mzalendo jisaili


Barua kwa mpenzi
August 1, 2006, 12:40 pm
Filed under: Mashairi

Mpenzi mwandani mahabubu

Naanza kwa kukuomba samahani

Kuandika kwa lugha hii legevu

Nilijaribu lakini sikuweza

Kuyasarifu maneno matamu

Kwa lugha muafaka ya kimapenzi

Mara nyingine ninaahidi

Kutakalamu kwa lugha inayofaa

Bidii nitafanya

Kuyaelewa machungu na matamu yangu

Kwa lugha tukufu isiyo yangu

Badala ya hiki kishairi duni,

Nitakwandikia poem

Nitajitahidi mpenzi

Maneno kuyaelewa

Si kwa jicho la kwangu kijijni

Bali kwa mboni na urazini wa kule kulikotukuka

Nitayatongoza machozi yangu

Kububujika kwa vokali na konsonanti za kimombo

Makali ya moyo wangu kulipuka kwa Kireno,

 Kitaliani au Kituruki

Badala ya huu msamiati nilokujazia hapa,

Nitakuwa na vocabulary  Mpenzi nitakusifu

Kwa majina ya mimea, wanyama na ndege

Wasiopatikana kwetuNitakutungia koja

Nilirembe kwa vito na maua ya nchi za baridi

Au mimea ya jangwaniNisamehe kwa sasa mpenzi

Naikumbuka tu lugha yangu

Ilonitoa tumboni mwa mama 

Ninajua mpenzi

Ni vigumu kwangu kujieleza

Vigumu kwako kuelewa

Nyimbo za nyumbani kwetu kijijini

Ambako tulitembea pamoja tukivikwea vilima

Mikono yetu ikiwa kama sumaku na chuma

Ni vigumu mpenzi

Wewe kuzikumbuka zile harufu

Za mimea iliyotushangilia

Katika sherehe yetu ya mahaba na huba 

Samahani mpenzi

Nimeianza barua hii kwa jina lako la kwanza

Wewe kwako ndilo jinalo la kati

Lililotumika kule nyumbani

Kabla ya kuujua mji,

Ugeni na ustaarabu wake.

Nitakuita kwa jina ajualo nyanyako kutamka

Nitajitahidi mpenzi

Kukujua kwa jina lako la mjini, dini na usasa wake 

Niwie radhi mpenzi

Nitasema nawe kwa sauti

Wanaokuona na kukusikia laazizi

Wajue asili na usuli wako

Kwa muda wasikunasibishe

Na ungwana wa lugha uliyoizoea

Kwa mishangao waashame

Badala ya salaale

Wamake na kubweka ’gosh’! 

Ningelipenda kuahidi kwenda nawe kupata mlo

Lakini natanguliza samahani

Ni haja yangu kukupeleka kula pizza

Lakini nimetafuta jinale katika lugha yangu

Nikakosa kabisa kabisa

Kwa hivyo mpenzi

Samahani zangu zikitangulia

Nakuahidi ugali wa wimbi

Samaki wa kuchemsha

Na mkunde wa kibakuli cha kando 

Mpenzi hitari kula mtori

Jasiri pia kuonja makande,

Rojo la mrenda,

Mukimo na muthogoi. 

Tutakula pia sageti,

Managu na wenzao. 

Tutanyunyiza mafuta

Matamu ya samli,

Kisha tummemene tombo,

Alochomwa kwa makaa. 

Jioni tutakaa

Chini ya uso wa mbalamwezi

Tukichoma ndizi,

Viazi na mihogo 

Anga zitachanua

Kwa thureya ya nyota

Zikiimba wimbo bora

Wa mapenzi motomoto 

Hewani kutafukizwa,

Uturi wa manukato

Ya samadi kavu inayoungua.

Samahani mahabubu,

Ingawa utatamani,

Kifukuza mbu muafaka,

Hii mwandani, haina viletamaradhi. 

Sikio letu kichuna,

Tutamwazima bibi,

Babu akiwa mwenzake

Fikira zetu tuwape pia

Kutusafirisha mbali

Watupatie paukwa pakawa

Za miaka hii na iliyokuwa 

Samahani mpenzi

Yameniishia maneno

Nimeyatesa macho yako,

Masikio na fikira zako

Misri kukurudisha

Japo kwa muda kidogo

Nikuandikiapo mara nyingine,

Nitakupeleka Zayuni

Kwenye miji mikuu ya utandawazi. 

Amadi



Afrika Tumezingirwa!
August 1, 2006, 12:11 pm
Filed under: Maoni ya jumla

Kujiwachilia

Kuna baadhi ya masaibu zangu ambao mimi hujumuika nao katika utundu wa hapa na pale. Wakati huu, inaaminika kwamba watu huwa wanataka kujihusisha katika utundu kwa sababu ya kutulia na kusahau mawazo ya kina.
Kama wasemavyo Wakenya, watu huwa wanataka ‘kujiwachilia’.

Kwa bahati mbaya, huku kujiwachilia huwa hakufanikiwi wakati nikiwa na watu fulani. Tukiwa pamoja, huwa tunataka kuswali kila kitu kwa kina na mapana yake. Ni kutokana na vikao hivi ambapo zimezuka hadithi na mitazamo ambayo tunataraji kuichapisha chini ya anwani ya lugha ya wenyewe “Looking at the World from Down Under”. Hii ni mitazamo ambayo inaelekea kwenye ulimwengu wa kufikirika na kuangalia mambo kama jinsi yangelifanyika. Huwa pia ni wakati wa kuchora taswira ambayo inaweza kuyaelezea mazingira yetu kwa uwazi na ujasiri zaidi.

Faru Hamsini

Ni kutokana na mojawapo ya vikao hivi kulipozuka taswira ambayo ilisema hivi:Waafrika tumezingirwa. Sisi hali yetu ni kama ile hali ya mtu anayejipata peke yake msituni, akiwa amekabiliwa na faru hamsini; wamemweka katikati, wakiwa umbali wa mita hamsini kila mmoja na pembe zake zikiwa tayari kukita. Hizi mita hamsini ni za kuwawezesha kupiga kasi na kumdengua mhasiriwa vilivyo.Kauli hii iliniacha nikiwa ninawaza zaidi. Ni kwa nini picha inayotuelezea sisi iwe kali na ya kutamausha kiasi hiki? Basi katika pitapita na donoadonoa zangu za kujaribu kupata maarifa zaidi, nilikumbana na mambo mawili ambayo yalinifunulia ukweli kwamba huenda kauli hii ikawa ni ya ukweli. Ni dhahiri kwamba kuendelea kuwa hai kama Mwafrika mwenye heshima na fahari yako ni jambo gumu sana. Kumbuka mambo ambayo yaliwahi kuwafika wale Waafrika ambao walikataa. Tazama masaibu ya wapiganiaji uhuru kama vile mashujaa wa Mau Mau. Hawa ni watu waliojitolea na kuyahatarisha maisha yao ili kutukomboa. Walikataa. Sasa hivi, wao ni masikini wa sina sinani. Wale waliokataa kama vile Marehemu Bildad Kaggia vile vile walijipata wakiwa kwenye Saiberia ya kisiasa; kama wasemavyo katika hiyo semi ya Kirusi.Marais wa Afrika ambao walikataa kumfuata mzungu kikondoo na wakasisitiza fahari ya Mwafrika wote walishughulikiwa. Kumbuka Lumbumba alivyouawa kinyama na kuyeyusha kwa chachu! Mkumbuke Thomas Sankara wa Bourkina Faso. Mifano ni mingi.

Mambo mawili yanayovuta nadhari

Hata hivyo, sinuii kuzungumzia marais ambao walidenguliwa na ulimwengu wenye nguvu kwa kosa lao la kuwatetea watu weusi. Niliguswa mno na mambo mawili katika majuma machache yaliyopita. Kwanza, ilikuwa ni ripoti katika mojawapo ya magazeti ya humu nchini Kenya, ambayo ilizungumzia mambo kuhusu maradhi na vile mataifa yaliyoendelea yanavyotufanyia mzaha sisi kama Waafrika. Pili ilikuwa ni mswada wa sheria ambao uliwasilishwa bungeni mwetu hivi karibuni na kupelekea wanaharakati kuandamana mjini nje yao majengo ya bunge.Kwanza, ni swala la magonjwa. Je, ulijua kwamba katika ulimwengu, kunayo magonjwa ambayo ni magonjwa ya maeneo fulani? Je, wajua kwamba mataifa yaliyoendelea na makampuni ya kutengeneza madawa huwa yana haja nayo sana? Ni kweli kwamba mashirika haya pamoja na vyuo na wataalamu wa nchi zilizoendelea wana hela za kuwawezesha kufanya utafiti. Kwa hivyo janga linapotokea katika mataifa ya Kusini kama yanavyoitwa haya mataifa yetu ya hela za madafu; wataalamu hawa hukimbia mbio na kuingia kwenye mataifa haya tayari kutafiti. Wingi wa utafiti hufanikiwa na dawa kupatikana. Jambo la kusikitisha ni kwamba, hata baada ya dawa kupatikana, shida huendelea kuwakumba watu wa mataifa haya kwa kuwa kifo huwa kimewakodolea macho makavu. Kisa na maana? Watafiti hawa kutoka nchi zilizotukuka huwa wanachukua hati miliki ya madawa haya na hivyo kuwazuia wanachi wa mataifa madogo kuzalisha dawa hizi. Kutokana na akili zao za kibepari, watu ni nyenzo ya kibiashara. Ikiwa uwezo wa kibiashara si mkubwa katika kuzalisha kitu fulani, huwa hakuna haja ya kuingilia shughuli kama hii ya uzalishaji.  Ndio, ni takwa la kimsingi kwa ubepari kutegemea faida. Lakini ni utu gani kuzuia uokoaji wa maisha?

Hati miliki

Je, wajua kwamba kuna madawa fulani ambayo yamepewa ulinzi wa hati miliki kiasi kwamba hata ninyi mkiitaka hati miliki hiyo kwa kukodi au kununua, hamuwezi kupewa? Jiulize haja hapa ni nini? Hebu fikiria na ujaribu kupata urazini ulioko katika hali hii hasa ukizingatia kwamba vingi vya vyanzo vya dawa hizi ni vyetu hapa! Ikiwa chembechembe za mkafuri, mkinduri au mwasumini ambao unaota kitaluni mwako zitahifadhiwa kwa hati miliki, je, kuna haki gani? Fikiria kwamba miti ambayo wazee wetu wamekuwa wakihifadhi kwa karne na karne wakifanyia ibada zao chini ya miti hii, sasa iko mikononi mwa watu ambao wanajali tu faida ya pesa ambayo wanataka kupata. Sasa ikiwa chembechembe za miti zitawekewa ulinzi wa hati miliki, basi tunayo miti ya kikwetu kweli?

Magojwa madogo na makubwa

Ndiposa unapata kuna magonjwa kama vile kalaazar na mengineyo, ambayo yanapatikana tu kwenye mataifa haya yetu, na ambayo wenzetu washajua tiba yake, lakini kwa sababu hati miliki wanayo wao, sisi twaendelea kufa tu kwa sababu haina faida kwao ikiwa tutapewa nafasi ya kujizalishia dawa. Kumbuka kwamba uwezo wetu wa kuzalisha dawa ulipigwa fimbo kwa kuambiwa kwamba waganga wetu ni wachawi. Tulisema Haleluyah na kukimbilia kanisani na misikitini na kusubiri dawa kutoka kwa wale waliotufundisha kujidharau. Sasa wakati tukiwa tumefumba macho yetu na kuwasubiri kumaliza sala, tunapata ni hii hii tu miti na magugu yetu ambayo yanatumiwa kutengenezea dawa, na yamemilikiwa! Hata katika taasisi zetu za utafiti, utapata kuwa kunao wageni wengi sana ambao wanakuja kuhudumu ndani. Jiulize ni kwa nini shirika kama vile KEMRI (Taasisi Ya Utafiti wa Kimatibabu ya Kenya) linapendwa sana na wageni. Utapata kwamba taasisi hii inapewa hela nyingi sana na wageni ambao wanazifuata ili kuja kuwa watafiti wakuu. Haja hapa ni kwamba kila matokeo yatakayopatikana yatakuwa na mvutano wa umiliki. Je, unacho kisa cha yule mtafiti wa
Cameroun kwa jina Victor Anomah Ngu? Huyu ni professa ambaye amefanya uchunguzi na kupata majibu fulani kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI. Mara tu walipojua wageni kwamba ana kitu
kama hiki, walikuja na kuomba kwamba washirikiane. Kufumba na kufumbua, ujuzi wake ulikuwa tayari umeshakuwa mali ya Mfaransa.

Vita juu ya umiliki wa madawa

Hapa nyumbani, kuna Authur Obel ambaye alifanya utafiti kwa kushirikiana na Dr. Davy Koech na wakazalisha dawa fulani ambayo waliiita Kemron. Kulitokea ugomvi mkubwa kutokana na dawa hii mpaka ikapigwa kumbo na kuondolewa sokoni. Kisa na maana? Ikiwa dawa hii ingelizalishiwa tu hapa Mbagathi na kusambazwa, soko la makampuni ya kuzalisha madawa la Afrika Mashariki na kati, na hata Afrika Kusini lingelikuwa nimechukuliwa. Vita vilizuka na kusema kwamba hiyo haikuwa tiba. Nani amesema kwamba sumu tunayoletewa na makampuni ya kimataifa ni dawa? Fikira zao zilikuwa kwamba kwa kuwa eneo hili (Afrika Mashariki, Upembe wa Afrika, Afrika ya Kusini) ndilo lililo na asilimia sabini ya wahasiriwa wa UKIMWI ulimwenguni. Hili ni soko kubwa sana kwa haya madawa ya kuja kwa meli na ndege. Vipi Wakenya wapewe ufunguo wa soko hili muhimu? Baadaye nilisoma katika vyombo vya habari kwamba Kemron, dawa iliyokataliwa hata na rais mwenyewe ilikuwa imerudi, kwa jina tofauti lakini kutoka Australia. Niambie kama huyo si faru aliyekulenga ewe Mwafrika?

Makahaba wetu, dawa si yetu

Tunakumbuka ule mvutano uliokuwepo kati ya watafiti wa Uingereza na maprofesa wa Chuo Kikuu cha
Nairobi kuhusiana na chanjo ambayo ilikuwa ikijaribiwa kutokana na utafiti uliofanyiwa makahaba wetu hapa nchini Kenya katika mtaa wa Majengo mjini Nairobi. Maprofesa hawa wa Uijngereza walichukua matokeo ya utafiti na wakaanza kuuendeleza, huku watafiti awali ambao walikuwa ni wasomi Wakenya wakiwa wanachukuliwa kuwa watu wa mkono tu.

Waliomakini wanunuliwa

Niliwahi kuwa na mazungumzo na daktari mmoja wa madawa ya kienyeji ambaye pia anazingatia
sana uchunguzi na matendo ya kisayansi kulingana na wazungu. Mganga huyu aliniambia kwamba kuna vita baridi vinavyoendelea kati ya makampuni ya kutengeneza madawa na waganga wa kienyeji. Mganga huyu alinifunulia kwamba ikiwa makampuni haya yatajua kwamba unafanya vizuri na kwamba wewe ni mtu makini, huwa wanafuatilia akaunti yako kwenye benki, kujua kiasi cha pesa unachozalisha, kisha wanakuita kando na kukupatia bonge la kazi katika kampuni yao. Hapa, unapewa mshahara mkubwa na majukumu ya kuhudhuri makongamano, warsha zisizokuwa na malengo maalum, na kadhalika. Haya yote yanafanywa ili kukukengeusha kutokana na lengo lako la kupata tiba kwa manufaa ya watu wako. Niambie kama hujazingirwa masikini Mwafrika!

UKIMWI kwenye orodha ya magonjwa madogo!

Katika ripoti ambayo niliirejelea hapo juu, inasemekana kwamba ikiwa magonjwa ya aina fulani hayawadhuru kwa wingi hawa wenzetu, basi huwa hawajishughulishi sana nayo.Kama takwimu za ulimwengu zinatwambia ukweli, basi ni kweli kwamba UKIMWI ni ugonjwa ambao una sura nyeusi. Wengi wa wahanga ni watu wa mataifa ya Afrika. Katika mataifa ya weupe, wengi wa wahasiriwa ni watu weusi. Kulingana na hiyo ripoti ambayo bado ninaifuata, huu UKIMWI umeshadhihirika kama ugonjwa ambao si wa weupe. Ni ugonjwa ambao hauwagusi sana wananchi wa mataifa yaliyoendelea. Hapa, unaweza kuwa unajiuliza ni vipi usiwe ugonjwa wao ikiwa weusi miongoni mwao wameathiriwa kwa kiasi kikubwa kuliko weupe? Hapa, nitakutuma kwa mshairi wa Jamaica, Mutabaruka, ambaye anasema “It no good to stay in a white man country too long!” Mwenzake Linton Kwesi Johnstone wa Uingereza atakwambia England Is a Bitch” Uklweni ni kwamba hata ukae kitambo gani katika nchi hizi tunazozikimbilia, hutawahi kuwa mmoja wao! Kwa hivyo, kuna juhudi ambako sasa mataifa haya yatajiondoa katika kushughulika na utafiti na uzalishaji wa madawa ya kupambana na gonjwa hili. Jambo hili sasa linatuleta kwenye tajiriba niliyoirejelea ya maandamano mjini Nairobi.

Maandamano Mjini Nairobi

Wanaharakati wa kupambana na UKIMWI, pamoja na wahasiriwa walijimwaga jijini na kulizingira bunge ili kuweza kuzipaaza sauti zao za wanyonge kwa wabunge wao ambao wamepanda ngazi na kuingia kwenye jumba la ulaji na kuwasahau kule chini. Wabunge, kwa udhamini wa makampuni makubwa ya kutengeneza madawa walikuwa wameletwa mswada kuhusiana na hati miliki. Kifungu katika mswada huu kilisema mambo kuhusiana na ununuzi wa madawa kutoka ng’ambo. Kifungu hiki kilinuia kuharamisha uagizaji wa madawa mbadala kutoka nchi ambazo zinayazalisha na kuyauza kwa bei nafuu. Wenye madawa haya wameutupilia mbali utu na kufuata faida. Ikiwa mswada huu ungelipitishwa, basi bei ya madawa ya kupunguza makali ya UKIMWI yangelipanda bei kwa asilimia elfu moja. Bei hii ingelikuwa juu sana kiasi kwamba masikini, ambao ndio wengi wa wananchi wa taifa hili, hawangelimudu bei ya madawa haya.

Mbona wenzetu mmetuacha?

Sijui ni kwa nini wabunge wetu hawakuyaona haya. Sijui ni kwa nini wabunge nao wamejiunga na hili genge la kuwala watu wao wenyewe. Ilichukua uingiliaji kati wa wizara ya afya kupitia mkurugenzi wa huduma za afya, kwa serikali kulegeza msimamo wake wa kuwa pamoja na hawa wageni walafi. Ninatumai kwamba mswada huu utapitishwa na marekebisho muafaka kama tulivyofahamishwa na wizara ya masuala ya kikatiba ya kwamba kipengele cha kuhusiana na madawa ya UKIMWI imeondolewa.

Ikiwa Mwafrika ungelijua jinsi ulivyozingirwa, hungelimchukia ndugu yako. Hizi tofauti za kipumbavu zilizoko kati yetu zingeliyeyuka. Mwafrika, jiulize na ufikirie tena!

Amadi(Msailimambo)




Follow

Get every new post delivered to your Inbox.