mzalendo jisaili


Siku kuu ya madaraka i hapa tena
May 31, 2006, 1:37 pm
Filed under: Maoni ya jumla

Karibu Madaraka!

Hapo kesho, tarehe mosi Juni, Wakenya tutasherehekea
kama ilivyo kawaida, siku kuu ya Madaraka. Hii ni siku ambayo
Kenya ilijipatia idhini ya kujitawala. Ninapoikumbuka siku hii, siwezi kujizuia kuziwaza zile siku nilipokuwa mtoto mdogo nikikua. Enzi hizo, watu walikuwa na ari ya uzalendo. Kunao wimbo mmoja ambao nitaunukuu hapa kwa mapana na marefu. Huu ulikuwa wimbo wa kumhimiza kila Mkenya kuwa na fahari ya kuwa Mkenya katika
Kenya iliyo huru. Wimbo huu pia uliyakariri mawaidha ya Mzee Kenyatta katika nyingi ya hotuba zake. Wakati huo, Kenyatta aliwahimiza Wakenya kuweka vifua mbele na kuona fahari ya kuwa na uhuru na kuwa wanajitawala wenyewe. Nao waimbaji wa bendi ambayo nafikiri ilikuwa ni bendi ya Vijana wa Huduma kwa Taifa wakayarudia maneno hayo. Wimbo wenyewe ulienda hivi:

Kanyaga nchi yako kwa nguvu na raha

Hili ni hakikisho la rais wetu

Zamani tuliwekwa eti namba four

Sasa abautani tuko namba wani 

Pambio:

Kenya, Kenya

Kenya taifa letuKenya, Kenya

Kenya nchi Yetu 

Wako wapi wabeberu waone haya

Tuliyoyatimiza kwa miaka chache

Ni wao walisema hatuna akili

Na huku watunyonya afadhali kupe   

Hizi ni nyimbo ambazo zilikuwa zikiipamba kila siku kuu ya kitaifa nasi kama watoto tukazikariri na kufikiri kwamba zilikuwa na maana kuu mno. Baadaye nikiwa mkubwa kidogo nikaishi wakati wa enzi ya Mtukufu Rais Daniel Arap Moi. Enzi hii ilikuwa na mahanjam yake pia. Wakati huu nyimbo za dini zilibadilishwa mashairi yake na zikafanywa za kumtukuza mtukufu rais. Mbali na jambo hilo, kulikuwa pia na nyimbo zingine ambazo zilikuwa za kizalendo mno. Kulikuwa na huu wimbo mmoja ambao mpaka sasa bado unanigusa ninapoukumbuka. Kwa bahati mbaya, hatuchezi tena nyimbo hizi kwenye redio kwa sababu zinawakumbusha watu sana kuhusu enzi ya Moi, ilhali serikali iliyopo sasa ingelipenda tuamini kwamba enzi hiyo ilikuwa mbaya sana na hii iliyopo ni serikali nzuri sana ambayo haina uhusiano wowote na falsafa ya Nyayo. Hilo tulirudie wakati mwingine. Kwa sasa na tuulenge wimbo wetu ambao unaenda hivi: 

Tushangilie Kenya taifa letu tukufu,

Kenya tunayoipenda

Daima!

Kenya nchi tunayoipenda

Daima!

Anayependa Kenya ni yule mwenye kutenda haki kwa watu wote

Daima!

Mtu mwenye kutenda haki

Daima! 

Jamani

Kenya kipenzi chetu hatutaiacha milele daima

Sitaiwacha Kenya nchi yangu Mimi ni mwanakenya daimaNa nikienda ng’ambo nitarudi

Mimi ni mwanakenya daima

Sitadanganywa kamwe na wageni

Mimi ni mwanakenya daima

Wala sitapotoshwa na wabaya

Mimi ni Mwanakenya daima! 

Na tumeapa sote wananchi wa Kenya kutumikia Kenya daima na milele

Kenya kipenzi chetu, hatutaiacha milele daima 

Mistari mikali ya kizalendo

Maneno mazito kweli ambayo yalizifanya fikira zangu changa kuanza kuuliza maswali kuhusiana na haki na uzalendo. Nikajiuliza, je, mtenda haki ni nani? Nikajiuliza je, uzalendo ni nini? Nikafahamishwa kwamba mzalendo ni mtu ambaye anaipenda nchi yake. Mzalendo ni mtu ambaye ataitetea katiba na  fahari ya bendera yake. Nikaisoma historia na ikanionyesha kwamba kuna watu ambao hawapendi nikiwa na raha na uhuru wa usogevu nchini mwangu. Nikasoma jinsi walivyojaribu kuniweka utumwani na mababu zangu walionitangulia wakajitolea kulipigania taifa hili. Ndiposa Kenyatta akaja na huu usemi wa kukanyaga nchi yako kwa nguvu na raha. Nilimwamini Mzee Kenyatta pamoja na yule aliyenifunza kuhusu uzalendo. 

Laiti ningalijua kwamba utu uzima ungenitolea picha tofauti kabisa. Nasikitika kwamba taifa hili lina picha tofauti kabisa ya uzalendo. Wazalendo wake ni watu ambao hata kidogo hawafai kupewa hiyo hadhi. Huwezi kuamini kwamba hadi sasa, kunao mashujaa wa Mau Mau ambao wanaishi katika umasikini wa sina sinani. Wale wachache walioiramba miguu ya wakoloni na kuwasaidia wanyonyaji hao katika njama zao za kuwazima wazalendo, ndio sasa waheshimiwa wetu. Ukifikiri ni uongo, chukua tu tathmini ya baraza la sasa la mawaziri kisha ikiwa hutaelewa ninasema nini, basi nipe mji, na usiwe wa mbali sana. 

Hivi karibuni, mimi mwenyewe nimekumbwa na visa ambavyo vinanifanya kuziona hizi nyimbo kuwa kama bembelezi wanazoimbiwa watawala wangu. Hazina kina chochote, la sivyo zingeugusa moyo wa mtawala hata mmoja. Kama nilivyoahidi kwamba katika makala zangu mbili tatu zitakazofuata nitajikita zaidi katika visa nilivyovishuhudia hivi karibuni, wacha sasa niikite makala hii katika mkumbo huo.

Siku ya kufa kwa nyani

Siku moja nimejitokea kazini. Ilikuwa jioni mno na nikapitia kwenye duka pale mjini ili ninunue vitu kadha vya nyumbani. Kisha rafiki yangu akanipigia simu. Tulikuwa tukutane mtaani ili tuweze kuyanyoosha mawili matatu kabla ya siku kuisha. Basi nikamaliza ununuzi wangu na nikaelekea kwenye kituo cha magari ya usafiri wa umma ambayo kwa lugha ya huku kwetu tunayaita matatu, au kwa lugha ya vijana Matt. Kufika mtaani, ilikuwa ni mwendo wa saa mbili na nusu jioni. Tulikaa na mwenzangu na kuzungumza hadi mwendo wa saa tano na vichopo, wakati tulipotii zile saa ambazo wakaazi wa Dar Es Salaam wanaziita saa za Makamba. Kutoka nje, tulikuwa jumla ya watu watatu. Tukaiona teksi ambayo ilikuwa imeegeshwa hapo nje. Tukazungumza na dereva na kukubaliana malipo. Mmoja wetu alikuwa ashaingia kwenye teksi tuliposikia sauti ikitokea gizani ” Wee! Msiingie kwenye gari. Simameni hapo!” Nilipotupa macho nikaona kumbe ni polisi. Nikajua kwamba mtumishi kwa wote anakuja kunijulia hali, huku nikikanyaga nchi yangu kwa nguvu na raha. Alipofika karibu, mheshimiwa askari na bunduki lake kubwa na la kutisha alizunguka nyuma yangu na kunichota juujuu kwa mkanda wa suruali. Nikataka kujua ni kwa nini nachukuliwa kipopo namna hiyo. Askari akaniamuru kwenda kujiunga na kundi la watu wengine ambao walikuwa mahali gizani.

Jambazi mbeba mboga

Tulikuwa jumla ya watu wapatao ishirini. Mimi na mfuko wangu wa plastiki uliosheheni mboga za aina mbali mbali, pamoja na watu wengine tukawa tumebatizwa wahalifu. Mimi, pamoja na shehena yangu ya mizigo nilikuwa jambazi ambaye nilikuwa nawahangaisha watu. Mimi, pamoja na kutii serikali yangu, nikawa nimekuwa mhalifu badala ya kuwa mzalendo. Au si katiba ya nchi inayotoa mamlaka kwa polisi? Kwa kutii mamlaka ambayo yametolewa kwa mtu fulani na chombo kinacholiongoza taifa langu, kumbe nilikuwa nimetenda kosa! Tuliburutwa na kuzungushwa usiku huo kweli, kisha askari waliokuwa wakituongoza kama kondoo wakaanza kutuvuta kando mmoja mmoja au wawili wawili. Watu walipelekwa kando na hela kubadilishana mikono. Nikashangaa ilikuwaje kwamba magaidi na majambazi wa hivi karibuni tu wanakuwa wananchi wazuri tena mara tu baada ya kumpakaza askari polisi kitu mkononi? Mimi nilipovutwa kando pamoja na mwenzangu (mwenzetu wa tatu alikuwa tayari ameshaingia ndani ya teksi wakati wa mavamizi haya) tukapelekwa kando na askari kudai kwamba tumpe ’kitu kidogo’. Ingawa nilikuwa na hela nyingi kuliko zile shilingi mia moja ambazo alikuwa akidai, nilikataa kumpa askari chochote. Sababu yangu ilikuwa kwamba sina hatia yoyote. Nina kila namna ya ushahidi kwani nilikuwa nimebeba mboga! Hii si silaha! Askari alijua fika kwamba alinishika kwa kunizuia kuingia teksi. Si hatia kuingia teksi. Hata kama kulikuwa usiku, hakuna amri ya kutotoka nje usiku! Basi usistaajabu kwamba hatimaye, watu tuliokuwa zaidi ya ishirini tulikuwa tumebakia tu wawili: mimi na mwenzangu. Tulipelekwa kwenye kituo cha polisi na taarifa ikaandikishwa haraka sana. Taarifa yenyewe ilikuwa inasema kwamba sisi tulishikwa tukiwa tumelewa chakari, huku tukihujumu amani na utulivu. Vilevile tulikuwa tukienda kama watu tuliokuwa na nia ya kutekeleza uhalifu.

Uvundo wanikaribisha

Usiku huo katika seli, niliwaza na kuwazua. Kweli kabisa askari anayejua vizuri kwamba mimi na mwenzangu, pamoja na wale wote waliomhonga yeye na mwenzake, hawakuwa na hatia yoyote, alikuwa radhi kunitosa ndani. Tulikuwa kumi na wanne katika chumba hicho kidogo. Kwanza, kwanye ushoroba unaoelekea kwenye seli yenyewe, kulikuwa na choo ambacho kilikuwa kimeachwa mlango wazi, nacho kilikuwa kimejaa pomoni. Nilikaribishwa na uvundo ulionipiga kombora. Kwenye seli nilimowekwa, kulikuwa hakuna nafasi ya kulala. Nilikaa karibu na mlango ambapo kulikuwa na ndoo ambamo pia mlikuwa na mchanganyiko wa kinyesi na mkojo wa wakazi wa chumba hiki. Mmoja wa wale waliokuwemo aliinua kichwa chake na kunisabahi ”Sasa rasta?” Mimi nami nikambwagia jibu langu ”Fit”. ”Umebambwa na noma gani maze” . Hapo ujanja wangu ukaniambia kwamba ninafaa kuwa sugu la sivyo hawa wenzangu huenda wakaninyanyasa. Basi nikambwagia ”Maze imekuwa ni noma jo. Maze nimebambwa na hawa maponyi nikiwa juu ya ma-hussling na ma-deal ambayo wasee wamenikinda maze”. Basi mwenzangu akaniliwaza ”Usijali maze. Tuta-conquer chali yangu. Rata never die jo!”.

 One Man Guitar aimbia jela

Kwa makaribisho hayo nikakaa chini na nikakumbuka hotuba ya Kenyatta: Kanyaga nchi yako kwa nguvu na raha. Nikakumbuka ule wimbo ambao unaniambia kwamba anayependa Kenya ni yule mwenye kutenda haki kwa watu wote daima, na mtu mwenye kupenda haki daima. Mbona mimi nilikuwa naadhibiwa kwa kuwa niliyazingatia haya? Kule seli, nilikutana na watu ambao maisha ya Kenya huru yamewapiga vikumbo kweli. Kule kuwa kwao ndani kunatokana na hali ngumu ambayo uhuru wao umewatumbukiza ndani. Kulikuwa na kijana mdogo ambaye alikuwa amekaa seli kwa muda wa miezi sita kwa kuwa kaiba viatu. Kunaye jama mmoja ambaye alikuwa ni mchanganyiko wa vitu kadha: alikuwa ni mwanamuziki wa kucheza gitaa huku akiimba, huku Kenya maarufu kama One Man Guitar. Alikuwa pia ni hamali aliyekuwa na mkokoteni wake, kisha alikuwa makanga wa steji ya hapo karibu. Aliokotwa pale steji akipiga debe na akasukumwa ndani.

Uhondo wa seli

Mbali na hayo, kulikuwa na makabila mbali mbali ya miguu na buti zake. Kwa kawaida ya seli za hapa Kenya, mtu huvua kiatu kimoja anapoingia ndani. Ninafikiri hii ni hatua ya kuzuia wizi wa viatu. Basi nilipatana na miguu ambayo ilikuwa imetengana na maji kwa siku nyingi, na buti ambazo zilikuwa zimeganda miguuni utafikiri zimewekewa gundi. Usiniulize ni harufu gani iliyokuwemo mle ndani, ikichanganyikana na ile ya ndoo ambayo ilikuwa inchi chache mbali na mimi. Nilipandwa na ghadhabu lakini kasauti fulani kakaninong’onezea kwamba ilikuwa ni bure kukasirika kwani ningelijichosha bure. Usiku ungelikuwa mrefu na maumivu yangu mengi zaidi. Basi niliamua kuisogeza miguu ya watu kadha na kujinyoosha kwenye sakafu huku nikikiweka kichwa katikati ya miguu hii, na muda si muda, msono wangu ulijiunga na kwaya ya wakoromaji iliyokuwa ikihanikiza nyimbo zake kule seli. Hebu fikiria, hata tuseme nilikuwa nimeshikwa katika hali ya kunifanya kushukiwa, ilikuwa ni haki kuwaweka watu seli na kuwafungia kwa kufuli, huku  choo chao kikiwa ni ndoo, ambayo yeyote aliye na haja huichuchumaia, huku wenzake wote mkiwa mashabiki wake? Mbona hawa washukiwa tayari walikuwa wameshaanza kuadhibiwa hata kabla ya mahakama kuwapata na hatia? Usijali kujua haya yalimalizikaje.

Usiombe kukutwa na askari ukiwa umekwama

Kisa kingine kilinipata wakati nikiwa barabarani na gofu la gari. Kama unauelewa mji wa Nairobi, kuna hii steji ya hospitali ya Kenyatta. Basi kufika hapo, gari likagoma. Nikajaribu kuliweka kando ili nilijulie hali lakini halikufika kando sana. Ilikuwa Jumapili usiku wa mwendo wa saa tatu hivi. Wakati huu huwa hakuna magari mengi barabarani. Basi niliweka taa za tahadhari na nikampigia fundi simu. Naye kwa bahati akawa yuko maeneo hayo, na akaahidi kufika hapo bila kuchelewa. Muda si muda, wakaja watumishi kwa wote. Mara moja walinishambulia, wakalisukuma gari hadi kando ya barabara na kupiga simu kwa gari la kuvuta. Muda mfupi baadaye, ile langa langa yao ya kuvuta magari ilikuja na kigari changu kikainuliwa juu, hadi kituo cha polisi cha Kilimani. Nililifuata baada ya fundi kufika na tukapata gari lishaegeshwa na kuandikiwa taarifa. Taarifa yenyewe ilisema kwamba mwenye gari alikuwa kalewa chakari, akawatusi askari na vilevile alikuwa akiendesha gari kiholela huku akiyazuia magari mengine. Nilishangaa jinsi mtu anavyoweza kuwa analiendesha kiholela gari ambalo limekwama. Nikashangaa tangu lini polisi akatusiwa na mwenye kutusi asile kofi, risasi na kuchukuliwa juujuu hadi kituoni mwao. Haja yao ilikuwa nini? Nilipie uvutwaji wa gari. Kesho yake, nilirudi na kulipa shilingi elfu mbili mia saba za Kenya kwa hiyo huduma ya kuvuta. Askari wakapata kivuno.

Askari wa kuvuta magari

Siku nyingine tena nimekwama. Wakati huu, nilikuwa karibu na kituo cha polisi cha Langata. Niliona magari ya kuvuta yakiwa hapo karibu, nje ya kituo cha polisi. Nilienda na kukuta wenyewe hawamo. Basi nikaingia kwenye kituo cha polisi kuwauliza juu ya watu hawa. Watumishi kwa wote walipiga simu na baada ya muda wakaja. Ajabu ni kwamba walipofika, askari alikuwa ni mmoja wa wale waliokuwa kazini kwenye lile gari la kuvuta. Basi nikafikiri ni kwa sababu ya usalama. Kumbe amekuja ili ajipatie sehemu yake ya ndovu huyu aliyekuwa ameanguka. Basi nilipoambiwa malipo waliyotaka wale waheshimiwa, niligomba nikakataa hata huduma zao na kuwafukuzilia mbali pamoja na askari wao. Baadaye walirudi na kuniambia kwamba bei ambayo nilikuwa nimeikazania mimi ilikuwa ndiyo bei halali, lakini kwa kuwa askari alikuwepo, yeye pia alitaka sehemu na ikabidi malipo yaende juu zaidi ili askari wote wa zamu kituoni wapewe kitu. Fikiria uko nchini mwako, unalipishwa kodi kila kona, kisha umepatwa na matatizo, na ni wakati wa usiku. Wale ambao unalipa kodi kuwasitiri ndio wanaotaka kukuumiza zaidi. Je bado nikanyage nchi yangu kwa nguvu na raha?

Umuhimu wa wahalifu nchini

Kama kwamba kapu langu lilikuwa bado halijajaa, mengine yakanipata tena. Nilikuwa nimetoka kunyoosha viungo kwenye eneo la makazi la Chuo Kikuu cha Nairobi. Ukijua ni mazoezi ya namna gani niliyokuwa nimetoka kufanya, huenda utanichekelea sana. Hili ni eneo ambalo ni kama nyumbani kwani nimesomea hapo kwa muda wa takriban miaka saba na huwa sina sababu yoyote ya kuhofu kutembea katika eneo hili. Basi siku hiyo saa mbili za usiku, nikawa naenda kuvuka lile daraja la chini linalovusha barabara ya Uhuru. Nilichokiona, ni watu wakinikaba koo na kuniangusha. Nia yao ilikuwa ni kuninyongea mle ndani darajani ambamo mna giza. Nilijaribu kutapatapa na nikafanikiwa kutoka nje ila bado nilinyongwa tu, nikapokonywa saa, simu, kibeti kilichosheheni pesa, kitambulisho, kadi ya benki na vitu vingine. Baada ya shughuli hii niliachwa pale niko hoi na nikapepesuka kama mlevi nikijitosa kwenye barabara ya Uhuru bila ya kujali magari. Huku nikiwa nimelowa kwa kuangushwa kwenye maji na kwa mvua iliyokuwa ikinyesha rasharasha, nilienda hadi kituo cha usalama cha chuo na kuripoti. Niliambiwa kwamba wanajua vizuri sana kuhusu sehemu hiyo. Nikauliza ni kwa nini usalama haujashughulikiwa hapo, wakaniambia kwamba hiyo ni kazi ya polisi. Nilienda hadi kituo cha polisi cha Central ambacho ni jirani ya chuo. Nikapiga ripoti. Polisi waliniambia kwamba wanajua sana mambo kuhusina na hiyo sehemu, kwamba walikuwa wamepokea habari nyingi sana kuhusiana na mahali hapo. Niliandikisha taarifa na kuondoka. Kesho yake nilikuja kuchukua stakabadhi za kuonyesha kwamba nimepoteza vitu vyangu, hasa kitambulisho. Kwa bahati nikamwona askari fulani ambaye tuna uhusiano wa kinasaba kwa mbali. Aliponiuliza kilichonileta kituoni, nilimwelezea yaliyonipata, na nikalirudia swali langu la ni kwa nini hawakulinda doria pale wakati walijua kwamba kunao vibaka. Askari ambaye ni mtu wa ukoo wangu kwa mbali aliniambia kwamba wakora ni muhimu katika jamii. Aliniambia kwamba bila ya kuwepo wakora, basi watu wangelikuwa tu na uhuru wa kutembea na kunywa pombe jinsi wanavyotaka. Nilipomwuliza kuna shida gani katika kufanya hivyo, sijui alinijibu nini. Alikuwa tayari keshaniudhi. Nikabaki kinywa kikavu pale katika kituo cha polisi cha Central, nikiwa na maumivu ya shingo huku kumeza mate kukiwa shida tupu, uso wangu ukiwa na mipapuriko ya kuangushwa na kupigwa kucha, mtumishi kwa wote akiwa ameniambia yote. Je, niendelee kuikanyaga nchi yangu kwa nguvu na raha?

Nitakachofanya kesho

Kutokana na hizi tajiriba zangu pamoja na zingine nyingi, siku ya kesho nitaitumia vizuri. Najua wengi wenu mtaenda kwenye kumbi mbali mbali ili mkajazwe uongo masikioni. Kwa muda wa majuma kadha sasa, nimekuwa nikiwaona wanajeshi ambao ni vijana wenye nguvu zao wakiwa wanashinda pale katika uwanja wa michezo wa Nyayo, wakipiga paredi mchana kutwa. Mbona twapoteza muda na rasilimali hivi? Naona pia anga zikipasuka kwa milio na miruko ya ndege aina ya Jet ambazo zinapiga mbizi angani ati kwa matayarisho ya siku kuu hiyo. Mbona hii siku haina maana kubwa kwetu mbali na kupiga paredi kwa wanajeshi wetu, huku wanasiasa wetu wakija kutuonyesha wake na waume zao na mavazi maridadi waliyovaa, pamoja na magari yao ya kutisha? Mbona tusiseme kwamba ili kuadhimisha siku hii mwaka huu, tuwe na mwezi mzima wa wanajeshi wetu kutusaidia katika kujenga barabara, daraja na kuhudumu katika hospitali zetu? Mbona tuwachukue watu wenye nguvu na ujuzi na kwa majuma matatu mazima tunawapigisha paredi kule uwanjani, na mifuko yao ya migongoni, virungu, bunduki, vifaru, magari ya deraya na majibwa wao? Ni aibu kwamba hadi kufikia sasa, mimi kama masikini wa nchi hii hata sina nambari. Wimbo ulisema sasa abautani tuko namba wani. Sijui hao sisi walikuwa ni kina nani, nilifikiri kwamba ni Waafrika wote ambao walikuwa wamekanyagiwa. Kumbe ni kundi fulani la wateule wachache.

Maombi yangu

Kwa hivyo Mkenya mwenzangu, utakapoisherehekea siku hii, kumbuka kwamba mimi nitakuwa nimejifungia kwangu nyumbani nikishughulika na mambo tofauti. Pengine nitasoma, nitunge shairi moja hivi au hadithi fupi. Kisa na maana ni kwamba sioni haja ya kusherehekea madaraka wakati ambapo siruhusiwi kukanyaga nchi yangu kwa nguvu na raha. Sioni ni lipi la kusherehekea na kuadhimisha ikiwa nimeonyeshwa mara nyingi kwamba ni haramu kutii sheria. Nyote nawatakieni siku kuu njema ya Madaraka. Maombi yangu ni kwamba siku moja, hata kama itakuwa muda mrefu baada ya uhai wangu, mzalendo wa nchi hii ataikanyaga nchi yake kwa nguvu na raha.

Amadi. 


5 Comments so far
Leave a comment

[…] pili mhandisi wa lugha Amadi , nakala yake na Sikukuu ya madaraka i hapa tena nafikiri ndio imeshika taswira ya mwananchi wa kawaida kuhusu maana haswa ya sikukuu hii ya madaraka na sikukuu zote za kitaifa . […]

Pingback by mawazo na mawaidha » taswira tofauti za madaraka

kwa kweli mkenya wa kawaida kamwe hatoweza kufurahia ukenya wake hadi mambo kadha wa kadha yatekelezwe. Ni uchungu mtupu tunaposikia baadhi ya mambo haya, siyo kwamba ni mageni lakini tunatamani yawe walau yamepungua. Kusikia mapolisi kuseme ati wahuni wanahitajika ili kurekebisha wakenya imekithiri kipimo….
Hongera kwa posti hii, imebidi nitoe kamusi yangu ambayo kajaa vumbi

Comment by wawuda

this story is a story that consane about me really from kenya teens

Comment by hanad

Miaka nane baadaye, maudhui ya haya maandishi bado yanasheheni. Mkenya halisi ni yule mwananchi wa kawaida, huyu ndiye anafaa kuikanyaga nchi yake Kenya kwa nguvu na raha. Lakini bado twatokomea kwenye lindi la kutokuwa na usawa. Mungu na atuonee sisi.

Comment by Lucas Wafula

Nani anajua majina ya mwenyeameimba,”Tushangilie Kenya taifa letu tukufu, ?”

Comment by Stella




Leave a comment