mzalendo jisaili


Mhasiriwa, uko peke yako!
November 1, 2006, 6:57 am
Filed under: Maoni ya jumla

Miezi michache iliyopita, ulimwengu uliadhimisha miaka ishirini na mitano tangu kugunduliwa kwa hali ya UKIMWI. Kuna mazoea ya watu kuiita hali hii ugonjwa. Madai yangu ni kwamba hii ni hali bali si ugonjwa. Ni hali ambayo huufanya mwili kupungukiwa na kinga na kuruhusu vimaradhi ambavyo kwa kawaida ni vya kuwinga tu, kuwa na uwezo wa kusababisha kifo. UKIMWI ni hali ambayo tumekuwa nayo kwa hicho kipindi kiasi kwamba kama angelikuwa ni mtoto, basi angelikuwa tayari ameshatupatia mjukuu. La kusikitisha ni kwamba, licha ya kipindi kirefu cha kuishi na hali hii pamoja na masaibu yake, bado tunaonyesha kiwango cha chini mno cha uelewa.

Unyanyapaa

Wakati kongamano likiendelea nchini Canada, kuna madaktari ambao walikutana mjini Nairobi. Miongoni mwa hawa madaktari walikuwa na mawazo ambayo yalinifanya kupigwa na butwaa. Kundi moja lilidai kwamba kutengenezwa na kusambazwa kwa madawa yanayopunguza makali ya virusi vya UKIMWI ni jambo baya sana. Kulingana na kundi hili la madaktari, hali ya kutumia madawa na kurejesha nguvu mwilini ni mbaya sana. Eti wale walioambukizwa viini hivi huwahadaa watu walio ’sawa’ kwamba wao ni watu sawa na wao, hivyo basi kuwaambukiza kiholela! Rai yao ni kwamba heri tungeliwaacha wahasiriwa wafilie mbali kwani wanastahili kufa. Haya ni mawazo yaliyojaa unyanyapaa. Ninashindwa kuelewa ikiwa madaktari wana mawazo kama hayo, basi watu wa kawaida nao watakuwa na mawazo ya namna gani?

Miaka kumi na saba nyuma

Nakumbuka miaka kumi na saba iliyopita wakati nikiwa shuleni. Tulisikia kwa mara ya kwanza kwamba UKIMWI ulikuwa umetufikia kwenye ujirani wetu. Hapo awali, tulikuwa tumefundishwa shuleni kwamba kulikuwa na ugonjwa ambao ulikuwa ni wa wasenge. Ninafikiri ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kusikia neno hilo ’usenge’ na halikuwa na maana sana kwangu. Sikujua ni nini na mwalimu wetu alichukua muda mrefu kujaribu kutuelezea (wakati huo tukiwa shule ya msingi kule mashamabani) hali hiyo na inavyoamili. Tuliambiwa kuwa ilikuwa ni hali ya mazoea ya Wazungu. Basi niliwashangaa sana Wazungu. Sikudhani kama kwetu pia tunayafanya mambo kama hayo. Tulipunga mikono na kusema kuwa tungelijali mambo hayo siku ile tutakayofika Ulaya, kwani sote tulikuwa tunasoma kwa bidii ili tufike Ulaya.

Jirani mhasiriwa

Basi fununu zilianza kutanda kijijini kwetu kuhusu huyu jama ambaye alikuwa jirani yangu na ambaye alikuwa ameishi Nairobi kwa miaka kadha. Alirudishwa nyumbani akiwa amenyauka kweli. Watu walisema kuwa alikuwa na ule ugonjwa ’uliokuja kwa meli’. Tuliogopa kuutaja ugonjwa huo kwa jina lake kamili kwa kuwa tuliogopa kuwa kama nyoka anayetajwa kwa jina usiku, tungeliuchochea kuja karibu nasi kwa haraka. Watu walitazama kando kwa kando. Majirani tukawa hatuingii mji huo kuomba maji tena. Njia iliyokuwa ikipitia mjini humo kama ilivyo kawaida na vijia na vichochoro vya vijijini tukawa tunaiepuka jinsi mkoma alivyoepukwa katika enzi za Yesu.

Mavuno ya kwanza

Siku ya kupumzika kwa mwenzetu ilifika. Alifariki nyumbani na sisi kama majirani tukaomba ruhusa shuleni ili kuhudhuria matanga kwani mmoja wetu alikuwa ni mpwa wake marehemu. Tulipigwa na bumbwazi tulipofika pale na kupata kaburi linachimbwa. Tangu lini kaburi likachimbwa mchana Maragoli? Sisi tulijitosa ndani ya mojawapo ya nyumba za hapo na kuendelea kunywa chai, huku tukipiga soga na kuburudika kwa muziki ambao ulikuwa umeshamiri wakati huo. Wakati tulipotoka nje, kulikuwa na kaburi bichi ambalo tayari lilikuwa limefukiwa. Mji mweupe! Isipokuwa waliofiwa ambao walikuwepo, vichwa chini. Tuliokuwa ndani tuliemewa.   Kwa bahati nzuri, mahudhura watarajiwa kwenye matanga haya walipata udhuru kwani malaika wa kifo alipiga panda yake kwa jirani na wote ambao wangelikuja kulala hapa matangani kama ilivyo kawaida ya destri zetu wakapata pengine pa kwenda, na udhuru tosha wa kutowaliwaza hawa ambao walikuwa wamemzika mgonjwa aliyekufa kutokana na matatizo yaliyosababishwa na UKIMWI. Tuliokuwa ndani wakati wa mazishi tuliambiwa kwamba askari walikuja, pamoja na madaktari wakubwa ambao waliagiza kuzikwa mara moja kwa marehemu. Kwa hivyo mwili ulifungwa kwenye karatasi jeusi la nailoni, kisha madaktari wakavaa glavu, wakajipaka viuaviini, kabla ya kuongoza katika sherehe ya kumzika marehemu. Askari walikuwa tayari kukabiliana na yeyote ambaye angeingiza ndani mambo ya utamaduni. Eti mtu kuzikwa na watu wake; aka! Huyu alikuwa ni mfu hatari.Fikira zilizodumaa

Ninashangaa kuona jinsi tulivyodumaa katika mawazo, fikira na imani zetu tangu miaka hiyo. Tumefundishwa kuogopa UKIMWI. Hatujafundishwa kuuelewa. Tangu wakati huo, tumechora picha mbalimbali za wahasiriwa. Tumewaona kama jama ambao wamekondeana na kuwa na kikohozi kisichopona, huku wakiwa na majipu mwili mzima. Taswira hii imetawala fikira zetu hadi wa leo. Sasa, madaktari wetu wazuri hawataki kukubali kwamba mtu unaweza kuwa na viini hivi hatari na ukaishi maisha ya kawaida kwa tahadhari zako kwa miaka mingi. Madaktari wanataka ufe! Kitambo kidogo, nilisoma katika magazeti yetu humu nchini kuwa kuna jama ambaye baada ya kupelekwa hospitali kwa kulemewa na maradhi nyemelezi, alikaa na baadaye kidogo akaomba kurudishwa nyumbani ili kufa. Kweli, baada ya siku tatu aliaga dunia. Kisa na maana? Wahasiriwa watakwambia kwamba kila wanapoenda hospitali, waganga huwatupia lile jicho la kufifilika. Ni kama kwamba yale wanayoyapitia ni matokeo ya msiba wa kujitakia mwenyewe. Tuliuchukua UKIMWI kuwa tatizo la makahaba na watu ambao hawajijali. Watu wenye maadili mema hawakutarajiwa kupata UKIMWI. Hali hii ilikuwa ni adhabu kwa watenda dhambi. Hata makanisani, nimeshasikia wahubiri wakiwakemea watu wenye UKIMWI kwa kuwataja kama wazinzi ambao Mungu amewapiga kiboko. Juzi, mhubiri fulani alikuja mkahawani tulipokuwa tunapata chamcha na kuhuruju mno kuhusu jinisi tunavyokataa kumpa yeye sadaka ilhali tunawalimbikizia pesa watu wenye UKIMWI, kama kwamba wanafaa kupewa tuzo. Eti watu wengine wanautafuta UKIMWI kwa kuwa kuna pesa sasa. Mhubiri hakutaka kujua kama kwenye ule mkahawa kulikuwa na mtu ambaye alikuwa anaishi na hali hii. Ajabu ni kuwa, hapo mbeleni, kulikuwa na kongamano mjini Nairobi la viongozi wa kidini ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI. Wao pia?Utata wa wenye ugonjwa

Huku sisi tukiuchukua UKIMWI kuwa janga la wataleshi, Wazungu nao walikuwa na yao ya kusema. Waliona janga hili kama janga la Afrika. Hata sasa, mojawapo ya viwakilishi ambavyo vinatumiwa kuelezea Afrika ni magonjwa na hasa UKIMWI. Kwa kulitazama swala hili katika mkabala huu, tunaweza kuona ni kwa kiasi gani tumemtenga maskini mhasiriwa wa UKIMWI. Yeye ni Mwafrika mzinzi!   Siku hizi, kunao makasisi ambao wanakataa kufungisha ndoa kati ya watu ambao wanajulikana kuwa na viini vya UKIMWI. Makanisa kadha huwa yanasisitiza kwamba kabla ya ndoa, wahusika waende kwenye kituo cha kupima na kuja na cheti cha kuonyesha hali yao. Kwanza, matakwa haya ni kinyume cha maadili yanayoongoza upimaji. Kupimwa kunafaa kuwa kwa hiari na kufichua kwa matokeo ni hiari ya mtu. Kimsingi, ni muhimu kwa wawili wanaotaka kuoana kujua hali yao. La kusikitisha ni kwamba, mara nyingi kupimwa huwa kunachangia kuvunjika kwa uchumba wa wawili wanaohusika. Jamii haijaweka misingi ya kuweza kuwalea watu wao hata kama mmoja wao amepatikana kuwa na hali hii. Kwa kuwatenga wenzetu, tumekuwa wa kuendeleza hali ya ubaguzi mithili ya ule wa Afrika Kusini miaka kadha iliyopita. Matendo kama haya yanaeneza hofu, hasa ya mtu kujua hali yake, kwa kuwa matokeo yakionyesha kuwa unao, basi utakuwa midomoni mwa watu, kutengwa na kubaguliwa na waganga ambao wanafaa kuwa wanajua zaidi, kupachikwa majina machafu kama vile taleshi na kadhalika. Hali hii imewafanya wahasiriwa wengi wa UKIMWI kujitia kitanzi ili kuepukana na dunia kali isiyowajali.UKIMWI waenea kama kabobo

Ni katika mkorogo huu wa imani potovu tunapopata UKIMWI ukienea kama zilizala. Watu wanapoogopa kupimwa kwa kuwa watatengwa au kuachwa, huwa wanatoa nafasi ya kueneza zaidi maambukizi haya. Baadhi ya watu wanapojua kuwa wanao, wanakuwa na hofu ya kufichua kwa kuwa wakifanya hivyo, basi watakataliwa. Mhasiriwa anapofanya juhudi za kumkinga mwenzake, kuna baadhi ya visa ambapo mwenzake huona ni kama ni yeye ambaye haaminiwi, na hivyo basi kumweka mtu katika hali ngumu ambapo ni aidha lazima atoboe siri (ambalo ni jambo gumu) au atende matendo hatari. Haya yote ukiyatazama yanakuelekeza kwenye unyanyapaa. Unyanyapaa unaeneza UKIMWI zaidi ya uzinzi na mambo mengine mengi. Wakati tunapofikiri kwamba hali hii ni shida ya wazinzi, tunakosea kwani watu wanaohusika na wazinzi wamepatikana kuchukua tahadhari kubwa zaidi kuliko wanapohusiana na wenzao wa kawaida.

Moto wawaka uzunguni

Wakati ulimwengu wa Wazungu ukikana kwamba hawamo humu, kuna moto unaofoka kwao. Wazungu wameweka vizingiti kwa wahamiaji na wasafiri wengine ambao wana haja ya kuhamia kwao kwa muda. Ikiwa unataka kwenda kusomea nchi hizi zilizopea, lazima upitie mitihani mingi. Mmojawepo ukiwa ni mtihani wa kupimwa UKIMWI ili ijulikane kama unao, ili unyimwe kibali. Hatua hii inaonekana ya kupunguza uwezekano wa kuhamisha maradhi kutoka Afrika hadi kwenye nchi za watu. Hiki ndicho kilele cha mkanganyiko. Ikiwa utafiti tunaoripotiwa unasema kwamba kunao watu ambao wameishi na hivi virusi kwa miaka thelathini sasa, ni kwa nini umnyime mtu nafasi ya kusoma kwa kuamini kuwa atakuwa mfu hivi karibuni tu? Je, ni kusema kuwa kila mtu ambaye ameambukizwa viini hivi ana haja ya kuambukiza mwenzake? Na je, unapomtenga mwenzako, una uhakika gani kuwa wewe uko salama, na utaendelea kuwa hivyo?  Hivi majuzi, serikali ya Zanzibar ilianzisha mjadala kuhusu haja ya kuwataka wageni wote kupimwa kabla ya kuingia kisiwani humo. Kulingana na taarifa hiyo, wale watakaopatikana kuwa na viini vya UKIMWI hawataruhusiwa kuingia kisiwani humo. Tunaambiwa kwamba hii ni hatua ya kupunguza kuenea kwa UKIMWI kisiwani Zanzibar. Ningelipenda kuwaambia kaka zangu wa visiwani kwamba hatua yao ni ya kuendeleza ubaguzi na pia kuendeleza ujinga. Kitu muhimu ni kuwahimiza watu kuwa waangalifu na kutahadhari wakati wa kujihusisha katika mapenzi. Wasije wakawaona wageni wanang’ara wakadhani kila kitu kiko shwari. Kuzuia wageni kuingia nchini ni kulinda ujinga wa watu wenu. Tukumbuke kuwa katika kisiwa cha Zanzibar, kuna shida kubwa sana ya matumizi ya mihadarati. Hili ni tatizo ambalo linafunikiwa pazia na hakuna anayetaka kupambana nalo moja kwa moja. Pindi tunavyoendelea kubugia mihadarati, hata bandari zetu ziwe salama vipi kwa wanabeba viini, bado tumo hatarini. Pindi tunavyozidi kufanya mapenze bila kujali usalama, suluhu haipo karibu. Pindi tunavyoendelea kuwabagua wanaosheheni viini vya UKIMWI na wale ambao wana UKIMWI mpevu, bado hatuna usalama.Kipindi cha Oprah Winfrey

Jambo lingine ambalo limeziteka fikira zangu ni kuhusiana na kipindi cha Oprah Winfrey kilichofanykia hivi majuzi (angalau kimetangazwa kwenye runinga za Marekani). Kwenye kipindi hicho ambacho ninaomba kwamba kipeperushwe Kenya hivi karibuni, Oprah anawahoji watu kadha ambao wanaishi na virusi. Mmoja wao ni Magic Johnson, yule mwanavikapu mashuhuri ambaye mimi nilimjua mapema miaka ya tisini kwa kuwa alitangaza hadharani kuwa alikuwa na virusi vya UKIMWI. Matokeo hayo yalisababisha kuondolewa kwake kwenye timu ya taifa…. Muhimu ni kauli ambayo aliitoa wakati huo. Johnson alisema kwamba, unapofikiria kuhusu UKIMWI, huwa hufikirii kuwa unaweza kukupata wewe pia. UKIMWI huwa ni ndwele ya wale watu wengine tu! Je, wakereketwa wa unyanyapaa twasikia?

Tovuti na blogu za walio na virusi

Katika chakurachakura zangu, nimepata tovuti inayoitwa aidsmeds.com, ambayo inasimamiwa na kuchangiwa na watu ambao wanaishi na virusi vinavyosababisha UKIMWI. Tovuti hii huchapisha jarida pepe ambalo husambazwa kwa wale wanaotaka. Wawili kati yao walikuwa miongoni mwa wageni mashuhuri katika kipindi hiki cha Oprah. Mmoja wao ni mhariri mkuu wa jarida pepe hili na katika blogu yake, alisema:  ”Watu wengi mno wanafikiri kwamba jambo hili haliwezi kuwatendekea. Aghalabu, ninapowaambia watu hali yangu, ninafikiri kuwa watu hutumia dakika kadha za kwanza kudhihirisha ni vipi nilivyo tofauti na wao-kama kwamba kwa kutambua tofauti zilizoko kati yetu ndivyo wanavyozidi kupunguza uwezekano wa wao kuwa na viini vya UKIMWI.  Nikifikiri, wao huchukua muda mfupi zaidi baadaye kuchambua tafsili za maisha yao ya ngono, na kushangaa ikiwa wamejihatarisha mbele ya virusi hivi”.   Nukuu hii ninaipenda kwa sababu inatuelezea sisi kama tunavyofikiria. Tunajiona kuwa watu mahususi na kuwa hiyo taabu ya UKIMWI ni ya watu wengine. Huyu dada anayezungumza ni Mmarekani mweupe. Katika dondoo lingine, dada yetu anasema jinsi alivyosisitiza kuwa anataka kiti cha ndege kando ya dirisha, wakati wa kusafiri kuelekea mahali pa kurekodia kipindi hiki. Anasema: ”Nilisema kuwa nilikuwa nina hofu ya kufa kutokana na ajali ya ndege (licha ya kuwa ni wazo la kipumbavu ukipima hatari inayohusika). Lakini nilikuwa na imani kwamba ningeliyaokoa maisha ya watu kadha ikiwa ningelitokea kwenye runinga. Na hata kama mtu mmoja tu angeliamini yale niliyokuwa ninasema kwenye kipindi hicho, angalau maisha ya mtu mmoja yangeliokolewa, na hiyo ingelifidia hofu ya kuonekana kwenye runinga.”Mhasiriwa kuwakinga wenzake

Hebu angalia jinsi mhasiriwa anavyofanya bidii ya kuwakinga watu. Hapa nyumbani, kunao watu kadha ambao wanaongoza katika vita dhidi ya UKIMWI na ambao wenyewe wanao. Je, wamjua Joe Muriuki? Huyu ni mtu wa kwanza mimi kusikia akitangaza hadharani kuwa alikuwa na UKIMWI. Hii ni kama miaka kumi na saba iliyopita. Bado yupo na anaongoza kampeni za kuhamasisha umma kuhusu hali hii. Haenezi! Yeye na mkewe ni kielelezo chema kwetu hasa kwa kupambana na unyanyapaa. Baada ya kugundua kuwa anao, mkewe ambaye yeye hana, alikata shauri kufunga pingu za maisha na mumewe! Bado wangali pamoja. Mkewe Magic Johnson pia hajamtoroka. Asunta Wagura naye ni kielelezo chema cha mtu aliye na UKIMWI, huku maisha anayaendesha kama kawaida. Ana mpenzi wake na mojawapo ya mambo anayofaidi maishani ni ngono. Rawland Lenya naye ni mfano wa mtu ambaye kimo cha mwili wake kinapinga tafsili zote ulizopewa na walimu wako kuhusu mhasiriwa wa UKIMWI. Je, watu wanaowazuia walio na virusi kuendelea na shughuli zao na kutafuta maendeleo maishani wanatoa imani zao wapi?


1 Comment so far
Leave a comment

Nimepita hapa!

Comment by ndesanjo




Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Connecting to %s



Follow

Get every new post delivered to your Inbox.