kirafiki kwa viwango vya kutisha.Njama ilikuwa ni kuhakikisha ya kwamba Ujerumani inabakia mbele. Kandili ya Afrika ikajipata kwenye mkondo wa kimbunga cha njama ya Wazungu. Kumbuka yaliyotokea wakati wa michezo ya Olimpiki ya mjini Berlin ambako kiongozi wa Ujerumani Adolf Hitler alikataa kumtunukia medali ya dhahabu yule mkimbiaji maarufu wa Marekani Jessie Owens. Kisa na maana? Alikuwa mtu mweusi!
Mchezaji wa Afrika na Masaibu Yake
Kwa wingi wa masaibu na vitimbi, Afrika imekuwa ikijikaza na kushiriki katika dimba hili.Tunakumbuka kuwa mwaka wa 1970 wakati Morocco waliposhiriki, rais wa nchi ya Zaire (ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Mobutu Sese Seko alivutiwa sana kiasi cha kumwita aliyekuwa kocha wa Morocco, ambaye alikiandaa kikosi cha Congo hadi kikafaulu kuingia katika fainali za kombe hilo zilizochezwa kule Ujerumani. Wakati huo, pamoja na matatizo ya kufanya msopeko, timu hii ilileta kwenye uwanja wa kimataifa tatizo ambalo limekuwa sugu sana kwa timu zetu. Hivi majuzi, mshambulizi matata wa Kenya kijana Dennis Oliech alikashifiwa na kuzomewa na vyombo vya habari kwa kususia kuchezea timu ya taifa Harambee Stars. Mchezaji huyu aliambiwa kwamba yeye si mzalendo na kwamba anafaaa kuliweka taifa mbele na maslahi yake nyuma. Aliyekuwa akiyafoka hayo alikuwa ni waziri wa michezo, ambaye ni mbunge, ambaye kazi yake ya kwanza alipoingia bungeni ilikuwa ni kujinenepeshea donge lake. Huyu ni mwanasiasa ambaye hivi majuzi alisusia kupitisha miswada muhumu kwa wananchi wa nchi hii na ambao walimchagua kuwatumikia eti kwa sababu alitaka nyongeza ya marupurupu yake. Huyu ni mwanasiasa ambaye halipi ushuru. Kuna ushahidi tele dhidi ya madai ya uzalendo wa mwanasiasa wa Kenya.Mbali na matatizo ya shujaa Oliech, timu ya Mobutu ilikumbwa na matatizo ya wachezaji kutolipwa marupurupu yao. Hili lilikuwa ni pigo kubwa kwa wachezaji ambao walikuwa ni kama wanajeshi wa taifa. Kumbuka kuwa Mobutu ni mtu ambaye alikuwa amekalia migodi ya nchi yake; ambayo ni nchi inayoweza kulisha Afrika nzima kwa karne kadha. Mobutu ni mtu ambaye misaada yote kwa taifa lake ilikuwa ikiishia kibindoni mwake, yeye, wanawe na makahaba zake. Basi huyu ni mtu ambaye alishindwa kuikimu timu ya taifa ambayo yeye mwenyewe alisaidia kuiunda. Hapo tulianza historia ya timu za Afrika kutojitayarisha vizuri hadi wachezaji wanaingia uwanjani na njaa na jitimai. Ilikuwa ni kwa vitisho (au kwa kuhurumiwa na Argentina) ndiposa Wazaire wakashindwa kwa mabao matatu kwa nunge na Argentina. Mobutu alikuwa ameahidi kwamba ikiwa wangelishindwa kwa mabao manne kwa nunge, basi hawangelirejea nyumbani. Kumbuka huyu ni jama ambaye alipanga na kusimamia kifo cha yule mzalendo Patrice Lumumba!
Wakati wa dimba hilo, Wacameroun nao walitoka sare katika mechi zao zote, na wakakosa nafasi katika raundi ya pili, baada ya Roger Milla kunyimwa bao.Kombe likawa limebaikia kwao!
Lazima Waafrika Wafurushwe!
Mwaka wa 1990, timu ya Cameroun ilirudi tena kwa kishindo.
Kule Italia, Cameroun walifanikiwa kuingia robo fainali. Hapa, waling’ang’ana na Waiongereza. Kulikuwa na tishio la karibu na kweli kabisa kuona timu ya Afrika ikiingia kwenye nusu fainali na hatimaye fainali; na pengine kulinyanyua kombe lenyewe hadi huku Afrika; nyumbani kwa dhahabu iliyolitengeneza kombe lenyewe. Kwa roho tutumivu, naikumbuka mechi kati ya Cameroun na Uingereza. Mambo yalikuwa yamechacha na Cameroun walikuwa wametoka nyuma na kuwafunga Waingereza mabao mawili kwa moja. Ni katika dakika za mwishomwisho tu ambapo Garry Lineker alijibwaga kwenye eneo la D na badala ya kulambishwa kadi ya njano na Wacameroun kupewa mpira wa madhambi, ilikuwa ajabu wakati refa alipopuliza kipenga akionyesha eneo la penalty. ‘Mtendewa madhambi’ ambaye ni Lineker alinyanyuka haraka na kuvurumiza mkwaju wavuni, huku akirejesha matumaini ya Mwingereza. Ilibidi sasa mechi kuingia katika muda wa ziada chini ya ile sheria ya kifo cha ghafla au bao la dhahabu;
kama wengine walivyoliita. Ni katika kipindi hiki ambapo Lineker alifyatua tena mdude ambao ulitingisha wavu kwa mtutumo wa buheri kwa Wacameroun. Ingawa walishindwa, ni Wacameroun ambao walichukua ule mzunguko wa heshima baada ya mechi. Kikombe kikawa salama, mikononi mwa wenyewe.
Nazikumbuka vizuri fainali za mwaka wa 1998 ambako kulikuwa na timu 32. Afrika ilikuwa na timu tano tu. Miongoni mwa timu hizo ilikuwa ni Cameroun, ambao walikuwa ni mashujaa wa Afrika. Katika mechi
yao dhidi ya Chile, wachezaji wawili wa Cameroun walionyeshwa kadi nyekundu katika hali ya kutatanisha. Pengine zilikuwa ni juhudi za refa, za kuhakikisha ya kwamba Waafrika hawasongi mbele.
Kama kwamba hili halikutosha, Frncois Omam Biyik alifyatua mkwaju na kuutikisa wavu wa Mchili. Ole wake jamani! Masikini ambaye alikuwa anacheza katika mchuano wake wa mwisho kabla ya kustaafu alinyimwa bao hilo. Kisa na sababu, hatujawahi kuambiwa.
Ghana na Brazil
Basi hivi majuzi nilipotazama mchuano kati ya Ghana na Brazil, niliona kama tumefika kilele cha ubaguzi dhidi ya timu za Afrika. Ingawa katika mechi hiyo kulikuwa dhahiri kwamba Waghana wangelishindwa, walishindwa kwa hali mbaya sana kwa sababu ya juhudi za refa. La kusikitisha ni kwamba, hatujawahi kusikia kwamba kikao cha FIFA kimeandaliwa ili kumjadili na kumwadhibu refa fulani ambaye aliilalia timu ya Afrika. Imekuwa sasa ni lakabu katika vyombo vya habari kusema kwamba timu fulani ya Afrika ilicheza dhidi ya wachezaji kumi na mmoja pamoja na refa. Huu ni upuuzi mtupu ikiwa kauli hii itachukuliwa kuwa kama pambo vinywani mwa wanahabari.Ilikuwa ni dhihaka tupu kuona manahodha wa Uingereza na Ufaransa wakisoma taarifa dhidi ya ubaguzi wa rangi, na jinsi soka inavyoweza kutumiwa katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Tulinde dhidi ya Waafrika!
Hebu tutizame hapa. Wakati wa matayarisho ya mechi kati Brazil na Ghana, kulikuwa na maombi maalum kutoka kwa Wabrazil kwamba wangelipenda kupewa ulinzi dhidi ya Waghana ambao waliwaeleza kuwa watu wanaocheza kiholela. Walisema kuwa Waafrika wana mchezo wa kimabavu sana. Inashangaza kwamba wenzetu walioko ughaibuni wanaweza kujitenga nasi kwa kiasi hicho.Kuna huu msisimko wa weusi wasioishi katika bara hili kutaka kuonyesha jinsi wasivyo Waafrika. Ukienda nchini Uingereza, utapata mgawanyiko mkubwa kati ya wakaazi ambao ni wahamiaji wa kutoka Afrika na wale wa kutoka katika mataifa mengine, hasa kule chini visiwani Caribbean. Utawapata Wajamiaca ambao wanadai kwamba Waafrika tuna harufu fulani isiyopendeza, pengine ningelisema kwamba tunavunda. Katika mataifa ya Amerika ya Kusini vilevile, kuna mgawanyiko mkubwa kati ya wale wananchi walio na ngozi ya maji ya kunde au waliochanganya damu na wale ambao bado wanao ule uasilia wa Kiafrika. Katika nchi kama vile Brazil ambalo ndilo taifa moja lililo na idadi kubwa zaidi ya watu weusi kuliko taifa lolote la bara Afrika, utapata kuwa kuna maudhi yanayonasibishwa na kuwa mweusi. Ndiposa dhana ya Kireno ‘moreno’ (ambayo inamaanisha shombe) ni maarufu mno. Kuna hili sokomoko la watu weusi kujitilia ushombe wasiokuwa nao. Ndiposa wananchi wenzangu wakawa wanastaajabu wakati waliposikia maombi ya Wabrazili. Nakumbuka mwenzangu akiniambia kwamba alishangaa mno alipomwona mwanasoka mashuhuri Pele, ambaye ni mweusi kama Mluo. Nilimkumbusha kwamba mtu kama vile Roberto Carlos akija hapa kwetu, watu watafikiri yeye ni Mtaita, Mkikuyu, Mmaasai, Mchagga, Mpare au Mpokomo! Mwangalie mchezaji Ze Roberto! Huyo ni Mluhya kamili. Lakini anapocheza na Mghana, anakuwa na cheo.
Refa Asikiliza Maombi ya Wabrazili
Basi refa aliyasikiliza maombi ya Wabrazil na akawapa ulinzi wa kutosha. Kila mtu alipomgusa tu Ronaldinho, ilikuwa ni makosa na mara moja mhusika kupewa kadi au kuonywa. Kila Ronaldo alipojikwaa kwa sababu ya uzito wake mwenyewe, refa alipuliza kipenga na kumwadhibu Mghana kwa tukio hilo…Mwishowe aliwapa zawadi ya bao la kuotea.Mechi hiyo ilipoanza, nyoyo za Wakenya zilikuwa zimegawanyika. Kama Waafrika, walikuwa pamoja na Waghana. Kama wapenzi wa Brazil, walikuwa wakiwachangmkia vilevile. Basi mechi hiyo ilipomalizika pamoja na vitimbi ilivyozua, wengi wa Wakenya walikuwa wamehamisha uaminifu wao hadi kwingineko. Walianza kuwapigia debe Wafaransa ambao waliwaona kama ndugu zao kwa kuwa ni timu ya weusi. Hali hii haingelitokea kama hakungelikuwa na matamshi fulani dhidi ya timu hii, matamshi ambayo kwa pakubwa yalikuwa ni ya kukebehi watu weusi. Kunaye msemaji mmoja katika taifa la Italia ambaye alisema kwamba timu hiyo ilikuwa imejaa weusi na wakomunisti. Watangazaji wengine nao wakaiita timu hiyo ‘All Blacks’.
Mwana wa Gaidi na Kahaba!
Mlinda ngome wa Italia aliutwanga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Mwafrika katika kombe la dunia. Wakati hisia zikiwa zimepanda, Mtaliani huyu alimtusi mshambulizi wa Ufaransa Zinedine Zidane. Wakati nikitazama mechi hiyo ya fainali, niliudhika sana kumwona Zidane akilitenda lile tendo lililompelekea kuyaaga mashindano hayo dakika chache tu kabla ya kipenga cha mwisho. Nayo hayo maago yake yalikuwa ya kufedhehesha Kwani alipewa kadi nyekundu. Ilikuwa aibu kwake kama nahodha, na kama mchezaji aliyeonyesha mchezo mzuri sana wakati wote wa fainali hizi, na kama mechi yake ya mwisho katika maisha yake kama mwanasoka wa kulipwa. Niliona maudhi makubwa sana. Ila, maudhi haya yalielekea kwingineko nilipoelewa ni kwa nini mungwana huyu akatenda jinsi alivyotenda. Materazzo alikuwa amemlunga kwa matusi. Alimtusi mamake Zidane, ambaye alikuwa mgonjwa wakati huo. Alimtusi dadake Zidane ambaye ninakisia kwamba hawajawahi kukutana naye. Alimtusi Zidane mwenyewe kwa matusi ambayo wameyaundia watu aina ya Zidane. Zidane ni mhamiaji ambaye wazazi wake wote walitoka nchi ya Algeria. Nchi hii inajulikana kwa Waislamu wkereketwa. Kwa sasa hivi, mataifa ya ulimwengu yanapambana na ugaidi, na dini ya Islamu imechukuliwa kimakosa kuwa ni dini ambayo inatangaza na kuendeleza ugaidi. Ni vigumu sana kuelewa wakati ambapo Marekani na washirika wake wanatumia Waislamu katika harakati zao; na wakati Waislamu wanapopigania haki yao. Kwa bahati mbaya, kuna imani iliyoenea kwamba Waislamu ni magaidi, eti watu wenye asili ya Kiarabu ni lazima wawe magaidi. Ninakumbuka mwaka wa 1998 bomu lilipolipua ubalozi wa Marekani hapa Nairobi, watu wengi walikuwa wakiwahepa watu waliovalia kanzu na kofia upara au mabuibui, kwa kuwa waliwadhania kuwa magaidi. Hivi sasa, ndugu zetu kule pwani mwa Kenya wanaumia kwa kushikiwa na kuzuiliwa na polisi ili kutimiza matakwa ya Marekani kwamba kuwe na vita dhidi ya ugaidi. Kosa lao kubwa ni kuwa waitifaki wa dini waliyoichagua, na kuwa na majina waliyoagiza kutoka Uarabuni. Nina imani ya kwamba anapoishi huko Ulaya, licha ya kuwa mwanasoka shupavu, Zinadine Zidane anatembea huku mabegani mwake akiwa na zigo kubwa linalotokana na usuli wake. Ni ajabu kwamba hata FIFA ilipoingilia kesi yake, ni Zidane aliyechunguzwa na kukemewa. Si huyu Mtaliani aliyechokoza nyuki!
Kombe Hili Ni Letu Kweli?
Kutokana na haya yote, nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini mataifa ya Afrika yanaendelea kushiriki katika michuano ya kombe la dunia. Ni jambo la kudumaza na kukengeusha fikira za watoto wetu kuendelea kuwaonyesha kushindwa kwa Mwafrika. Ni aibu kuendelea kuonyesha kwamba Arika ni fukara na haiwezi kujimudu hasa mbele ya mataifa ya limwengu. Wakati wachezaji wa Marekani na Uingereza wakipewa ulinzi wa hali ya juu wakati wa dimba hilo (kuonyesha kwamba nchi ilitumia rasilimali yake kuwakimu), masikini Watogo walikuwa wakilumbana kuhusu marupurupu yao, jambo ambalo lilimfanya kocha wao kung’atuka. Ni picha gani hii ambayo tunataka kuhifadhi kwenye kumbukumbu zetu?
Afrika Tususie Kombe La Dunia
Ni izara kuwaonyesha hasa watoto wetu kwamba mtu anaweza kumnyima Mwafrika haki yake na kumdhulumu na kumdhalilisha kadamnasi tu na iwe ni sawa tu! Mbona tumeona vita vikali vikizuka kati ya utawala wa Palestina na Israeli, na hata kuhusisha nchi jirani ya Lebanon kwa sababu ya wanajeshi wawili tu wa Israeli? Kwa nini sisi Waafrika tunaruhusu wenzetu wapatao mia moja kudhalilishwa kasha tunaendelea kutoa hiyo nafasi ya kutiwa doa hivyo? Maoni yangu ni kwamba, pindi tuendeleapo na kushiriki katika maigizo haya ya kutufedhehesha, hatutawahi kuheshimiwa. Wakati umefika ambapo Afrika inafaa kuyasusia mashindano haya na kuelekeza nguvu zake kwenye mechi za kitaifa na kimataifa ndani ya bara hili. Tutaendelea kuwatoa wachezaji wa kulipwa wa kucheza Ulaya, Asia na Uarabuni kama vile Michael Essien, Patrick Mboma, Dennis Oliech, Didier Drogba na wengineo. Kumbuka kwamba hata kama nchi zetu hazitashiriki, watu wenye asili ya Kiafrika watazidi kushiriki kama vile ilivyokuwa mwaka wa 1966 ambapo mataifa ya Afrika na Asia yalipojiondoa mashindanoni humu lakini bado kulikuwa na Mmorocco (Fontaine) ambaye alikuwa akichezea Ufaransa, pamoja na mwenzake Eusebio mwenye asili ya Kimsumbiji, ambaye alikuwa akichezea Ureno. Ninahofia aibu tutakayotiwa tena mwaka wa 2010. Fikiria adhabu ya kuonewa kwenu! Fikiria utoneshaji wa donda la ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini!
Filed under: Maoni ya jumla
Karibu Madaraka!
Hapo kesho, tarehe mosi Juni, Wakenya tutasherehekea
kama ilivyo kawaida, siku kuu ya Madaraka. Hii ni siku ambayo
Kenya ilijipatia idhini ya kujitawala. Ninapoikumbuka siku hii, siwezi kujizuia kuziwaza zile siku nilipokuwa mtoto mdogo nikikua. Enzi hizo, watu walikuwa na ari ya uzalendo. Kunao wimbo mmoja ambao nitaunukuu hapa kwa mapana na marefu. Huu ulikuwa wimbo wa kumhimiza kila Mkenya kuwa na fahari ya kuwa Mkenya katika
Kenya iliyo huru. Wimbo huu pia uliyakariri mawaidha ya Mzee Kenyatta katika nyingi ya hotuba zake. Wakati huo, Kenyatta aliwahimiza Wakenya kuweka vifua mbele na kuona fahari ya kuwa na uhuru na kuwa wanajitawala wenyewe. Nao waimbaji wa bendi ambayo nafikiri ilikuwa ni bendi ya Vijana wa Huduma kwa Taifa wakayarudia maneno hayo. Wimbo wenyewe ulienda hivi:
Kanyaga nchi yako kwa nguvu na raha
Hili ni hakikisho la rais wetu
Zamani tuliwekwa eti namba four
Sasa abautani tuko namba wani
Pambio:
Kenya, Kenya
Kenya taifa letuKenya, Kenya
Kenya nchi Yetu
Wako wapi wabeberu waone haya
Tuliyoyatimiza kwa miaka chache
Ni wao walisema hatuna akili
Na huku watunyonya afadhali kupe
Hizi ni nyimbo ambazo zilikuwa zikiipamba kila siku kuu ya kitaifa nasi kama watoto tukazikariri na kufikiri kwamba zilikuwa na maana kuu mno. Baadaye nikiwa mkubwa kidogo nikaishi wakati wa enzi ya Mtukufu Rais Daniel Arap Moi. Enzi hii ilikuwa na mahanjam yake pia. Wakati huu nyimbo za dini zilibadilishwa mashairi yake na zikafanywa za kumtukuza mtukufu rais. Mbali na jambo hilo, kulikuwa pia na nyimbo zingine ambazo zilikuwa za kizalendo mno. Kulikuwa na huu wimbo mmoja ambao mpaka sasa bado unanigusa ninapoukumbuka. Kwa bahati mbaya, hatuchezi tena nyimbo hizi kwenye redio kwa sababu zinawakumbusha watu sana kuhusu enzi ya Moi, ilhali serikali iliyopo sasa ingelipenda tuamini kwamba enzi hiyo ilikuwa mbaya sana na hii iliyopo ni serikali nzuri sana ambayo haina uhusiano wowote na falsafa ya Nyayo. Hilo tulirudie wakati mwingine. Kwa sasa na tuulenge wimbo wetu ambao unaenda hivi:
Tushangilie Kenya taifa letu tukufu,
Kenya tunayoipenda
Daima!
Kenya nchi tunayoipenda
Daima!
Anayependa Kenya ni yule mwenye kutenda haki kwa watu wote
Daima!
Mtu mwenye kutenda haki
Daima!
Jamani
Kenya kipenzi chetu hatutaiacha milele daima
Sitaiwacha Kenya nchi yangu Mimi ni mwanakenya daimaNa nikienda ng’ambo nitarudi
Mimi ni mwanakenya daima
Sitadanganywa kamwe na wageni
Mimi ni mwanakenya daima
Wala sitapotoshwa na wabaya
Mimi ni Mwanakenya daima!
Na tumeapa sote wananchi wa Kenya kutumikia Kenya daima na milele
Kenya kipenzi chetu, hatutaiacha milele daima
Mistari mikali ya kizalendo
Maneno mazito kweli ambayo yalizifanya fikira zangu changa kuanza kuuliza maswali kuhusiana na haki na uzalendo. Nikajiuliza, je, mtenda haki ni nani? Nikajiuliza je, uzalendo ni nini? Nikafahamishwa kwamba mzalendo ni mtu ambaye anaipenda nchi yake. Mzalendo ni mtu ambaye ataitetea katiba na fahari ya bendera yake. Nikaisoma historia na ikanionyesha kwamba kuna watu ambao hawapendi nikiwa na raha na uhuru wa usogevu nchini mwangu. Nikasoma jinsi walivyojaribu kuniweka utumwani na mababu zangu walionitangulia wakajitolea kulipigania taifa hili. Ndiposa Kenyatta akaja na huu usemi wa kukanyaga nchi yako kwa nguvu na raha. Nilimwamini Mzee Kenyatta pamoja na yule aliyenifunza kuhusu uzalendo.
Laiti ningalijua kwamba utu uzima ungenitolea picha tofauti kabisa. Nasikitika kwamba taifa hili lina picha tofauti kabisa ya uzalendo. Wazalendo wake ni watu ambao hata kidogo hawafai kupewa hiyo hadhi. Huwezi kuamini kwamba hadi sasa, kunao mashujaa wa Mau Mau ambao wanaishi katika umasikini wa sina sinani. Wale wachache walioiramba miguu ya wakoloni na kuwasaidia wanyonyaji hao katika njama zao za kuwazima wazalendo, ndio sasa waheshimiwa wetu. Ukifikiri ni uongo, chukua tu tathmini ya baraza la sasa la mawaziri kisha ikiwa hutaelewa ninasema nini, basi nipe mji, na usiwe wa mbali sana.
Hivi karibuni, mimi mwenyewe nimekumbwa na visa ambavyo vinanifanya kuziona hizi nyimbo kuwa kama bembelezi wanazoimbiwa watawala wangu. Hazina kina chochote, la sivyo zingeugusa moyo wa mtawala hata mmoja. Kama nilivyoahidi kwamba katika makala zangu mbili tatu zitakazofuata nitajikita zaidi katika visa nilivyovishuhudia hivi karibuni, wacha sasa niikite makala hii katika mkumbo huo.
Siku ya kufa kwa nyani
Siku moja nimejitokea kazini. Ilikuwa jioni mno na nikapitia kwenye duka pale mjini ili ninunue vitu kadha vya nyumbani. Kisha rafiki yangu akanipigia simu. Tulikuwa tukutane mtaani ili tuweze kuyanyoosha mawili matatu kabla ya siku kuisha. Basi nikamaliza ununuzi wangu na nikaelekea kwenye kituo cha magari ya usafiri wa umma ambayo kwa lugha ya huku kwetu tunayaita matatu, au kwa lugha ya vijana Matt. Kufika mtaani, ilikuwa ni mwendo wa saa mbili na nusu jioni. Tulikaa na mwenzangu na kuzungumza hadi mwendo wa saa tano na vichopo, wakati tulipotii zile saa ambazo wakaazi wa Dar Es Salaam wanaziita saa za Makamba. Kutoka nje, tulikuwa jumla ya watu watatu. Tukaiona teksi ambayo ilikuwa imeegeshwa hapo nje. Tukazungumza na dereva na kukubaliana malipo. Mmoja wetu alikuwa ashaingia kwenye teksi tuliposikia sauti ikitokea gizani ” Wee! Msiingie kwenye gari. Simameni hapo!” Nilipotupa macho nikaona kumbe ni polisi. Nikajua kwamba mtumishi kwa wote anakuja kunijulia hali, huku nikikanyaga nchi yangu kwa nguvu na raha. Alipofika karibu, mheshimiwa askari na bunduki lake kubwa na la kutisha alizunguka nyuma yangu na kunichota juujuu kwa mkanda wa suruali. Nikataka kujua ni kwa nini nachukuliwa kipopo namna hiyo. Askari akaniamuru kwenda kujiunga na kundi la watu wengine ambao walikuwa mahali gizani.
Jambazi mbeba mboga
Tulikuwa jumla ya watu wapatao ishirini. Mimi na mfuko wangu wa plastiki uliosheheni mboga za aina mbali mbali, pamoja na watu wengine tukawa tumebatizwa wahalifu. Mimi, pamoja na shehena yangu ya mizigo nilikuwa jambazi ambaye nilikuwa nawahangaisha watu. Mimi, pamoja na kutii serikali yangu, nikawa nimekuwa mhalifu badala ya kuwa mzalendo. Au si katiba ya nchi inayotoa mamlaka kwa polisi? Kwa kutii mamlaka ambayo yametolewa kwa mtu fulani na chombo kinacholiongoza taifa langu, kumbe nilikuwa nimetenda kosa! Tuliburutwa na kuzungushwa usiku huo kweli, kisha askari waliokuwa wakituongoza kama kondoo wakaanza kutuvuta kando mmoja mmoja au wawili wawili. Watu walipelekwa kando na hela kubadilishana mikono. Nikashangaa ilikuwaje kwamba magaidi na majambazi wa hivi karibuni tu wanakuwa wananchi wazuri tena mara tu baada ya kumpakaza askari polisi kitu mkononi? Mimi nilipovutwa kando pamoja na mwenzangu (mwenzetu wa tatu alikuwa tayari ameshaingia ndani ya teksi wakati wa mavamizi haya) tukapelekwa kando na askari kudai kwamba tumpe ’kitu kidogo’. Ingawa nilikuwa na hela nyingi kuliko zile shilingi mia moja ambazo alikuwa akidai, nilikataa kumpa askari chochote. Sababu yangu ilikuwa kwamba sina hatia yoyote. Nina kila namna ya ushahidi kwani nilikuwa nimebeba mboga! Hii si silaha! Askari alijua fika kwamba alinishika kwa kunizuia kuingia teksi. Si hatia kuingia teksi. Hata kama kulikuwa usiku, hakuna amri ya kutotoka nje usiku! Basi usistaajabu kwamba hatimaye, watu tuliokuwa zaidi ya ishirini tulikuwa tumebakia tu wawili: mimi na mwenzangu. Tulipelekwa kwenye kituo cha polisi na taarifa ikaandikishwa haraka sana. Taarifa yenyewe ilikuwa inasema kwamba sisi tulishikwa tukiwa tumelewa chakari, huku tukihujumu amani na utulivu. Vilevile tulikuwa tukienda kama watu tuliokuwa na nia ya kutekeleza uhalifu.
Uvundo wanikaribisha
Usiku huo katika seli, niliwaza na kuwazua. Kweli kabisa askari anayejua vizuri kwamba mimi na mwenzangu, pamoja na wale wote waliomhonga yeye na mwenzake, hawakuwa na hatia yoyote, alikuwa radhi kunitosa ndani. Tulikuwa kumi na wanne katika chumba hicho kidogo. Kwanza, kwanye ushoroba unaoelekea kwenye seli yenyewe, kulikuwa na choo ambacho kilikuwa kimeachwa mlango wazi, nacho kilikuwa kimejaa pomoni. Nilikaribishwa na uvundo ulionipiga kombora. Kwenye seli nilimowekwa, kulikuwa hakuna nafasi ya kulala. Nilikaa karibu na mlango ambapo kulikuwa na ndoo ambamo pia mlikuwa na mchanganyiko wa kinyesi na mkojo wa wakazi wa chumba hiki. Mmoja wa wale waliokuwemo aliinua kichwa chake na kunisabahi ”Sasa rasta?” Mimi nami nikambwagia jibu langu ”Fit”. ”Umebambwa na noma gani maze” . Hapo ujanja wangu ukaniambia kwamba ninafaa kuwa sugu la sivyo hawa wenzangu huenda wakaninyanyasa. Basi nikambwagia ”Maze imekuwa ni noma jo. Maze nimebambwa na hawa maponyi nikiwa juu ya ma-hussling na ma-deal ambayo wasee wamenikinda maze”. Basi mwenzangu akaniliwaza ”Usijali maze. Tuta-conquer chali yangu. Rata never die jo!”.
One Man Guitar aimbia jela
Kwa makaribisho hayo nikakaa chini na nikakumbuka hotuba ya Kenyatta: Kanyaga nchi yako kwa nguvu na raha. Nikakumbuka ule wimbo ambao unaniambia kwamba anayependa Kenya ni yule mwenye kutenda haki kwa watu wote daima, na mtu mwenye kupenda haki daima. Mbona mimi nilikuwa naadhibiwa kwa kuwa niliyazingatia haya? Kule seli, nilikutana na watu ambao maisha ya Kenya huru yamewapiga vikumbo kweli. Kule kuwa kwao ndani kunatokana na hali ngumu ambayo uhuru wao umewatumbukiza ndani. Kulikuwa na kijana mdogo ambaye alikuwa amekaa seli kwa muda wa miezi sita kwa kuwa kaiba viatu. Kunaye jama mmoja ambaye alikuwa ni mchanganyiko wa vitu kadha: alikuwa ni mwanamuziki wa kucheza gitaa huku akiimba, huku Kenya maarufu kama One Man Guitar. Alikuwa pia ni hamali aliyekuwa na mkokoteni wake, kisha alikuwa makanga wa steji ya hapo karibu. Aliokotwa pale steji akipiga debe na akasukumwa ndani.
Uhondo wa seli
Mbali na hayo, kulikuwa na makabila mbali mbali ya miguu na buti zake. Kwa kawaida ya seli za hapa Kenya, mtu huvua kiatu kimoja anapoingia ndani. Ninafikiri hii ni hatua ya kuzuia wizi wa viatu. Basi nilipatana na miguu ambayo ilikuwa imetengana na maji kwa siku nyingi, na buti ambazo zilikuwa zimeganda miguuni utafikiri zimewekewa gundi. Usiniulize ni harufu gani iliyokuwemo mle ndani, ikichanganyikana na ile ya ndoo ambayo ilikuwa inchi chache mbali na mimi. Nilipandwa na ghadhabu lakini kasauti fulani kakaninong’onezea kwamba ilikuwa ni bure kukasirika kwani ningelijichosha bure. Usiku ungelikuwa mrefu na maumivu yangu mengi zaidi. Basi niliamua kuisogeza miguu ya watu kadha na kujinyoosha kwenye sakafu huku nikikiweka kichwa katikati ya miguu hii, na muda si muda, msono wangu ulijiunga na kwaya ya wakoromaji iliyokuwa ikihanikiza nyimbo zake kule seli. Hebu fikiria, hata tuseme nilikuwa nimeshikwa katika hali ya kunifanya kushukiwa, ilikuwa ni haki kuwaweka watu seli na kuwafungia kwa kufuli, huku choo chao kikiwa ni ndoo, ambayo yeyote aliye na haja huichuchumaia, huku wenzake wote mkiwa mashabiki wake? Mbona hawa washukiwa tayari walikuwa wameshaanza kuadhibiwa hata kabla ya mahakama kuwapata na hatia? Usijali kujua haya yalimalizikaje.
Usiombe kukutwa na askari ukiwa umekwama
Kisa kingine kilinipata wakati nikiwa barabarani na gofu la gari. Kama unauelewa mji wa Nairobi, kuna hii steji ya hospitali ya Kenyatta. Basi kufika hapo, gari likagoma. Nikajaribu kuliweka kando ili nilijulie hali lakini halikufika kando sana. Ilikuwa Jumapili usiku wa mwendo wa saa tatu hivi. Wakati huu huwa hakuna magari mengi barabarani. Basi niliweka taa za tahadhari na nikampigia fundi simu. Naye kwa bahati akawa yuko maeneo hayo, na akaahidi kufika hapo bila kuchelewa. Muda si muda, wakaja watumishi kwa wote. Mara moja walinishambulia, wakalisukuma gari hadi kando ya barabara na kupiga simu kwa gari la kuvuta. Muda mfupi baadaye, ile langa langa yao ya kuvuta magari ilikuja na kigari changu kikainuliwa juu, hadi kituo cha polisi cha Kilimani. Nililifuata baada ya fundi kufika na tukapata gari lishaegeshwa na kuandikiwa taarifa. Taarifa yenyewe ilisema kwamba mwenye gari alikuwa kalewa chakari, akawatusi askari na vilevile alikuwa akiendesha gari kiholela huku akiyazuia magari mengine. Nilishangaa jinsi mtu anavyoweza kuwa analiendesha kiholela gari ambalo limekwama. Nikashangaa tangu lini polisi akatusiwa na mwenye kutusi asile kofi, risasi na kuchukuliwa juujuu hadi kituoni mwao. Haja yao ilikuwa nini? Nilipie uvutwaji wa gari. Kesho yake, nilirudi na kulipa shilingi elfu mbili mia saba za Kenya kwa hiyo huduma ya kuvuta. Askari wakapata kivuno.
Askari wa kuvuta magari
Siku nyingine tena nimekwama. Wakati huu, nilikuwa karibu na kituo cha polisi cha Langata. Niliona magari ya kuvuta yakiwa hapo karibu, nje ya kituo cha polisi. Nilienda na kukuta wenyewe hawamo. Basi nikaingia kwenye kituo cha polisi kuwauliza juu ya watu hawa. Watumishi kwa wote walipiga simu na baada ya muda wakaja. Ajabu ni kwamba walipofika, askari alikuwa ni mmoja wa wale waliokuwa kazini kwenye lile gari la kuvuta. Basi nikafikiri ni kwa sababu ya usalama. Kumbe amekuja ili ajipatie sehemu yake ya ndovu huyu aliyekuwa ameanguka. Basi nilipoambiwa malipo waliyotaka wale waheshimiwa, niligomba nikakataa hata huduma zao na kuwafukuzilia mbali pamoja na askari wao. Baadaye walirudi na kuniambia kwamba bei ambayo nilikuwa nimeikazania mimi ilikuwa ndiyo bei halali, lakini kwa kuwa askari alikuwepo, yeye pia alitaka sehemu na ikabidi malipo yaende juu zaidi ili askari wote wa zamu kituoni wapewe kitu. Fikiria uko nchini mwako, unalipishwa kodi kila kona, kisha umepatwa na matatizo, na ni wakati wa usiku. Wale ambao unalipa kodi kuwasitiri ndio wanaotaka kukuumiza zaidi. Je bado nikanyage nchi yangu kwa nguvu na raha?
Umuhimu wa wahalifu nchini
Kama kwamba kapu langu lilikuwa bado halijajaa, mengine yakanipata tena. Nilikuwa nimetoka kunyoosha viungo kwenye eneo la makazi la Chuo Kikuu cha Nairobi. Ukijua ni mazoezi ya namna gani niliyokuwa nimetoka kufanya, huenda utanichekelea sana. Hili ni eneo ambalo ni kama nyumbani kwani nimesomea hapo kwa muda wa takriban miaka saba na huwa sina sababu yoyote ya kuhofu kutembea katika eneo hili. Basi siku hiyo saa mbili za usiku, nikawa naenda kuvuka lile daraja la chini linalovusha barabara ya Uhuru. Nilichokiona, ni watu wakinikaba koo na kuniangusha. Nia yao ilikuwa ni kuninyongea mle ndani darajani ambamo mna giza. Nilijaribu kutapatapa na nikafanikiwa kutoka nje ila bado nilinyongwa tu, nikapokonywa saa, simu, kibeti kilichosheheni pesa, kitambulisho, kadi ya benki na vitu vingine. Baada ya shughuli hii niliachwa pale niko hoi na nikapepesuka kama mlevi nikijitosa kwenye barabara ya Uhuru bila ya kujali magari. Huku nikiwa nimelowa kwa kuangushwa kwenye maji na kwa mvua iliyokuwa ikinyesha rasharasha, nilienda hadi kituo cha usalama cha chuo na kuripoti. Niliambiwa kwamba wanajua vizuri sana kuhusu sehemu hiyo. Nikauliza ni kwa nini usalama haujashughulikiwa hapo, wakaniambia kwamba hiyo ni kazi ya polisi. Nilienda hadi kituo cha polisi cha Central ambacho ni jirani ya chuo. Nikapiga ripoti. Polisi waliniambia kwamba wanajua sana mambo kuhusina na hiyo sehemu, kwamba walikuwa wamepokea habari nyingi sana kuhusiana na mahali hapo. Niliandikisha taarifa na kuondoka. Kesho yake nilikuja kuchukua stakabadhi za kuonyesha kwamba nimepoteza vitu vyangu, hasa kitambulisho. Kwa bahati nikamwona askari fulani ambaye tuna uhusiano wa kinasaba kwa mbali. Aliponiuliza kilichonileta kituoni, nilimwelezea yaliyonipata, na nikalirudia swali langu la ni kwa nini hawakulinda doria pale wakati walijua kwamba kunao vibaka. Askari ambaye ni mtu wa ukoo wangu kwa mbali aliniambia kwamba wakora ni muhimu katika jamii. Aliniambia kwamba bila ya kuwepo wakora, basi watu wangelikuwa tu na uhuru wa kutembea na kunywa pombe jinsi wanavyotaka. Nilipomwuliza kuna shida gani katika kufanya hivyo, sijui alinijibu nini. Alikuwa tayari keshaniudhi. Nikabaki kinywa kikavu pale katika kituo cha polisi cha Central, nikiwa na maumivu ya shingo huku kumeza mate kukiwa shida tupu, uso wangu ukiwa na mipapuriko ya kuangushwa na kupigwa kucha, mtumishi kwa wote akiwa ameniambia yote. Je, niendelee kuikanyaga nchi yangu kwa nguvu na raha?
Nitakachofanya kesho
Kutokana na hizi tajiriba zangu pamoja na zingine nyingi, siku ya kesho nitaitumia vizuri. Najua wengi wenu mtaenda kwenye kumbi mbali mbali ili mkajazwe uongo masikioni. Kwa muda wa majuma kadha sasa, nimekuwa nikiwaona wanajeshi ambao ni vijana wenye nguvu zao wakiwa wanashinda pale katika uwanja wa michezo wa Nyayo, wakipiga paredi mchana kutwa. Mbona twapoteza muda na rasilimali hivi? Naona pia anga zikipasuka kwa milio na miruko ya ndege aina ya Jet ambazo zinapiga mbizi angani ati kwa matayarisho ya siku kuu hiyo. Mbona hii siku haina maana kubwa kwetu mbali na kupiga paredi kwa wanajeshi wetu, huku wanasiasa wetu wakija kutuonyesha wake na waume zao na mavazi maridadi waliyovaa, pamoja na magari yao ya kutisha? Mbona tusiseme kwamba ili kuadhimisha siku hii mwaka huu, tuwe na mwezi mzima wa wanajeshi wetu kutusaidia katika kujenga barabara, daraja na kuhudumu katika hospitali zetu? Mbona tuwachukue watu wenye nguvu na ujuzi na kwa majuma matatu mazima tunawapigisha paredi kule uwanjani, na mifuko yao ya migongoni, virungu, bunduki, vifaru, magari ya deraya na majibwa wao? Ni aibu kwamba hadi kufikia sasa, mimi kama masikini wa nchi hii hata sina nambari. Wimbo ulisema sasa abautani tuko namba wani. Sijui hao sisi walikuwa ni kina nani, nilifikiri kwamba ni Waafrika wote ambao walikuwa wamekanyagiwa. Kumbe ni kundi fulani la wateule wachache.
Maombi yangu
Kwa hivyo Mkenya mwenzangu, utakapoisherehekea siku hii, kumbuka kwamba mimi nitakuwa nimejifungia kwangu nyumbani nikishughulika na mambo tofauti. Pengine nitasoma, nitunge shairi moja hivi au hadithi fupi. Kisa na maana ni kwamba sioni haja ya kusherehekea madaraka wakati ambapo siruhusiwi kukanyaga nchi yangu kwa nguvu na raha. Sioni ni lipi la kusherehekea na kuadhimisha ikiwa nimeonyeshwa mara nyingi kwamba ni haramu kutii sheria. Nyote nawatakieni siku kuu njema ya Madaraka. Maombi yangu ni kwamba siku moja, hata kama itakuwa muda mrefu baada ya uhai wangu, mzalendo wa nchi hii ataikanyaga nchi yake kwa nguvu na raha.
Amadi.
Filed under: Maoni ya jumla
Katika miezi michache iliyopita, kuna kadhia kadha zilizojiri nchini mwangu ambazo zitakuwa mada ya makala zangu kadha zitakazofuata.Kwanza, nakumbuka kabisa ziara ya rais wa Uchina pamoja na mkewe na wapambe kadha. Waswahili husema mgeni njoo mwenyeji apone. Wakenya walingojea kwa hamu kumkaribisha rais wa Uchina ambaye alikuwa amekuja ili kutathmini hali ya uchumi nchini na kuwaza na kuwazua na mwenzake juu ya uwezekano wa kuwekeza zaidi nchini.
Wana bidii
Mimi ninawapenda sana Wachina. Ninawapenda kwa sababu Wachina ni taifa la watu ambao wameonyesha kwamba juhudi zinaweza kufanikisha maendeleo ya watu. Unaposoma kitabu cha mwandishi Edgar Snow kiitwacho Red Star Over China, utaona kwamba wakati mfupi tu kabla Mao Tze Tung alipoyaanzisha mapambano yake nchini Uchina, Uchina ilikuwa ni nchi masikini sana. Kuna maelezo kuhusu jinsi Wachina masikini walivyokuwa wakisaga mawe na kuyapika kama supu ya kunywa. Lakini tazama sasa. Uchina ni mojawapo ya nchi ambazo zimeendelea mno.
Ni wajanja
Ninawapenda Wachina kwa sababu wao ni wakaidi. Wachina si watu wa kupokea maagizo na maelekezo kutoka kwenye nchi zinazojifikiria kuwa viranja wa kimataifa. Uchina imefuata mfumo wake wa kijamaa ambao pia umejumuisha ubepari. Wao waliuchukua mfumo wa kijamaa na badala ya kufuata barabara iliyosakafiwa na vigogo kama vile kina Lenin, wao waliuelewa kivyao na wakaunda mfumo wao ambao ni wa Kichina. Ninawapenda Wachina pia kwa ukaidi wao wa kutotii hati miliki. Waafrika tumekataa kujitengenezea vitu vyetu kwa kutii sheria ya hati miliki ambayo huwa inatunnyang’anya hata vitu vyetu na kuviweka mikononi mwa wageni. Wachina hawayajui hayo! Ni mara ngapi unatembelea duka la vifaa vya umeme na kupata kasha lina jina kama vile Sony, na unapofungua ndani, unapata kwamba kumbe utumbo wa kile kifaa ulichonunua ni wa Uchina. Utakumbana na majina kama vile Mecosonic na mengineyo ambayo ni maujudi kwa Uchina.
Wanatuuzia hata vibatari
Ninawaheshimu Wachina kwa kuwa huku kwetu, hakuna hata nyumba moja ambayo haina bidhaa ya kutoka Uchina. Wachina hawalengi masoko ya matajiri. Wao hulenga soko la mtu wa kawaida. Nao watu wa kawaida ni wengi kuliko matajiri. Ndiposa tajiri hujulikana sana kwani si wengi kama yeye. Mchina alijua kitambo sana mantiki ya kutengeneza na kuzalisha kwa minajili ya soko hili. Ndiposa utapata kandili zinazowaka vibandani mwetu ni za kutoka Uchina, hata vibatari! Utapata nyembe, sindano na vibiriti vyote vya kutoka Uchina. Baiskeli ambazo ni usafiri wa mtu wa kawaida, tumepewa na Uchina. Wachina wakaona pia kwamba matajiri walikuwa wamehodhi vyombo vya starehe ambavyo sasa vilikuwa vimevuka mpaka wa starehe na kuingia katika eneo la kuwa muhimu; vyombo kama runinga na radio. Kwa kuwa vyombo hivi ni muhimu kwa kusambaza habari za uongo na kweli, Wachina walituundia viredio vidogo na viruninga pia. Ndiposa ukifanya uchunguzi humu nchini, utapata kwamba moja kati ya kila nyumba tatu utakazoingia itakuwa na angalau karuninga kanakoonyesha kwa weupe na weusi, aghalabu rangi yake nyekundu, chapa yake Greatwall, nako ka kutoka Uchina. Utapita mitaani na kumwona mwuza karanga akiwa na kiredio chake cha kusikiliza salamu, pengine chapa Jec, kutoka Uchina.
Mwamba wa bidhaa ghushi
Wachina ni mafundi wakubwa wa kughushi hasa majina ya bidhaa. Mchina huendesha mambo yake kama kunguru ambaye atatua kwenye merikebu iendayo mbali. Atayala makombo ya humo melini na bila ya kutumia gharama yoyote, atafika kule anakoenda.Hata ukimwinga, yeye huselelea tu na kuzengea hapo karibu na merikebu, kisha unapomchoka anarudi pale kwake. Basi Mchina kama kunguru msafiri atachukua jina kama vile Sony na kulifanya Suny. Unapokuja kununua bidhaa ile, wewe utarubuniwa na jina kwa kuwa akili zako zimehifadhi lile jina mashuhuri. Ikiwa wewe ni mfuasi wa sheria ambazo zimeundwa na majabali wa ubepari, basi yumkini utaoliona jambo hili kuwa kama ujambazi wa kibiashara. Lakini kabla ya kufanya hivyo, ni lazima tujiulize, hizi sheria ziliwekwa kwa minajili gani? Jiulize ni mara ngapi tumefungwa magoli na hao hao walioziunda hizo sheria? Ni mara ngapi sheria zenyewe zimekiukwa ili kutunyanyasa sisi?
Mabingwa wa kukiuka kaida
Matilaba yangu hayakuwa kuwapigia debe Wachina wala kuuliza maswali mengi ya balagha. Fikira zangu zilisisimuliwa na ziara ya rais wa Uchina ambaye ana jina fupi lakini gumu kutamka. Alipokuja kwetu huyu mheshimiwa, alituaga kwa namna ambayo wageni hawapaswi kuaga wenyeji wao, hata kama wao ni mabingwa wa kukiuka kaida na ada. Katika hafla ya kupiga picha na rais wa Kenya pamoja na mawaziri wake kadha, rais wa China alimwuliza rais wa Kenya maswali nyeti kuhusiana na ufisadi nchini. Hili lilitendeka baada ya yeye rais wa Uchina kutoa ruzuku ya milioni kadha za dola. Kwa njia ya kumfedhehesha mwenyeji wake, rais wa Uchina alitaka kujua kama hizo pesa zingetafunwa au zingetumiwa vizuri. Sijui rais huyu alitaka kujibiwa nini.
Rais wangu avuliwa nguo kadamnasi
Kuongeza msumari wa moto kwenye kidonda, mmoja wa waandishi wa habari waliokuwepo naye akajichovya ndani ya zogo kwa kumwuliza rais swali nyeti. Kusema kweli, tangu achukue hatamu za urais, Kibaki hajawa msemaji mzuri sana. Huyu ni mmoja wa watu ambao wakianza kuzungumza, unachoka. Hata unashikwa na hofu kwa kuwa hujui kama atatamka maneno yanayofaa au atabwabwaja tu. Rais akajipata akitanza ulimi ”Kama unataka kuuliza swali, uliza tu; sisi hatuna lolote la kuficha…..” Malumbano yakaendelea hivyo huku Mchina akizungumza kichina, mkalimani akitubadilishia kwa Kiingereza na waandishi wa habari wakipata uhondo. Rais aliokolewa kutoka kwa mikono ya mwandishi wa habari na waziri wake wa mambo ya nchi za kigeni bwana Raphael Tuju ambaye alirusha kishale mithili ya yale makombora ya babake Joji Kichaka ambayo yalijulikana kwa jina la Patriot, ambayo kazi yake ilikuwa ni ya kuyazima yale makombora ya Saddam.
Tunakubali tu
Mojawapo ya vituo vya kurusha matangazo ya runinga vikapata malighafi ya kuunda mojawapo ya vipindi vyao ambavyo huwakejeli wanasiasa. Nilikitazama kipindi hiki na nikajiuliza ”kweli sisi fahari yetu ilienda wapi?” Nilimwona waziri wangu wa mambo ya nchi za kigeni akimwahidi rais wa Uchina kwamba sisi Wakenya tumekubaliana kabisa na vikwazo vya Uchina kwamba kwa kuwa tulikuwa tumepewa dola kadha, basi tunapinga kwa dhati madai ya uhuru ya nchi ya Hong Kong. Ati hatutawaunga mkono watu wa Hong Kong katika kudai kujitenga. Nashangaa ni kwa nini Uchina inataka kung’ang’ania Hong Kong ikiwa watu wake wenyewe wanataka kujitenga na kuwa na nchi yao. Niliwahi kuutazama mchezo wa kuigiza kutoka nchi ya Hong Kong. Maudhui yake yalikuwa ni madai ya Hong Kong kutaka kujitawala. Kwanza walighadhabika kwamba kwenye kadi zao za mwaliko na visusu vya majina ambavyo tulijitundika wakati wa hafla hiyo, walikuwa wametambulishwa kama Wachina. Basi katika mchezo wao, walionyesha jinsi watu walivyotoka Uchina na kuhamia pembe mbali mbali za ulimwengu lakini bado wanao ule utambulisho wao kama Wachina. Ikiwa wangelijitenga, bado wangelikuwa na historia yao kama watu ambao walitokana na Uchina iliyo pana. Walikuwa na maswali kwa nchi ya Uchina kwamba je, ni kwa nini Uchina isiende kudai hizo nchi ambako Wachina wamehamia? Rais wangu pamoja na waziri wake hawakumwuliza mwenzao wa Uchina ni kwa nini hakutaka Wahong Kong kujitawala. Aliliona kuwa swala nyeti ambalo tulifaa kuliunga tu mkono. Kwetu hapa, swala la ufisadi ni nyeti. Inakuwaje kwamba Mchina awe na urahisi wa kutuuliza kuhusu maswala nyeti kutuhusu bali sisi lazima tuingie mikataba ya kutuzuia?
Je, Wachina wananijali mimi?
Unaweza kufikiri kwamba ninafanya ukaidi usiokuwa na msingi kwa kuwa rais wa Uchina ni binadamu na aliona ufisadi ukilinyonga taifa langu na kwa kuwa ananijali sana, basi akapiga nduru. Mbona tudanganyane? Kumbuka kwamba Uchina ni nchi mojawapo ambazo hazijali kabisa wakati vita vinapoendelea kule Darfur. Haja yao? Mafuta! Kwani wale Wasudani wafao si wanadamu? Uchina ni nchi ambayo inajulikana kwa kutumia mabavu dhidi ya watu wengine. Je, wakumbuka kisa cha Tibet? Hebu fikiria, Tibet ambayo ni nchi iliyo na historia ya zaidi ya miaka 3000, ilikaliwa kimabavu na Uchina kwa zaidi ya miaka arobaini. Uchina haikutosheka bali iliishambulia Tibet mwaka wa 1949. Watu wa Tibet walipoamka na kudai haki yao miaka kumi baadaye, Uchina ilitekeleza mauaji na uharibifu mkubwa sana wa mali ya Tibet. Ilimlazimu Dalai Lama, kiongozi wa Tibet, ambaye pia ni kiongozi wa kidini kuhamia nchini India ambako amekuwa akiishi uhamishoni.
Baada ya mashambulizi na kukaliwa huku, Watibet wameuawa kwa wingi. Kuna tarihi mbali mbali zinazosimulia safari ndefu na hatari ya Watibet ambao wanatoka kwao na kukwea mlima Himalaya ili kuvuka hadi nchini India na Nepal, ili angalau waweze kuonana na kiongozi wao na kuepukana na unyama wa utawala wa Uchina. Safari hii ni ngumu na ni wachache mno wanaofanikiwa. Wengi miongoni mwa hawa wachache hufika ng’ambo ya pili ya milima hii wakiwa bila vidole vya miguu kwa sababu ya kudonolewa na barafu ya milimani.
Muangwi wa Mauaji ya Tiananmen Square
Pengine unapotazama vilele vya majengo ya pagoda ya miji ya Uchina, unasikia kwa mbali muangwi wa mizimu waliofariki wakati wa mauaji ya Tiananmen Square. Ulikuwa ni mwaka wa 1989. Mwezi ulikuwa ni wa Mei.Tarehe ya kuanza kwa mambo ilikuwa ni nne Ulikuwa ni wakati wa enzi za Li Peng, ambapo wanafunzi, wasomi pamoja na wafanyikazi wengine waliamka na kudai kusikilizwa. Maandamano haya ambayo hayakuwaguza viongozi wa Kichina baadaye yalichukua mwelekeo aliotufunza hayati Mohandas K. Gandhi. Wanafunzi waliamua kususia chakula na kukaa kwenye bustani ya Tiananmen hadi wasikilizwe. Majibu ya serikali nzuri sana ya Uchina yalikuwa ni kutangaza sheria ya kijeshi na kuyamwaya majeshi yake mjini Beijing. Kulingana na takwimu za shirika la Msalaba Mwekundu, jumla ya watu 2,600 waliuawa na wengine wapatao 10,000 kujeruhiwa. Wakati huo pia, tukio muhimu katika historia ya maovu ya Uchina lilitokea. Mmoja wa vigogo wa chama tawala ambaye alipinga utekelezwaji wa sheria ya kijeshi- Zhao Ziyang alifurushwa kutoka mamlakani, akaingia mheshimiwa Jiang Zemin, ambaye baadaye alikuja kuwa Waziri Mkuu wa Uchina, ambaye wakati huo alikuwa Meya wa jiji la Shanghai. Yeye Zemin hakuhusika hata kidogo na maandamano na utetezi uliokuwa umepamba moto nchini mwake. Yeye alichaguliwa kuwa rais wa chama.
Falun Gong Yapigwa Gongo
Baadaye katika uongozi wake, Zemin naye akawa na jukumu lake la kutekeleza- kutangaza vita dhidi ya jamii ya Falun Gong, au kwa jina lingine Falun Dafa. Jumuiya ya Falun Gong ambayo inafanya mazoezi ambayo yanajulikana kama Qi gong (kwa matamshi Chi-gong) ilijitokeza wazi wazi mnamo mwaka wa 1992. Wafuasi wa hili kundi walikuwa na bado ni wengi. Kulingana na takwimu za wakati huo, kulikuwa na wafuasi wapatao milioni 70 nchini Uchina halisi pekee, na wengine wapatao milioni 30 kwingineko. Duru zinasema kwamba wafuasi wa kundi hili walikuwa wengi mno zaidi ya wanachama wa chama cha Kikomunisti kinachotawala Uchina. Hapo ndipo zogo lilianzia. Serikali ya Jiang Zemin ilianza kampeni ya kuwafunga, kuwatesa na hata kuwaua wafuasi wa Falun Gong. Kiongozi wao Bw. Li Honzhi au kwa jina maarufu Master Li alilazimika kukimbilia Marekani mnaomo mwaka wa 1994. Mara yangu ya kwanza kusikia habari za Falun Gong ilikuwa ni mwaka wa 1999 wakati wafuasi 700 walipokusanyika Seatle ambako kulikuwa kukifanyika mkutano wa mawaziri kuhusu shirika la biashara ulimwenguni. Nilishangaa kuona wakifanya mambo mbali mbali ambayo yalikuwa pamoja na kutulia tuli kwa njia ambayo si ya fujo hata kidogo. Nilishangaa ni kwa nini watu hawa ambao wanayafanya mambo yao kwa amani waingiliwe. Baadaye nilibahatika kukutana na wafuasi wa kundi hili ambao wanaishi uhamishoni nchini Sweden. Katika mji wa Gothenburg, wafuasi hawa walikuwa wakifanya mambo yao ambayo ni ya kutulia kwa mikao mbali mbali. Katika hali hii ya utulivu, walikuwa na bango lililosema ”Hebu fikiria, serikali yangu yanitesa kwa sababu ya kufanya hivi tu!” Wafuasi hawa wa Falun Gong walinipa maelezo kem kem kuhusu mambo yao na nikawa naelewa zaidi kuliko hapo awali. Serikali ya Uchina inadai kwamba kiongozi wao Bw. Li Hongzhi ni msambazaji wa ushirikina. Sijui kama serikali ina haki ya kunipinga ikiwa ninataka kuwa na imani fulani. Si ajabu kwamba vyombo fulani vya habari vinasema kwamba serikali ya Uchina inawachukua wananchi wake kuwa kama vyombo na mali yake. Hii ndiyo serikali inayonitetea mimi inapozuru hapa Nairobi.
Uchina na hujuma zake dhidi ya mpango wa Agoa
Turudi kwetu Afrika. Kuna huu mpango wa serikali ya Marekani ambao ulianzishwa na rafiki yangu Bill Clinton na baadaye kuendelezwa na Joji Kichaka. Mpango wenyewe ni maarufu kwa akronimu ya AGOA. Chini ya mpango huu, nchi za Kiafrika zinaruhusiwa kuuza bidhaa za nguo katika soko la Marekani bila kutozwa ushuru. Mpango huu umekuwa na matokeo mazuri kiasi kwa nchi husika. Ingawa kumetokea hali ya udanganyifu(na nchi ya Uchina inahusika katika udanganyifu huu), kuna ushahidi wa kuundwa kwa nafasi za kazi kwa wafanyakazi wa Afrika ambao wanatengeneza nguo hizi. Pengine nirudi nyuma na kuukabili udanganyifu wa Uchina. Imegunduliwa kwamba mataifa kadha hayana uwezo wa kuzalisha kiasi cha nguo kinachohitajika sokoni Marekani. Kwa hivyo, Wachina huzichukua nguo zao zilizotengenezewa kwao Uchina, wanazisafirisha hadi mataifa haya, kisha baadaye zinasafirishwa kupelekwa Marekani ili kuuzwa kama bidhaa za kutoka Afrika. Pengine huu ni ujanja mzuri. Hila ni pale ambapo licha ya uwezo wa nchi kuzalisha, Uchina kupitia shoroba za ufisadi inanyenyeresha bidhaa zake na kuzidumaza bidhaa za taifa mhasiriwa. Hayo hayatoshi. Sasa hivi, mataifa ya Afrika yanapong’ang’ania kuongezewa muda kwa mpango huu wa AGOA, Wachina nao wanapiga kampeni ya kuwafungulia soko la Marekani bila vikwazo vya kuwekewa kwota. Katika nadhari yao, wanajua kwamba wanaweza kufurikisha soko hili na kuyafungia nje mataifa ya Afrika. Hawa ndio Wachina wanaotujali kiasi kwamba wanawakebehi viongozi wetu hadharani. Swali ni je, ni lini tutakuwa na fahari tena? Mbona watu waliopakazwa damu tele mikononi mwao wanakuja kututolea mihadhara kuhusu uongozi bora? Mbona watuamulie tutakuwa rafiki ya nani na adui ya nani? Twakumbuka miaka michache iliyopita wakati kiongozi halali wa Tibet Mtakatifu Dalai Lama alipokuwa safarini kupitia nchini humu. Kulingana na mpangilio wake, angelitua Kenya kwa muda wa siku mbili tatu hivi na baadaye kuendelea na safari yake. Kilichotendeka ni kwamba Uchina ilitoa vitisho na Kenya ikaukunja mkia wake na kutoa taarifa ya kumzuilia kiongozi huyo kuingia Kenya. Eti Kenya ilikuwa haitaki kuzorotesha uhusiano mwema ilio nao na Jamhuri ya Watu wa China. Mbona bado twanunua bidhaa za Hong Kong ambayo ni hasimu wa Uchina?
Utayajadili lini mambo ya Uchina?
Swali ambalo ningelipenda kuuliza ni je, Wachina wataturuhusu kuyajadili mambo ya kwao? Hivi sasa, tayari Uchina imeingia mkataba na watoaji wa huduma za kusambaza habari kwa mtandao ya kwamba ikiwa watakubaliwa kuendeleza shughuli zao nchini Uchina, basi mitandao yao pamoja na vifaa vya kusaka kama vile google visiwe na uwezo wa kuonyesha mambo kadha wa kadha. Mojawapo ni mjadala kuhusu Tibet. Ikiwa Wachina hawataki watu wengine au hata Wachina wa kawaida kuujadili uongozi wao, je, wana ruhusa na mamlaka gani ya kuja kutufedhehesha sisi?