mzalendo jisaili


Barua kwa mpenzi
August 1, 2006, 12:40 pm
Filed under: Mashairi

Mpenzi mwandani mahabubu

Naanza kwa kukuomba samahani

Kuandika kwa lugha hii legevu

Nilijaribu lakini sikuweza

Kuyasarifu maneno matamu

Kwa lugha muafaka ya kimapenzi

Mara nyingine ninaahidi

Kutakalamu kwa lugha inayofaa

Bidii nitafanya

Kuyaelewa machungu na matamu yangu

Kwa lugha tukufu isiyo yangu

Badala ya hiki kishairi duni,

Nitakwandikia poem

Nitajitahidi mpenzi

Maneno kuyaelewa

Si kwa jicho la kwangu kijijni

Bali kwa mboni na urazini wa kule kulikotukuka

Nitayatongoza machozi yangu

Kububujika kwa vokali na konsonanti za kimombo

Makali ya moyo wangu kulipuka kwa Kireno,

 Kitaliani au Kituruki

Badala ya huu msamiati nilokujazia hapa,

Nitakuwa na vocabulary  Mpenzi nitakusifu

Kwa majina ya mimea, wanyama na ndege

Wasiopatikana kwetuNitakutungia koja

Nilirembe kwa vito na maua ya nchi za baridi

Au mimea ya jangwaniNisamehe kwa sasa mpenzi

Naikumbuka tu lugha yangu

Ilonitoa tumboni mwa mama 

Ninajua mpenzi

Ni vigumu kwangu kujieleza

Vigumu kwako kuelewa

Nyimbo za nyumbani kwetu kijijini

Ambako tulitembea pamoja tukivikwea vilima

Mikono yetu ikiwa kama sumaku na chuma

Ni vigumu mpenzi

Wewe kuzikumbuka zile harufu

Za mimea iliyotushangilia

Katika sherehe yetu ya mahaba na huba 

Samahani mpenzi

Nimeianza barua hii kwa jina lako la kwanza

Wewe kwako ndilo jinalo la kati

Lililotumika kule nyumbani

Kabla ya kuujua mji,

Ugeni na ustaarabu wake.

Nitakuita kwa jina ajualo nyanyako kutamka

Nitajitahidi mpenzi

Kukujua kwa jina lako la mjini, dini na usasa wake 

Niwie radhi mpenzi

Nitasema nawe kwa sauti

Wanaokuona na kukusikia laazizi

Wajue asili na usuli wako

Kwa muda wasikunasibishe

Na ungwana wa lugha uliyoizoea

Kwa mishangao waashame

Badala ya salaale

Wamake na kubweka ’gosh’! 

Ningelipenda kuahidi kwenda nawe kupata mlo

Lakini natanguliza samahani

Ni haja yangu kukupeleka kula pizza

Lakini nimetafuta jinale katika lugha yangu

Nikakosa kabisa kabisa

Kwa hivyo mpenzi

Samahani zangu zikitangulia

Nakuahidi ugali wa wimbi

Samaki wa kuchemsha

Na mkunde wa kibakuli cha kando 

Mpenzi hitari kula mtori

Jasiri pia kuonja makande,

Rojo la mrenda,

Mukimo na muthogoi. 

Tutakula pia sageti,

Managu na wenzao. 

Tutanyunyiza mafuta

Matamu ya samli,

Kisha tummemene tombo,

Alochomwa kwa makaa. 

Jioni tutakaa

Chini ya uso wa mbalamwezi

Tukichoma ndizi,

Viazi na mihogo 

Anga zitachanua

Kwa thureya ya nyota

Zikiimba wimbo bora

Wa mapenzi motomoto 

Hewani kutafukizwa,

Uturi wa manukato

Ya samadi kavu inayoungua.

Samahani mahabubu,

Ingawa utatamani,

Kifukuza mbu muafaka,

Hii mwandani, haina viletamaradhi. 

Sikio letu kichuna,

Tutamwazima bibi,

Babu akiwa mwenzake

Fikira zetu tuwape pia

Kutusafirisha mbali

Watupatie paukwa pakawa

Za miaka hii na iliyokuwa 

Samahani mpenzi

Yameniishia maneno

Nimeyatesa macho yako,

Masikio na fikira zako

Misri kukurudisha

Japo kwa muda kidogo

Nikuandikiapo mara nyingine,

Nitakupeleka Zayuni

Kwenye miji mikuu ya utandawazi. 

Amadi


2 Comments so far
Leave a comment

Mzee Amad nimeipitia blog yako nimegundua kwamba swahili uliyoitumia ni fasihi sana na bado si amini ka mluya wa kenya anaweza kuandika swahili ya namna hii ,hii ni kitu ya darasani hata watanzania wenzangu wengi hawawezi andika kama wewe,lugha yako imenyooka sana.
Aziz Toronto

Comment by Aziz

Hata mie sijaamini,ni changamoto kubwa kwetu si sote haswa wadhamini wa lugha hii tukufu.kutoka kenya mluo

Comment by George




Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Connecting to %s



Follow

Get every new post delivered to your Inbox.