Filed under: Maoni ya jumla
Kabila na ukabila
Kila ninapojieleza kama mwananchi au mshirika katika jumuiya ya kimataifa, mimi huanza kwa kujitambulisha kama mmoja wa watu wanounda jumuia fulani ambayo inatambuliwa kwa lugha na utamaduni fulani. Jambo hili linatokana na ukweli kwamba, dhana ya utamaduni wa Mwafrika ni nzito na pana
sana. Katika Afrika, kuna jumuiya nyingi ambazo zina mienendo, mitindo ya maisha na imani tofauti toafauti. Tofauti hizi wakati mwingine zimechangia maafa au uadui na uhasama mwingi miongoni mwa jamii hizi ambazo zinajulikana
kama makabila.
Kimsingi, kabila ni kundi ambalo halifai kuwa na viambata ambavyo vimesheheni uzito wa dharau na ubaguzi. Kabila linafaa kuwa ni mizizi ya mtu fulani. Kabila ni
kama hifadhi ya urejelezi, ambayo inampa mtu dira kuhusu jinsi ya kuindesha mitafaruku na purukushani ambazo ndizo shughuli za kujikimu kwake maishani. Kabila linafaa kutoa misingi ya tafsiri na fasiri ya mambo fulani fulani katika jamii,
kama si mambo yote ya jamii inayohusika. Kwa mfano, kabila langu lina hifadhi ya maelezo (ambayo ni ya kimapokeo na sasa watu kadha wanajaribu kuyanakidi katika vitabu na makala mbali mbali) kuhusu miiko, matambiko, unyago, mazishi, ndoa na kadhalika. Haya ni mambo ambayo ni muhimu kwani yanatoa mwangaza na njia ya kufuata ikiwa mwanajamii anataka kushiriki katika matukio au shughuli hizi za maisha. Kabila basi linakuwa ni kama hema ambamo watu fulani hujisitiri wakati wa haja.
Kabila kama msingi wa Ubaguzi
Kwa bahati mbaya, kabila, hasa katika nchi ninamotoka limechukuliwa kuwa ni mkusanyiko wa wakereketwa ambao ubongo wao wote umo midomoni mwao na kwenye ndimi zao ambazo hulewalewa na kuyumba kama makuti wakati wa upepo mkali. Ni jambo la kushangaza kwamba bado tunaziamini fasiri kutuhusu sisi ambazo tuliachiwa na mkoloni baada ya yeye kulikunja tambara lake (bendera) ambalo liliueleza ukandamizaji. Wakati wa kilele cha ukoloni katika nchi ya Kenya, wakoloni walikalia nchi na kuzitwaa sehemu zote zilizokuwa na rutuba, hasa katika maeneo ya kati mwa nchi, katika eneo la bonde la ufa na katika maeneo ya milimani ambayo waliyabatiza ”Milima myeupe”. Hapa, dhana ya weupe ikiwa ni ya kubwia rangi ya ngozi yao, na hivyo basi kutia chapa ya utimbakwira kwenye maeneo ambayo hapo kabla yakimilikiwa na Mkenya mweusi. Kwa kuwa walihitaji kuistawisha hii ngawira ambayo walikuwa wameitwaa kimabavu, basi wakaanzisha mfumo wa kulipa ushuru- ikiwa nitaruhusiwa kunong’ona hapa kwamba rais wangu wa sasa hivi anasisitiza sana suala la kulipa ushuru. Usiulize huu ushuru unamfaidi nani! Hivyo basi wazalendo weusi walilazimika kuchukua kazi kwenye mashamba ambayo walikuwa wamepokonywa kimabavu na kufanywa vijakazi, ili waweze kulipia ushuru. Wengine wao walikuwa ni wafanyikazi wa nyumbani kwa wazungu. Mzungu alikuja na mizungu yake ambayo ilikuwa imejaa hadaaa ya kwamba kulikuwa na utukufu katika kufanya kazi za nyumbani kuliko kufanya kazi za shambani, kwani nyumbani kulikuwa karibu na kiti cha utukufu- mtu angeliweza kuvigusa vitu anavyovitumia mzungu!
Kijakazi wa shambani na kijakazi wa nyumbani
Kumbuka ile hotuba maarufu ya mpiganiaji wa haki za watu weusi katika nchi ya Marekani kwa jina Malik Al Shabaaz au kwa jina maarufu Malcom X. Akijilinganisha na wale watumwa ambao walikuwa wakijiona kuwa na fahari kwa kufanya kazi jikoni mwa mtu mweupe huku wakijinyenyekeza mbele yake, Malik alikuwa na fahari ya kutangaza kwamba yeye alikuwa ni kijakazi wa shambani (Field Nigger). Huu ni muundo wa uwili ambao ulifanywa na mkoloni kokote alikokuwa ili kuwatenganisha wazalendo kwa kuwafanya wengine wao kuwa upande wake, na waliobaki kuwa upande wa pili uliokuwa mbaya. Nchini Kenya, mambo haya yalidhihirika pale ambapo mapambano ya uhuru yalishika mkiki na kukuwa na kundi au kabila ambalo lilionekana kuwa na mtandao sugu wa kumbwaga chini mzungu. Jamii ya Kikuyu ndio waliokuwa wapishi na mabawabu wa kwanza wa mkoloni. Njama zao za kula kiapo na kutetea haki za mweusi ziliponusiwa na mzungu, mzungu aliamua kuwatosa nje ya nyumba yake. Badala yake aliwachukua wenzetu wa kutoka mkoa wa Magharibi (Waluhya) na kuwasogeza karibu naye na kuwaambia kwamba wao walikuwa ni watu wazuri mno kuliko wenzao ambao walikuwa wazushi.
Kenya Twendapi?
Tendo hili lilikuwa kiwakifishi muhimu katika uhusiano kati ya makabila ya Kenya. Uhusiano huu uliathiri jinsi ngawira iliyoitwa ’matunda ya uhuru’ ilivyogawiwa Wakenya. Jambo hili liliendelea kukita mizizi na hadi kufikia sasa, kuna hisia kali mno za kikabila katika nchi yetu. Kila utawala ambao umechukua uongozi wa nchi umekuwa katika harakati za kujistawisha katika nafasi za utawala huku makabila mengine yakifudikizwa. Kama alivyodokeza yule mzee Karl Marx, nguvu za kiutawala, nguvu za kiuchumi na ushawishi wa kijamii ni mambo ambayo huandamana kama mapacha waliounganishwa kiunoni. Nguvu hizi huathiriana na kulishana kwa njia zote za chanya na hasi. Ndiposa alipokuwa akitawala Kenyatta, kabila la Waluo lilitengwa ati kwa sababu Jaramogi Oginga Odinga alikuwa hasimu yake Kenyatta. Kimsingi ni kwamba Oginga alihitari kuuliza ”Kenya twendapi?” Uhuru tulioupigania sio ule tuliokuwa tunauona. Basi Jaramogi na wafuasi wake walitengwa na eneo zima la Nyanza likatengwa. Tendo hili la Kenyatta kumtenga Odinga pamoja na jamii yake lilikuwa ni somo alilopata kutoka kwenye vitabu vya wakoloni naye akalifuata sawasawa. Katika jamii za Kenya, kukawa na jitihada za jamii kuwa na ’mtu wao’ ambaye angalau angelikuwa katika vitabu vizuri na utawala ili angalau matunda ya uhuru yawadondokee watu wake. Hayo matunda yalikuwa ni kama majitu tunayosimuliwa katika hadithi za paukwa pakawa.
Nyayo za Kenyatta
Wakati Mzee Kenyatta akiwa katika hatua zake za mwisho za kuwatumbukiza Wakenya kwenye dindi la ukabila, Baba Moi alikuwa akifanya kile ambacho Waibo wanakiita mwanang’ombe kuitazama midomo ya mama ng’ombe wakati mama ng’ombe anapokula nyasi. Naye alikuja na genge lake na wakatawala na kupora.
Tulipokuwa tunapiga kelele na kutaka mambo tofauti, kumbe kulikuwa na genge lingine ambalo lilikuwa likijiandaa kuchukua hatamu za ulaji na uporaji. Sasa, ukabila umekomaa kiasi kwamba hata nikaoza sasa hivi, Wamaragoli wenzangu watasimama kidete nyuma yangu na kunipigia kidedea kama kwamba mimi ni malaika kutoka mbinguni.
Kashfa ya wizi wa pesa za umma
Miaka miwili iliyopita, mbunge wa upinzani katika bunge la Kenya Mheshimiwa Maoka Maore, alipiga filimbi kuhusu sakata ya Anglo Leasing. Hii ni kashfa inayohusu njama ya watumishi wa serikali wakiwemo makatibu wakuu, mawaziri, makamu wa rais pamoja na rais mwenyewe kuwaibia Wakenya kwa kupitia kandarasi kadha za serikali. Kandarasi moja ilikuwa ni ya kulijengea jeshi la wanamaji la Kenya meli fulani ya kivita. Kandarasi nyingine ilikuwa ni ya kutengeneza pasi ambazo ni ngumu kuhujumiwa na kughushiwa na matapeli. Basi baada ya Mheshimiwa Maore kupiga ukwenzi bungeni, baadaye makatibu wakuu walifurushwa, huku wakilalama kwamba wao walikuwa wakiyatimiza tu matakwa ya wakubwa wao. Baada ya mwaka mmoja, katibu wa maadili Bw John Githongo alijiuzulu na kukimbilia nchini Uingereza ambako anakaa hadi sasa.
Katika ripoti ambayo Githongo alikuwa amemkabidhi rais Kibaki, kuna malalamiko kwamba kulikuwa na nia hafifu sana kutoka kwa ofisi kuu ya utawala ya kuwachukulia hatua wale waliohusika katika maovu haya. Vile vile, Githongo alidokeza kwamba kashfa hizi zilichochewa na haja ya moja kwa moja kutoka ikulu kwamba pesa zikusanywe tayari kwa uchaguzi wa mwaka wa 2007. Mantiki hapa ni kwamba, ukiwafilisi watu na kuwafanya kuishi maisha ya vibapara, inakuwa rahisi mno kuwatawala kwani unaweza kuwanunua kwa bei ya kitumbua. Rais na utawala wake tayari walikuwa wamekengeuka kutoka kwenye barabara ya kuwatendea wanachi waliyotaka na hivyo kuwafanya kuwachagua tena kwa misingi ya ubora wao. Haja yao ni kutaka kuwanunua wanachi kwa pesa zao wenyewe!
Majina mazito serikalini
Basi majina kadha yalitajwa katika kashfa hizi, ambazo balozi wa Uingereza nchini wakati huo- Sir Edward Clay – aliziorodhesha kama ishirini, na mabilioni ya pesa yaliyolengwa yakiwa ni ya kutikisa bara lote la Afrika. Majina ya wahusika yakatajwa. Ilikuwa ni jambo la kushangaza sana kuona jinsi watu walivyojitokeza kuwatetea watu wa makabila yao! Kulikuwa na majina ya kina Chris Murungaru ambaye alipigwa marufuku ya kusafiri kwenda au hata kuzivuka anga za Marekani, Uigereza, kukiwa na uvumi kwamba mataifa ya jumuiya ya ulaya yalikuwa tayari kumpa marufuku kama hiyo. Kulikuwa pia naye Kiraitu Murungi, mtu wa kuumeni wa rais Kibaki ambaye alikuwa waziri aliyehakikisha kwamba ndoto za Wakenya za kuwa na katiba mpya zimefudikizwa, kwa kutumia ushawishi wake kama waziri wa masuala ya kikatiba. Kulikuwa pia naye waziri wa fedha Daudi Mwiraria. Kigogo wa vigogo alikuwa ni makamu wa rais ambaye kwa bahati mbaya, anatoka katika jamii moja na mimi katika ukoo mpana wa Waluhya.
Watu pamoja na mwizi wao
Nilistaajabu kuwaona Wakenya ambao ndio wanaoshuhudia kila siku watoto wao wakifa kwa magonjwa yanayotibika, eti kwa sababu wakubwa wameiba pesa za dawa. Nilistaajabu kuwaona wakiwa ndio watetezi wakubwa wa wezi wa makabila yao. Nilishutuka kuona watu wakisahau kwamba wao ndio wanaolala njaa kila siku. Nilishangaa kuwaona hawa wahasiriwa wa ghasia za uchaguzi wakiwa wanawatetea watu ambao ni magaidi wanaofaa kufungwa maisha. Niliaibika mno hasa nilipomwona makamu wa rais akizuru nyumbani na kuwauliza Waluhya kwa jicho kavu ’Lero luno khandi muri nange?’ Eti vipi safari hii watu wangu, si bado mko pamoja nami? Nilishangaa zaidi kusikia vigelegele vya kumshangilia mshukiwa wa wizi akirejea nyumbani. Nilifunga runinga yangu na kuelekea kwenye sehemu ya starehe ambako niliukuta mjadala wa kashfa hii ukiendelea. Ninaweza kusema kwamba ulikuwa ni mjadala wa kikabila kwani mtu mmoja kutoka jamii ya Waluhya ambaye alionekana kwamba hajafarukwa sana na mambo ya kimsingi kuhusu mantiki alisikika akibweka ”Makamu wa rais si mwizi!” Nikahitari kumwuliza ni kwa nini yeye alikuwa na maoni kama hayo wakati ambapo yeye makamu wa rais aliidhinisha malipo kwa kampuni ambayo haijulikani na anuani waliyotoa ya kule kwao Uingereza ni gofu fulani ambalo hata halikaliki. Mwenzangu alinijibu ”Waluhya si wezi”, na kwa sisitizo atakalokupa Mkenya yeyote anayetaka kukutolea dhati yake, akachombeza kwa lugha tukufu ”Luhyas are not thieves!” Niliusikia muangwi wa sauti ya mkoloni katika miaka ya ishirini akiwafukuza Wakikuyu kutoka jikoni. Niliamua kufanya jambo tofauti kwa kuwa hapa sasa mantiki yalikuwa yamekalishwa miguu juu kichwa chini. Mimi si shabiki wa kushuhudia nyuchi kwa hivyo nilijiepusha na fedheha hiyo na nikaendelea na burudani ya namna nyingine. Ila moyoni niliwaza mno, mawazo yakanitesa. Hivi, huku kwetu hatuna tena aibu? Ni wapi tulipoipotezea hii aibu? Inakuwaje mzee wa umri wa babu yangu kunipatia fursa ya kumkosea heshima? Ni jambo la kusikitisha sana ikiwa mzee atajiweka kwenye nafasi ambapo inakuwa vigumu kwetu vijana kumheshimu. Ni vipi atakavyoniwaidhi mimi? Je, atawaambia nini wajukuu zake kuhusu maadili?
Haki ya kuiba
Katika ripoti fulani katika mojawapo ya magazeti ya humu nchini, Mamake Kiraitu Murungi, mmoja wa washukiwa wa wizi alisema kuwa mwanawe ameonewa. Katika mikutano ya hadhara ambayo Kiraitu na mwenzie Daudi Mwiraria na Murungaru waliyoandaa, kulikuwa na umati wa watu ambao waliwaunga mkono na kusema kuwa walikuwa wakipigwa vita na makabila ambayo yaliwaonea wivu. Hata viongozi wa makanisa wa maeneo yao wakawaunga mkono. Huna haja tena na torati. Huna haja tena na amri kumi, hasa sehemu zinazohusu kusema ukweli na kutoiba. Viongozi wa makanisa wametutolea tafsiri huria ya amri hizi. Mtu akiwa ni wa kabila lako, hawezi kuwa mwongo au mwizi. Kama ni mwanao, vivyo hivyo kwani yuko karibu sana na kitovu cha kabila lako. Niliona mafunzo haya yakiwa kinyume na yale ambayo mamangu mwenyewe alinionyesha. Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kunipiga pindi tu niliposhukiwa kwa kosa lolote; sembuse la wizi! Nakumbuka mamangu akinicharaza mara nyingi sana kwa sababu ya kushukiwa tu, kisha baadaye ananiomba msamaha baada ya ukweli kudhihiri. Sijui maadili haya yalipotelea wapi na yalibatilishwa lini!
Lilikuwa ni jambo la kukata maini wakati ambapo mzee Moody Awori, makamu wa rais alipoitisha mkutano wa wanahabari na badala ya kujiuzulu, alitapika cheche na kudai kuwa katika kashfa hii, alikuwa hana mshtaki. Aliongezea msumari moto aliposema kwamba yeye pia ana haki zake za kibinadamu. Alishangaa kwa sauti eti tangu lini akawa amezipoteza haki hizo. Kwa mara ya kwanza nilijulishwa kwamba haki ya kuiba na kuifilisi nchi pia ni haki ya kibinadamu. Lakini bado nilikataa kumtetea mwizi wa kabila langu!
Amadi.
Filed under: Maoni ya jumla
Kwa jina la amani, ninawasalimu nyote mnaojumuika katika ulimwengu wa blogu. Mimi ninajulikana kama Mari-Djata Amadi kwaa Atsiaya. Usuli wangu ni nchi ya Kenya. Niliingiwa na hamu ya kublogu pamoja na kuhimizwa kufanya hivyo baada ya kuvinjari blogu ya Kaka Ndesanjo Macha na hasa baada ya kuandikiana barua mbili tatu hivi. Kwa nyote ambao tayari mnablogu, naomba mnikaribishe. Kwa wale ambao wanaitembelea hii blogu yangu, ningelipenda kujulisha ya kwamba hili ni tone la kwanza tu la jasho la moyo wangu. Ninalichukua tendo hili kuwa kama lile la mtunzi wa ule utenzi maarufu wa Al-Inkishafi ambaye anazungumza na moyo wake huku akitufanya sote kusikia haya mazungumzo nafsia.
Mimi nitakuwa tayari kuchangia chochote au kuutoa mkorogano wa mawazo katika uwanja wowote ule kulingana na jinsi akili zangu zinavyonielekeza kufanya. Nawaombeni kwamba katika kufanya hivyo tuwe pamoja. Kwa wale mnaotaka kuujua uraibu wangu ni upi, ningelipenda kusema kwamba wa kwanza ni kupiga soga, hasa lile lenye utomvu ndani yake. Ninafurahia pia upishi na matumizi ya mazao ya tendo hilo. Ninapenda pia; kama inavyotarajiwa kwa mpenda soga yeyote; kujumuika na jamaa na marafiki. Ninapenda sana kusoma! Ninapenda vile vile kuuliza maswali, muziki na minenguo inayoandamana nao, kufanya mazoezi ya viungo, na kukata maji.
Karibuni kwenye blogu yangu, nami nitazivamia zenu.
Shukurani.
Amadi.
Filed under: Maoni ya jumla
Welcome to WordPress.com. This is your first post. Edit or delete it and start blogging!