Filed under: Maoni ya jumla
Hivi majuzi, nilishangaa mno kuona vioja vikitendeka hapa Nairobi. Mimi ni mpinzani mkubwa wa serikali hii iliyopo na ile iliyokuwepo kabla ya hii. Sababu yangu ni kwamba sioni tofauti yoyote kati ya serikali hii na ile iliyopita kama utahesabu mambo kama vile kuwajibika, kufuata na kuzingatia sheria, kuwa na dhati katika vita dhidi ya umasikini, maradhi, ukabila, rushwa na kutenda kazi kwa uaminifu na inavyotakikana.
Wakati wa utawala wa KANU, tulishuhudia watu wakivunja sheria na kuachwa kujisikia vizuri na utamu na uhuru pamoja na wapendwa wao. Kisa na maana? Walikuwa upande ufaao wa chama tawala.
Wakati Kibaki alipochukua kiapo cha kuitawala nchi hii, nakumbuka akipaaza sauti yake kwenye kipaza sauti akitangaza mwisho wa mambo fulani. Mojawapo ilikuwa ni uongozi wa mtu mmoja, ambapo mambo fulani makubwa yanayohusu sera hayafanywi tu kiholela barabarani. Kwa maneno yake mwenyewe, Kibaki aliharamisha ‘maazimio ya barabarani’. Haukuwa muda mrefu tulipomwona katika kibonzo kwenye gazeti moja la humu nchini, akiwa kama mwanafunzi ambaye alienda shuleni, na baada ya kupewa matokeo yake ambayo alifaa kuyalinganisha na majukumu yake, alirarua hiyo ripoti na kuendelea kujikongoja kwa mkwaju wake wa kucheza golfu, huku akipiga mbinja ni kama kwamba hakuna lililotendeka.
Wanupinzani wamekuwa wakilalamika (na wana haki ya kufanya hivyo) kuwa serikali hii ina kiburi mno. Na hilo ni jambo la kweli. Watazame tu mawaziri wetu. Utafikiri ni viumbe walioumbiwa kwenye chemba maalum kwenye mastakimu ya mfinyanzi mkuu aliyewafanya hao. Utadhani kwamba utawala wao ulitoka kwa Mungu, bali si kwa hawa watu kina yahe ambao wamebaki kuashama kwa njaa na magonjwa, huku kila aina ya tahadhari ikichukuliwa ili kuhahikikisha starehe na ulimbwende wa watawala wetu. Rais anajulikana wazi kwamba ana kimada, ambaye watu walio karibu naye wameamua kumwita mwanaharakati wa chama cha NARC (sasa ni NARC-Kenya) ambaye tunamlipia mpaka ulinzi wa polisi wa umma! Rais aliharamisha wabunge na viongozi wa serikali kuongoza mikutano ya harambee. Huku wahudumu wengine wa serikali na bunge wakiwa wamefungwa mikono, rais, kupitia nyumba ndogo, anaendelea kumwaga pesa.
Juzi tu, rais alisema kwamba anashangazwa na kuudhiwa na wanasiasa wa upinzani ambao tayari wameshaanza kupiga kampeni. Jambo ambalo hakutuambia ni kwamba yeye kampeni zake zilianza mwaka wa 2003 mara tu ya kuchukua hatamu za uongozi na kusahau ahadi zake kwa Wakenya kama rais atakayetuunganisha kama Wakenya, na kutuongoza kwenye barabara ya fahari inayoelekea mustakabali wa ufanisi. Badala yake amekuwa ndiye fisi mkuu na mlinzi nambari moja wa nunda mla watu.
Huku mawaziri wakilewa kiburi, ninashangaa kuwaona vigogo wa upinzani nao wakionyesha sifa za kinyonga kama za serikali.
Reuben Ndolo, mkosoaji mkuu wa serikali alikuwa kwenye habari juzi akikwepa kukamatwa na polisi kutokana na matumizi yake ya pesa za hazina ya usitawishaji maeneobunge. Ni kwa nini viongozi wa upinzani waende kuzingira nyumba ya Ndolo ili kuwazuia polisi kumkamata? Huu ni upuuzi mtupu. Ikiwa upinzani una haja ya kuwa chaguo bora kuliko serikla iliyopo sasa, ni lazima waanze kuonyesha dalili sasa. Kumkubalia tu kila mwizi kwa sababu yeye huongoza nyimbo za kuipinga serikali katika mikutano ya upinzani. Itakuwa bora ikiwa upinzani utamwepuka na kumkana mtu yeyote ambaye ataonekana kuwa na dosari hasa kutokana na matumizi mabaya ya pesa za wapiga kura.
Ni aibu kuona kuwa wale wanaotarajia kuunda serikali bora zaidi ya ile tuliyo nayo, nao wamekuwa ni wa kutetea wezi wa upande wao, huku wakipiga kelele kubwa kwa kutaka mchunguzi wa mambo ya ufisadi kuwachukulia hatua kali wale waliotajwa kwenye visa vya ufisadi kutoka upande wa serikali. Ni ya aina gani hii sheria? Ni maadili ya namna gani haya? Ilhali tunaambiwa kwamba uchaguzi mkuu ujao utakuwa kati ya ‘farasi wawili’, yaani ODM-Kenya na NARC-Kenya! Nakuhurumia ewe Mkenya!
Leave a Comment so far
Leave a comment